27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda aiundia kamati Machinga Complex

makonda-1Asifiwe George na Secilia Alex (A3), Dar es Salaam

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameunda kamati ndogo ya kuchambua na kupitia mkataba wa jengo la Machinga Complex lililopo Karume, ambayo itaanza kazi leo.

Makonda alizungumzia kuunda kamati hiyo Dar es Salaam jana, wakati wa ziara yake ya kukagua jengo hilo na kuangalia namna wafanyabiashara wanavyofanya shughuli zao kila siku.

Alisema jengo hilo ambalo lilijengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 12 zilizokopwa kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), hadi sasa linadaiwa Sh bilioni 36 kutoka uongozi wa Jiji la Dar es Salaam.

“Dk. Magufuli (Rais John) yupo kwa ajili ya kuwapigania wanyonge, tupo upande wake tunamuunga mkono, tutahakikisha wanaotetea  walarushwa na walioingia na kupewa vizimba kwa njia ya rushwa tutawakamata.

“Baada ya kumaliza kuchambua mikataba, tutaangalia nani wa kubaki kwenye vizimba na nani wa kuondoka kwa sababu kuna watu wakubwa kama mimi, wana vizimba zaidi ya 100 na hawavifanyii kazi, badala yake wamevikodisha kwa watu wengine tena kwa gharama kubwa hali inayosababisha watu kushindwa kuvikodi,” alisema.

Alisema sasa jengo hilo lililokuwa chini ya usimamizi wa Jiji la Dar es Salaam, amekabidhiwa Makonda na tayari amepewa taarifa kutoka kwa meneja wa jengo hilo ambaye hakumtaja jina lake.

Aliwataka wafanyabiashara kuacha kufanya biashara barabarani, badala yake wafike kwa viongozi husika ili wapewe eneo kwa ajili ya kuendelea na biashara zao.

“Wanaofanya biashara barabarani hawalipi kodi, idadi kubwa ya wanunuzi wanaishia nje, wanawanyonya wanaolipia kodi na biashara zao zinakuwa hazinunuliwi, kuanzia leo (jana) sitaki kuona mtu akifanya biashara barabarani,” alisema Makonda.

Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, aliifuta bodi ya usimamizi wa jengo hilo kutokana na kushindwa kulisimamia vizuri na kutojali wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles