24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Makali ya risiti yaanza kung’ata

Na WAANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

HATIMAYE makali ya Serikali ya kuwataka wafanyabiashra kutoa risiti kwa wateja wao, yameanza kung’ata, baada ya wafanyabiashara wawili kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini Sh milioni 1.5 kila mmoja.

Walitiwa hatiani jana na Mahakama ya Wilaya ya Ilala, baada ya kukiri kushindwa kutoa risiti na kutokuwa na mashine za kielektroniki (EFD’s).

Wafanyabiashara hao, Mustapha Adamjee (44) na Yahaya Kimaro (44) walikamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Machi, mwaka huu kwa nyakati tofauti.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Saidi Mkasiwa, alisema kutokana na washtakiwa kukiri makosa yao, wanatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 1.5 kila mmoja au jela miaka mitatu. Walilipa faini.

Awali, akisoma mashtaka hayo, Wakili wa TRA, Helord Angomi, alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza, Adamjee, alitenda kosa Machi 23, mwaka huu kwa kuuza magodoro matatu yenye thamani ya Sh 759,000 kwenye duka lake lililoko Mtaa wa Uhuru, Kariakoo bila kutoa risiti.

Naye Wakili Amandius Ndayezaa alidai kuwa mshtakiwa wa pili, Kimaro, Machi 14, mwaka huu, alikutwa akiwa hana mashine ya EFD’s kwenye duka lake lililopo Mtaa wa Kongo/Mchikichi bila ya kuwa na sababu za msingi.

 

TAASISI ZA SERIKALI

Katika hatua nyingine, TRA imezitaka taasisi zote za Serikali ambazo zinafanya biashara na kuingizia mapato zaidi ya Sh milioni 100, kuanza  kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Kamishna wa Walipa Kodi Wakubwa, Neema Mrema, alisema hayo jana Dar es Salaam wakati TRA ilipotangaza makusanyo ya mapato ya mwezi Aprili hadi Juni, katika kipindi cha mwaka 2015/16.

Alisema Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Mipango, imezitaka taasisi hizo kutumia mashine za kielektroniki (EFDs).

“Mfano wa taasisi hizo ni kama Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Suma JKT,” alisema Kamishna Neema na kuongeza kuwa pia wameanza utekelezaji wa kukusanya VAT kutoka makampuni ya utalii.

Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, alisema baada ya kuziba mianya ya upotevu wa mapato, wamefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh tril. 1.414 sawa na asilimia 107.83 wakati lengo lilikuwa ni kukusanya Sh tril. 1.311 katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni cha mwaka wa fedha wa 2015/16.

Alisema katika mwaka mzima wa fedha wa 2015/16, TRA imefanikiwa kukusanya Sh tril. 13.371 sawa na asilimia 100.04 wakati lengo la Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar lilikuwa kukusanya Sh tril. 13.366.

 

BEI YA MAFUTA JUU

Nayo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo ya bidhaa za mafuta.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, ilisema bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa imeongezeka na zitaanza kutumika kuanzia leo.

Alisema bei ya rejareja kwa mwezi Julai, petroli ni Sh 23 kwa lita sawa na asilimia 1.26, dizeli Sh 88 kwa lita sawa na asilimia 5.36 na mafuta ya taa Sh 80 kwa lita sawa na asilimia 5.01 kwa kulinganisha na mwezi uliopita.

 

KAMATAKAMATA

Taarifa zaidi zinasema kikosi kazi maalumu cha vyombo vya dola, kinaendelea na kamatakamata dhidi ya wafanyabiashara wanaodaiwa kuwa kwenye mtandao wa ukwepaji kodi na utengenezaji wa stakabadhi feki, huku kilio kikitawala kwa wafanyabiashara wa Arusha na Dar es Salaam.

Idadi ya wafanyabiashara hao waliokamatwa katika msako huo, imeongezeka na kufikia zaidi ya 10 hadi kufika jana.

Chanzo cha kuaminika jijini Arusha kililiambia MTANZANIA kuwa wafanyabiashara wawili walikamatwa Julai 2, mwaka huu na kulazwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi.

Wafanyabiashara hao ambao majina yao yamehifadhiwa walikamatwa na kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam.

Mmoja wafanyabiashara hao ni mmiliki wa kampuni za ujenzi na huduma za kusambaza mafuta kwenye minara ya kampuni za simu.

Meneja wa TRA, Apili Mbarouk, alipoulizwa kuhusua suala hilo alisema hana taarifa za tukio hilo.

 

KAMBI TAKUKURU

Mkurugenzi wa Takukuru, Valentino Mlowola, alipotafutwa kwa njia ya simu kutoa ufafanuzi, alimtaka mwandishi kuwasiliana na Msemaji wa Takukuru kwa ufafanuzi zaidi ambaye alipoulizwa alisema hana mamlaka ya luzungumzia suala hilo.

Bunge lililomalizika wiki iliyopita lilipita sheria ya fedha ya mwaka 2016 ambayo pamoja na mambo mengine mtu atakayeshindwa kutoa au kudai risiti anakabiliwa na adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela au faini isiyopungua Sh milioni 3.

Imeandaliwa na Faraja Masinde, Koku David, Veronica Romwald na Hamidu Abdallah (DSJ)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles