27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

MAKALA; Umuhimu wa Elimu na Huduma ya Uzazi wa Mpango kwa Makundi Maalumu

Na Yohana Paul, Geita

MAKUNDI maalumu yanajumuisha watu wenye ulemavu mwilini unaowapa changamoto ya kuishi ama kupata huduma za kijamii na kushindwa kumudu shughuli za kiuchumi na kisiasa kama ilivyo kwa watu wengine.

Katiba ya serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uwepo wa makundi ya watu wenye ulemavu na kuagiza walio katika makundi haya kupewa kipaumbele cha huduma za elimu, afya na sekta zingine.

Uzazi wa Mpango ni miongoni mwa huduma za afya ya uzazi wanazostahili watu walio kwenye makundi haya ili  kusaidia na kuwezesha kufikiwa lengo la kitaifa la uzazi salama na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Walemavu wa Macho   

Akizungumuzia hali ya huduma na elimu ya uzazi wa mpango kwa kundi maalumu la watu wenye ulemavu wa macho,   Mwenyekiti wa Chama Cha Wasioona Mkoani Geita (TLB) Paul Nyanda anasema kundi hilo lina uhitaji mkubwa wa huduma hiyo.

Nyanda anasema mbali na umuhimu wa elimu ya uzazi, tatizo lililopo ni njia ya mawasiliano inayotumika na kuwafanya kushindwa kupata elimu hiyo kwa undani kwani ujumbe wanaotegemea zaidi ni kupitia masikio na siyo macho.

Anasema kundi lao linahitaji kueleweshwa kwa undani zaidi jinsi ya kutumia njia salama na rafiki za uzazi wa mpango kwa kuwa wanasikia tu kupitia vyombo vya habari na wanakosa ufafanuzi.

“Kwa utafiti wangu, elimu hii bado haijawa kamili, asilimia kubwa jamii yetu imetengwa mpaka sasa, labda wajitokeze wadau, maana mahitaji ya elimu hii kwa kundi letu ni makubwa sana, na bado mwamko wa uelimishaji kwa kundi hili ni mdogo,” anasema.

Anaeleza, iwapo elimu  itawafikia kwa ufasaha watu walio na ulemavu ikiwemo wasioona itawasaidia kuwaongezea uelewa njia sahihi za kuepuka kuzaa bila mpangilio na hata kung’amua idadi ya watoto na kupunguza majukumu. 

“Juzi nimekutana na dada mmoja, mwenye ulemavu na umri wa miaka 21 ana watoto wanne, kila mmoja na baba yake, nikamufahamisha aende kuongea na manesi, kujilinda asiendelee kuzaa, amefanikiwa kuweka njiti na anakiri zimemusaidia,” anasema Nyanda.

Nyanda anatoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu ya uzazi wa mpango na hata wadau kuitisha semina kwani wao wapo tayari kushiriki kwa imani kuwa elimu hiyo itawawezesha kumudu familia zao na kuacha kuranda randa mitaani.

Walemavu wa Viungo

Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Viungo mkoani Geita, Kelfrin Zephania, anasema uhitaji wa elimu afya ya uzazi ni mkubwa kwa kundi lao ila  kikwazo ni elimu na huduma ya uzazi wa mpango kupatikana zahanati na vituo vya afya pekee ambapo ni vigumu kwao kufika.    

“Wananchama wetu wengi hawawezi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, kwa hiyo elimu kuipata inakuwa siyo rahisi, hivo kukutana na changamoto ya kubeba mimba zisizotarajiwa na kuishia kutelekezwa.

“Mtu akishabebesha mimba anaona aibu kuonekana amemubebesha mimba mlemavu, anamtenga,  kumupata baba wa mtoto  inakuwa shida, changamoto kubwa ndio hiyo. 

“Ikitolewa elimu itasaidia sana kwa sababu walemavu wa viungo kuipata siyo rahisi kwani hawana uwezo wa kuzunguka kwenye mikutano,” anasema Kelfrin.

Anapendekeza uwepo utaratibu mzuri kwa maafisa wa afya kutoa semina ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kuwawezesha kujitambua, kujiamini, na hata kuwa huru na furaha pale wanapokuwa kwenye mahusiano.

Anashauri elimu hiyo iambatanishwe na elimu ya kujikinga na magonjwa ya zinaa kwani ni wazi kwamba walemavu wengi wa viungo wanaishi na magonjwa hayo bila kujua nini cha kufanya kutokana na kukosa elimu

“Tumeshawashuhudia wengi, wanajutia, walikuwa hawatarajii, muhusika anakutana kimwili na mtu, anaishia kupata ujauzito na wote walikuwa hawategemei, kwa hiyo ikiwezekana elimu ianze kwa viongozi nasi tutaweza kuwasambazia,” anaongeza.

Walemavu wa Ngozi

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Watu wenye Changamoto ya rangi ya Ngozi mkoani hapa, Leah Magesa anasema kundi lao kwa kiwango fulani limeanza kushirikishwa na kwa kiasi fulani mwamko umeanza kuonekana.

Leah anaeleza kuwa elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango imeanza kuenea kwa kundi lao kutokana na mabadiliko ya mila na desturi potofu na sasa walemavu wa ngozi wanaingia kwenye mahusiano na kuhudhuria kliniki kama watu wengine. 

Anasema awali watu wengi walikuwa hawana uelewa juu ya elimu hiyo kwa kuwa kundi lao lilitengwa na hawakuweza kupata nafasi ya kuchangamana kama ilivyo sasa.

Leah anakiri kwamba uwepo wa mikopo ya ujasiliamali kwa kundi hilo pia imekuwa na msaada mkubwa hususani katika kupunguza mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwani walikuwa tayari kufanya mapenzi wakiamini watapata chochote.

“Nasi tunawakumbusha wenzetu wawe tayari kuzaa mtoto na mtu ambaye tu ataridhia na atakuwa tayari kulea, tunawaambia wasikubali ovyo kwa sababu ya fedha, ndiyo maana halmashauri imetenga asilimia mbili kuwakopesha.

“Nami kama kiongozi mara kwa mara nazungukia vikundi, kuwaeleza na kuwakumbusha wasije kuishia kudanganywa kingono, na tunawaelimisha ikiwezekana watumie kondomu na tunaendelea kutoa elimu, kila baada ya kikao lazima tuongelee uzazi wa mpango,” anasema Leah.

Anaeleza, kwa wale ambao bado wana hofu ya kutumia uzazi wa mpango wa kisasa basi wanaelimishwa kutumia njia ya asili kwa maana ya kuzingatia na kufuata  kalenda ingawa wengi hawaielewi basi wanaendelea kuwashawishi watumie vipandikizi, vidonge na vitanzi.

“Mashirika yasiyo ya kiserikali yasaidie kusogeza huduma ya afya ya uzazi hasa kwa makundi maalumu, wasiishie kutoa misaada tu, maana uzazi wa mpango ndio utapunguza gharama za maisha kwa watu wenye ulemavu,” anashauri.

Leah anaiopongeza serikali kwa kuleta Bima ya Afya iliyoboreshwa (CHF) inayohusisha watu sita ambapo imewasaidia kudhuru kliniki na vituo vya afya na hata kusaidiwa jinsi ya kupangilia watoto kupitia bima hiyo.

Mtazamo wa SHIVYAWATA

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Nchini (SHIVYAWATA) kwa mkoa wa Geita, Majaliwa Masaka anasema kwa hali halisi makundi ya walemavu ni kama yametengwa kwenye suala la elimu ya afya ya uzazi pasipo kujua nao wana haki ya kuipata.

“Kuna changamoto moja inayojitokeza, kuna baadhi ya mambo hatushirikishwi, labda wanashirikishwa watu ambao wala siyo viongozi, au wanashirikishwa watu wachache, ila siyo viongozi na wala siyo wawakilishi wa hilo kundi letu.

“Hii elimu tunaihitaji itatusaidia kujikinga na magonjwa ya zinaa, mimba za utotoni, kuzaa watoto wengi bila mipango maana kuikosa imesababisha wengi wetu kupata mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa,” anaeleza Majaliwa.

Anasema imefika wakati sasa kwa elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kuwekewa mkazo kwa watu wenye ulemavu kwani nao wanayo haki ya kuingia kwenye mahusiano, kuwa kwenye ndoa na kuzaa kama ilivyo kwa wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles