Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amezitaka taasisi na mashirika ya umma mkoani hapa kuiunga mkono Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa kutumia mawasiliano yanayotolewa na kampuni hiyo.
Makonda alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana alipokuwa akizindua wiki ya huduma kwa wateja wa TTCL.
“Serikali imeonyesha nia njema ya kuirejesha TTCL katika hali nzuri baada ya kuimiliki kwa asilimia 100.
“Kwa hiyo litakuwa jambo la busara na la heshima kama mashirika na taasisi za umma zilizoko Dar es Salaam zitaunga mkono juhudi za Rais, Dk. John Magufuli za kuirejesha kampuni hiyo chini ya umiliki wa Serikali kwa asilimia 100.
“Katika hili, mimi kama kiongozi wa mkoa nitahakikisha ofisi zote za umma zilizopo chini yangu zinatumia huduma za TTCL kuimarisha uzalendo.
“Kama kuna ofisi yoyote ya umma itasita kutekeleza jambo hili, naomba mniambie niingilie kati kwa sababu hakuna sababu ya kutojali bidhaa zetu wenyewe,” alisema Makonda.
Makonda pia alizitaka taasisi za umma zinazodaiwa na kampuni hiyo zilipe madeni yao kampuni hiyo iweze kujiendesha kwa mafanikio.
“Kama wadaiwa watashindwa kulipa madeni yao basi wafikisheni mahakamani wakalipie huko,” aliagiza Makonda.
Naye Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, alisema TTCL ilianza mchakato wa kuleta mabadiliko tangu mwaka 2014 kwa mpango uliopewa jina la TTCL Business Transformation Project.
Kwa mujibu wa Kindamba, mpango huo ulilenga kuongeza utendaji na ufanisi katika uzalishaji na uwajibikaji kutoa huduma bora kwa wateja wa kampuni hiyo.
Kuhusu Wiki ya Huduma kwa Wateja, alisema inalenga kutambua na kuthamini mchango wa wateja ambao wamekuwa chachu ya kukua kampuni hiyo.