23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Makanisa Tabora yaungana kuliombea Taifa

Na Allan Vicent, Tabora

Maaskofu, Wachungaji, Mapadre na waumini wa makanisa mbalimbali Mkoani Tabora wamefanya ibada ya pamoja kuliombea taifa ili amani, umoja, mshikamano na upendo viendelee kudumishwa miongoni mwa Watanzania wote.

Akizungumza katika ibada hiyo iliyofanyikia katika kanisa la KKKT-Tabora mjini Katibu wa Umoja huo, Askofu Elias Mbagata alisema kuwa ibada hiyo ni muhimu sana katika kudumisha imani, kujengana kiroho na kutiana moyo katika kipindi hiki ambacho taifa linaomboleza msiba wa Rais Dk. John Magufuli.

Alisema wamekutana ili kumwomba Mungu alinusuru taifa na roho zozote za uhalibifu, machafuko, rushwa, ikiwemo kuombea mchakato mzima wa kumpata Makamu wa Rais ili apatikane mtu sahihi aliyekusudiwa na Mungu.

Askofu Isaack Kisiri Laizer wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Magharibi Kati, Tabora alibainisha kuwa wamekutana kumwomba Mungu ili taifa liweze kuyasimamia na kuyaenzi kwa vitendo yale yote yaliyoanzishwa na hayati Dk. Magufuli.

Alisisitiza kuwa kifo cha Rais Magufuli kimemgusa kila mtu hivyo hawana budi kuungana na kumwomba Mungu ili alinusuru taifa na hila zozote za maadui wa maendeleo ikiwemo kuiombea faraja na utulivu familia ya marehemu.

Askofu mstaafu wa Kanisa la TAG-Kitete Christian Center, Paul Meivukie alisema kuwa Watanzania wanahitaji umoja wa kweli utakaoliwezesha taifa kuendelea kudumisha amani na mshikamano huku tukikataa ubaya na mambo yote yasiyofaa.

“Taifa linahitaji amani na mshikamano wa kweli, ndiyo maana tumeungana ili kumwomba Mungu atuepushe na migawanyiko ya aina yoyote ile na amwezeshe Rais wetu Samia Suluhu Hassan kufuata nyayo za mtangulizi wake,”alisema.

Mwakilishi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Padre Faustine Rwechungura alisema kuwa maombi hayo ni faraja kubwa kwa hayati Rais Magufuli kule aliko kwa sababu alimtanguliza Mungu katika kila jambo katika maisha yake yote.

Alimwomba Mungu awape tumaini, imani, faraja, awatunze na kuwalinda wanafamilia wote wa hayati Rais Magufuli.

Akizungumza katika ibada hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Dk. Philemon Sengati, Mkuu wa wilaya ya Kaliua, Abel Busalama alipongeza uamuzi wa watumishi hao kuungana na kuwaombea viongozi na taifa kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa serikali inathamini sana mchango wao katika suala zima la kudumisha amani, upendo na mshikamano wa wananchi hivyo akawataka kuendelea kumwomba Mungu ili kuliepusha taifa kwenye machafuko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles