31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa kuchunguza madini ya gypsum

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa

Na MWANDISHI WETU, DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema atafuatilia ili ajue ni kwanini bidhaa za ‘gypsum’ zinazoagizwa kutoka nje ya nchi hazitozwi kodi.

Waziri Mkuu ametoa ahadi hiyo juzi mjini hapa wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Kiwanda cha Premalt Limited kinachotengeneza unga wa ‘gypsum’ aina ya Afri Bond, baada ya kukikagua kiwanda hicho kilichopo Zuzu, nje kidogo ya Mji wa Dodoma.

“ ‘Gypsum’ inayozalishwa Dodoma ina ubora kama ile inayozalishwa Mchinga kule Lindi na hakuna ‘gypsum’ yenye ubora kama huo hapa Afrika isipokuwa ‘gypsum’ ya Tanzania.

“Nilikuwa sielewi ni kwa nini ‘gypsum’ ya wenzetu ilikuwa inakimbiliwa, lakini sasa nimetambua kwamba ilikuwa na bei nafuu kwa sababu tumetoa kodi. Kwa hiyo, hili jambo nalibeba, nakwenda kulishughulikia.

“Nimeangalia kwenye orodha niliyopewa katika madini yote, nimekuta kodi ya ‘gypsum’ ni asilimia sifuri.

“Katika hili ni lazima tuweke kodi ili tutengeneze soko zuri kwa ‘gypsum’ inayozalishwa hapa nchini. Ni lazima tuweke kodi kwenye madini yetu mengine kama makaa ya mawe ili tutengeneze soko zuri,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema wakazi wa Dodoma wamepata fursa kutokana na uwepo wa kiwanda kama hicho kwani kiwanda kinahitaji mali ghafi, kwa hiyo ni jukumu la wakazi wake kuchangamkia fursa ya uchimbaji wa madini hayo.

Alitumia fursa hiyo pia kumpongeza mmiliki wa Kampuni ya STJ Enterprises, Adella Nungu, ambaye ni mmoja wa wajasiriamali wa Kitanzania wanaotumia ‘gypsum’ kutoka Dodoma na kutengeneza mapambo mbalimbali ya ndani ya nyumba.

Naye Nungu akizungumza mbele ya waziri Mkuu, alisema anaponunua unga wa ‘gypsum’ kutoka Dodoma, kwa wastani anaweza kutengeneza bidhaa za tani 20 hadi 25 kwa mwezi kutegemea na hali ya soko na mahitaji kutoka kwa wateja wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles