24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

MAKAMU WA RAIS AELEZA CHANGAMOTO ZA KUMSAIDIA JPM

 

Na Bakari Kimwanga-Aliyekuwa Zanzibar


SASA ni wakati wa kazi. Ni kauli ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa mara ya kwanza ameweka wazi namna anavyofanya kazi ya kumsaidia Rais Dk. John Magufuli, ili kufikia uchumi wa viwanda.

Alisema ili kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa wakati mwingine viongozi wa juu wa Serikali hulazimika kukesha ili kuhakikisha wanapanga mikakati thabiti ya kuliongoza Taifa.

Hata hivyo Makamu wa Rais alisema, bado taifa linakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo anashiriki vizuri kumsaidia Rais Magufuli katika kuzitatua, huku akitolea mfano kero za Muungano.

Kutokana na hali hiyo amesema suala hilo bado limekuwa likichangiwa na watendaji kutokana na kutotekeleza makubaliano yaliyofikiwa kwenye vikao.

Akizungumza katika mahojiano ya kwanza na Wahariri wa Gazeti la MTANZANIA nyumbani kwake Tunguu mjini Unguja, Zanzibar mwishoni mwa wiki, alisema tangu alipokuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) alikuta kero 13 ambazo kila mara walikuwa wakikutana na viongozi wa pande mbili na kuzitafutia ufumbuzi.

Alisema kero hizo zilizokuwa zimegawika katika mafungu matatu zikiwemo kero za kisiasa kwa mfano nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Serikali ya Muungano, kero za uchumi na ushirikishwaji nafasi za ajira kwenye wizara na taasisi za muungano, ushirikiano wa kifedha, mgawanyo wa fedha asilimia 4.5 ya Zanzibar.

Alisema pamoja na hali hiyo wakati wote hadi sasa umekuwa ukiibuka mjadala hasa kwa upande wa Zanzibar kuhoji fedha zao za iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977.

“Kwa sasa bado haijajulikana suala la fedha za Zanzibar zilikuwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika , Zanzibar walitaka kujua zilikuwa ngapi, zipo wapi kitu ambacho mpaka leo hakijatatuliwa,” alisema.

Msaidizi huyo namba moja wa Rais, alisema kutokana na hali hiyo ndiyo maana kupitia Bunge la Katiba  Iliyopendekezwa walihakikisha kila jambo linalohusu maslahi ya kila upande liliingizwa kwenye Katiba hiyo  kama njia ya kuyatambua kwa mujibu wa sheria.

“Si hilo tu hata suala la ushirikiano wa kifedha nalo liliingizwa pia katika Katiba inayopendekezwa ambayo kwa sasa mchakato wake umesimama. Na pale sisi kama Serikali tutakaposema sasa tunaanza basi itakuwa ni kazi ya kumalizia tu,” alisema Samia.

Alisema suala la mabadiliko ya sera za nje na ndani ni moja ya kazi wanayoifanya kama njia ya kuimarisha muungano ili uwe imara zaidi.

Alipoulizwa malalamiko yanayojitokeza kila wakati kuhusu kutozwa kwa ushuru wa forodha kwa bidhaa hasa zinazotoka Zanzibar kuja upande wa Tanzania Bara, Samia alisema kuwa suala hilo lilishafanyiwa kazi na kilichobaki ni utekelezaji kutoka kwa watendaji.

“Wapo waliokubali mageuzi na hili ni suala ambalo limekuwa likipigiwa kelele sana na kila mara nimekuwa nikikutana na mawaziri wa fedha wa pande zote (Zanzibar na Bara). Kwani hata sheria hii inayotumika ni ya miaka ya 1950  na wanashindwa kutekeleza hilo labda wana hofu.

“Hili si haki na hata katika kikao kilichopita niliagiza walirekebishe ila ninachokiona ni changamoto za utendaji tu,” alisema Samia

MISIMAMO YA WABUNGE

Alipoulizwa namna wabunge wa Zanzibar wanavyoshirikiana na kuwa kitu kimoja linapotokea suala linalohusu nchi yao, Samia alisema ni kweli jambo kama hilo hutokea linapotokea suala la kiuchumi lakini si katika misimamo ya kisiasa.

“Mfano linapotokea suala la uchumi wa Zanzibar ndani ya Bunge wote huwa kitu kimoja ila linapokuwa suala la Muungano kumezwa kwa upande mmoja hapo hutofautiana na kila mmoja husimamia msimamo wa chama chake.

“…wapo ambao huona Muungano hauna maslahi kwao na wengine husimama na kueleza faida za Muungano jambo ambalo ni jema kwa maslahi ya nchi yetu,” alisema

AKUMBUKA VIBALI KWA WABUNGE

Makamu wa Rais alisema alipokuwa Waziri wa Muungano alihakikisha anawaombea vibali wabunge kutoka Zanzibar ili waweze kuruhusiwa kuingiza magari yao upande wa Bara pindi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kibunge.

“Mfano nchi zinazotuzunguka Malawi, Kenya na Zambia wanapoingiza magari yao hawapati usumbufu kama wanaopata watu wetu hasa kutoka Zanzibar. Hili suala halihitaji kila wakati tulisimamie sisi viongozi maana lipo katika ngazi ya watendaji  wetu ambao ni mawaziri hasa wa fedha na makatibu wakuu wao,” alisema

Kutokana na hali hiyo alisema ameshawaelekeza wahusika wakutane mapema ili kulimaliza tatizo hilo likiwamo suala la ushuru wa forodha hasa kwa bidhaa zinatoka Zanzibar.

“Kwa mfano magari yanatoka Bara yanapoingia Zanzibar huingia bila usumbufu wowote ila yanayotoka Zanzibar kwenda Bara yanapofika upande wa pili hukutana na vikwazo,” alisema.

FEDHA ZA WAHISANI

Akizungumza suala la mgawanyo wa rasilimali fedha, hasa kutoka kwa nchi wahisani, alisema suala hilo bado nalo linaonekana changamoto hasa upande mmoja kuhisi unazidiwa na mwingine.

“Kwa sasa tuna mfuko mkuu wa bajeti ambao hapo awali wahisani walikuwa wakiingiza fedha zao kuchangia bajeti ya  Serikali.

“Lakini kwa sasa wengine hawafanyi hivyo kutokana na baadhi ya mambo ambayo wanahisi hawajapendezwa nayo likiwemo suala la Uchaguzi wa Zanzibar na badala yake sasa wanatoa fedha moja kwa moja miradi ya maendeleo.

“Leo kuna baadhi ya fedha zinazotolewa na wahisani ambao wengine hutoa kwa masharti. Tuna mfumo wa kuchangia bajeti kuu ya Serikali lakini hawaingizi fedha, bali kwa sasa huchagua miradi na kuisimamia, sasa hapo utakuta labda ni mradi wa kilimo kama tunavyojua kilimo sio suala la muungano na utakuta mfadhili anasema ameipa Tanzania fedha kumbe ni upande mmoja huu mwingine haujui.

“Kwa hiyo hilo nalo ni sehemu ya changamoto,  ndiyo maana hata kwenye kikao nilichokifanya hivi karibuni niliwaambia mawaziri, makatibu wakuu waache kusema pembeni walete hoja zao kwenye vikao rasmi,” alisema.

ALIPOTEULIWA MGOMBEA MWENZA

Kutokana na utendaji wake MTANZANIA ilitaka kujua siku alipoteuliwa kuwa mgombea Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alijisikiaje ?, Samia alivuta pumzi na kusema alijikuta akibubujikwa na machozi huku akitafakari.

“Nilitafakari sana na kujiuliza kwa nini nimeteuliwa mimi na si wengine Mungu wangu. Wapo waliokuwa wakijiuliza kwamba ataweza nafasi hiyo huku wengine wakiwa na matumaini ya kutimiziwa malengo yao (hasa wanawake) huku wakishindwa kujua mimi ni mmoja tu niliyekuwepo huku juu.

“Nilikaa na kisha nikajiuliza kwa nini Mwenyezi Mungu umenichagua mimi, baada ya hapo nikasema ewe Mungu ninakuachia wewe uniongoze. Kwani nchi ni kubwa wanawake wana matumaini makubwa na wewe lakini wakisahau  mimi ni mmoja na nipo peke yangu kule juu.

“Ukija kwa watu wa NGO’s, Ulingo, TGNP. Ulingo wana malengo yao ya kisiasa na TGNP ni wanaharakati wa usawa wa kijinsia. Na wote hao wananiangalia mimi mmoja kwa kunitegemea kusukuma mbele ajenda zao kumbe mimi mmoja siwezi kufanya yote. Hivyo kila mmoja anatakiwa kufanya kwa nafasi yake ikiwemo mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi ambao ni wanawake nao wanatakiwa kuliona hilo”…….

Kwa habari zaidi, jipatie nakala yako ya MTANZANIA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles