26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Makamu wa Rais awasha umeme wa REA Kituo cha Afya Ketumbeine

*Aipongeza REA kusambaza umeme vijijini kwa ufanisi

*DG REA aeleza Shilingi Bilioni 73.9 zimewekezwa kutekeleza Miradi mitano ya umeme vijijini mkoani Arusha

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Isdor Mpango amewasha umeme katika Kituo cha Afya Ketumbeine, kilichopo katika kijiji cha Armanie wilayani Longido, Mkoa wa Arusha na kupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusambaza nishati hiyo kwa ufanisi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Isdor Mpango akibonyeza kitufe kuashiria kuwasha umeme kwa mara ya kwanza kwenye Kituo cha Afya cha Ketumbeine kilichopo katika kitongoji cha Irbilin, kijiji cha Armanie, Wilaya ya Longido mkoani Arusha, leo Februari 10, 2024.

Akizungumza leo Februari 10, 2024 na umati wa wananchi katika uwanja wa Kituo cha Afya Ketumbeine baada ya kuwasha umeme na kukizindua rasmi, Dk. Mpango amesema azma ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwapelekea wananchi maendeleo inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi na Serikali anayoiongoza.

“Nimefika hapa, kwanza tumewasha umeme kwa ajili ya kituo hiki cha Afya. Napenda niwapongeze sana watu wa REA kwa kazi nzuri. Sasa Kituo chetu cha Afya, nina hakika wananchi watakaokuja kupata huduma hapa watapata huduma ya uhakika,” amesema.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika Mkoa wa Arusha, mbele ya Makamu wa Rais, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa Serikali kupitia REA imewekeza jumla ya shilingi Bilioni 73.9 kwa Mkoa huo.

Amesema fedha hizo ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi mitano ya umeme vijijini ambapo jumla ya vijiji 263 kati ya 268 vya Mkoa wa Arusha vimekwishafikishiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, ikiwa ni asilimia 71.46.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Isdor Mpango (wa kwanza kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi, Hassan Saidy (mwenye fulana ya njano) pamoja na Viongozi wengine mbalimbali alipowasili katika hafla ya kuwasha umeme katika Kituo cha Afya Ketumbeine kilichopo katika kijiji cha Armanie, wilayani Longido Mkoa wa Arusha leo tarehe 10 Februari, 2024. Wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Fedha na Uhamasishaji Rasimali kutoka REA, CPA Daniel Mungure.

Mhandisi Saidy ameongeza kuwa, vijiji vilivyosalia vitaendelea kupelekewa umeme kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA na kwamba ifikapo Juni mwaka huu, vijiji vyote vitakuwa vimekwishafikiwa.

Ameitaja miradi mingine inayoendelea kutekelezwa na REA mkoani Arusha kuwa ni REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B, Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Migodi midogo na maeneo ya kilimo pamoja na Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.

Akifafanua zaidi, amesema kuhusu Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu, fungu la Kwanza limekamilishwa kwa asilimia 61 likihusisha uwashwaji wa vijiji 27 kati ya 44; na la Pili limekamilika kwa asilimia 95 likihusisha uwashwaji wa vijiji 58 kati ya 61.

Akizungumzia malengo ya kutekeleza Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B, Mkurugenzi Mkuu ameeleza kuwa unalenga kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha ambapo wigo wa kazi unahusisha kuyafikishia umeme maeneo 81 kwa gharama ya Sh Bilioni 11.

Kwa upande wa Mradi wa kupeleka umeme katika Migodi midogo na maeneo ya kilimo, wigo wa kazi unalenga kuifikia migodi na maeneo ya kilimo 27 kwa gharama ya Sh Bilioni 6.5.

Aidha, Mhandisi Saidy amesema kuwa Mradi wa kupeleka umeme katika Taasisi za Afya na Pampu za Maji unalenga kupeleka umeme katika maeneo hayo ambayo hayajafikiwa ili kupambana na magonjwa ya mlipuko ukiwemo UVIKO-19.

“Wigo wa kazi unahusisha kupeleka umeme katika pampu za maji 17 kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.5 na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 9 ambapo kazi ya ujenzi imefikia asilimia 97.”

Tukio la kuwasha umeme na kuzindua Kituo cha Afya limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, Maafisa wa Serikali pamoja na wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles