29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Umuhimu wa chakula kwa watoto katika shule za awali

Na Samweli Mwanga, Maswa

Shule ya awali ni kituo cha kuwalelea au kuwasomesha watoto wadogo ambao hawajaanza elimu ya msingi (darasa la kwanza)na kwa sasa Serikali imeagiza kwa shule zote za msingi zinazomilikiwa na serikali zimetakiwa kuwa na madarasa ya wanafunzi wa awali.

Na kwa msingi huo hata miundo mipya ya idara za serikali katika halmashauri za wilaya ambazo ndizo ziko karibu wa wananchi kumeanzishwa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi.

Katika vituo vya shule ya awali, mara nyingi watoto huwa na umri kati ya miaka 2 mpaka 6 au zaidi kidogo. Umri huo ni muhimu sana kwa maendeleo ya mtoto, kimwili na kiroho. 

Chakula kina nafasi kubwa ya kumjenga mtoto kimwili na wengine wanasema hata kiroho. Kwa hiyo, umuhimu wa chakula katika vituo hivyo ni jambo lililowazi. 

Hata hivyo, kwa vile bado kuna baadhi ya shule za awali hasa wazazi ambao wanaona kuwa suala la chakula katika vituo vyao si muhimu na litaongeza gharama.

Lakini ni lazima jamii izinduliwe hasa wazazi wa aina hiyo kwa kuielimisha jamii kwa ujumla juu ya dhana ya chakula katika shule ya awali. 

“Kuna Wazazi bado wanaona chakula kwa wanafunzi wa awali kuwa ni gharama hivyo wanapaswa kuelimishwa juu ya umuhimu wa chakula kwa wanafunzi hao katika kujifunza sambamba na makuzi yao,” amesema Mwl Rose Joseph wa Shule ya Awali Magereza wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.

Amesema  tunacho kula kina faida kubwa moja, nayo ni kutupatia virutubisho (nutrients) hivyo virutubisho vina kazi kubwa tatu mwilini.

Mwl Rose anazitaja kazi hizo huku akibainisha ya kuwa kazi ya kwanza ni kujenga mwili huku akitolea  mfano kuwa watu wote tuna jua kuwa binadamu kwa hali ya kawaida huzaliwa na baba na mama.

Anasema anapozaliwa huwa ni mdogo na hapo tunamwita mtoto mchanga. Baada ya miaka kadhaa huwa mkubwa na kuweza kufanya mambo yake mwenyewe. Mwanaadamu kama huyo anaweza kuongezeka umbo, kutoka mtoto na kuwa mkubwa kwa sababu ya virutubisho vinavyotokana na vyakula tunavyokula. 

Kazi ya pili ya virutubisho ni kuupa mwili nguvu na joto. Mambo au kazi mbalimbali zinazofanywa na binadamu zinawezeshwa na nguvu (energy) inayotokana na virutubisho. Kutembea, kuongea, kulia, kubeba mizigo, kusoma ni baadhi tu ya kazi hizo. 
Kazi ya tatu ya virutubisho ni kulinda mwili usipate magonjwa. 

“Ulaji duni na magonjwa ni sababu kubwa zinazosababisha vifo vingi kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika nchi hasa za ulimwengu wa tatu ikiwemo Tanzania,” amesema.

Mwl Rose anasema kuwa taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na mambo ya watoto (UNICEF) ya mwaka 1990 inaonyesha kuwa watoto 176 kati ya 1,000 wanaozaliwa Tanzania hufa kila mwaka kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano. 

Naye Mkuu wa Divisheni ya Shule za Awali na Msingi,Mwl Lucy Kulongwa amesema kuwa ni muhimu watoto katika shule ya awali (madarasa, chekechea) wapatiwe chakula cha kutosha, safi na salama na kilicho mlo kamili (balanced diet).

Amesema hii  ni kwa sababu baadhi yao wanatoka nyumbani bila kula chakula chochote na wengine wanakaa mbali, wanapoteza muda mwingi njiani kabla ya kufika nyumbani. 

“Katika kutayarisha chakula cha watoto wa shule ya awali, mwalimu au mlezi lazima azingatie mafungu makuu ya chakula  ambayo ni chakula cha kujenga mwili, chakula cha kuupa mwili nguvu na joto pamoja na chakula cha kulinda mwili,”amesema.

Amesema chakula cha kujenga mwili  ni muhimu sana kwa watoto wa shule ya awali. Hii ni kwa sababu mwili wake (pamoja na akili) unahitaji kujengeka na kukua. 

Mwl Kulongwa amessma vyakula vinavyojenga mwili ni kama vile maziwa, nyama, samaki, mayai, senene, ndege, maharage, choroko, soya, njegere na  karanga  
Pia amesema kuwa watoto hufanya shughuli mbalimbali kama vile kucheza, kusoma, kukimbia ili mwili uweze kumudu kazi hizo na zile za kujenga mwili, lazima mwili upate vyakula vyenye kutoa nguvu huku akivitaja vyakula hivyo  kuwa ni mchele, viazi, mahindi, mtama, ndizi, karanga, alizeti, samli, siagi, asali na mihogo hivyo vyote kuupa mwili nguvu na joto.

Amesema vyakula vya kulinda mwili hivi  husaidia kulinda mwili wa mtoto asipatwe na magonjwa mbalimbali huku akitolea mfano wa vyakula hivyo ni kama vile mbogaamboga (mboga za majani, nyanya, karoti) na matunda mbalimbali, embe, machungwa, mananasi, papai, ubuyu, ukwaju).

“Zaidi ya makundi hayo ya vyakula, watoto wa shule za awali lazima wapatiwe maji safi na salama  yaliyochemshwa na kuchunjwa na kuhifadhiwa katika chombo safi,” amesema.

Hivyo ni matarajio makubwa kwa wamiliki wa shule hizi za awali hasa zilizo nyingi zinamilikiwa na watu binafsi wakiwemo wazazi na jamii kwa ujumla wataendelea kutoa chakula bora na maji safi na salama kwa watoto wetu na wale ambao bado hawajaanza kutoa huduma hiyo wataanza sasa la sivyo tuaathiri ukuaji wa watoto hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles