NA THERESIA GASPER, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez na msaidizi wake, Yeray Romero, leo wanatarajia kuanza rasmi kibarua cha kuinoa timu hiyo katika mazoezi yatakayofanyika Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Makocha hao raia wa Hispania, walirejea jijini Dar es Salaam juzi kwa ajili ya kuanza kazi rasmi baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kila mmoja baada ya kumalizika kwa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.
Aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Stewart Hall, msaidizi wake, Mario Marinica pamoja na mtaalamu wa viungo, Adrian Dobre, waliondolewa kwenye nafasi zao kutokana na kushindwa kufikia malengo ya kutwaa ubingwa msimu uliopita baada ya kupata matokeo yasiyoridhisha.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Jaffar Idd, alisema sasa wanaanza ukurasa mpya baada ya benchi la ufundi kufanyiwa mabadiliko kwa ajili ya maandalizi ya ligi msimu ujao.
“Kila mchezaji anatakiwa kujitambua na kufanya mazoezi kwa kujituma kipindi ili waweze kukubalika kwa makocha na kujihakikishia namba ya kucheza kikosi cha kwanza, kwani ushindani lazima utaongezeka msimu ujao,” alisema.
Pia aliwataka mashabiki kutoa ushirikiano na kuzidisha hamasa ambayo itaongeza morali kwa makocha wapya na wachezaji ili kukabiliana na changamoto za michuano mbalimbali.