24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Ulinzi ni muhimu kwa Watoto

Na Samwel Mwanga, Simiyu

Watoto wote wana haki ya kulindwa. Kila mtoto ana haki ya kuishi, kuwa salama, kuwa na wazazi au walezi, kusikilizwa, kupata huduma muhimu na kukua katika mazingira salama.

Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyi, Elizabeth Mushi amesema familia ndicho chanzo cha awali cha ulinzi wa mtoto kwani wao ndiyo wenye jukumu la kutengeneza mazingira ya nyumbani.

“Familia ndicho chanzo cha ulinzi wa mtoto, wazazi au walezi wengine wana jukumu la msingi la kutengeneza mazingira ya nyumbani ambayo ni salama na yenye upendo pia shule na jamii ina jukumu la kutengeneza mazingira ya nje ya nyumbani ambayo ni salama na rafiki kwa mtoto,” amesema Elizabeth.

Amefafanua kuwa kwa isivyo bahati takwimu mbimbali zinaonyesha mamilioni ya watoto hawana ulinzi. 

“Kupitia vyombo vya habari zipo habari zinazoripotiwa kila siku zinazohusu watoto wengi wanakabiliwa na ukatili, unyanyasaji, utelekezwaji, unyonyaji, utengwaji au ubaguzi. 

“Aina hii ya ukiukwaji wa haki za watoto hupunguza uwezekano wao wa kuishi, kukua vizuri na kufikia ndoto zao.

“Zaidi ya watoto milioni 160 hutumikishwa badala ya kufurahia utoto wao duniani, aidha inakadiriwa kwamba zaidi ya watoto milioni 160 wa umri wa miaka 5–14 wanatumikishwa katika ajira za watoto. Mamilioni ya watoto, hususan wasichana wanafanya kazi za nyumbani kwa watu binafsi na zaidi ya watoto milioni moja husafirishwa kila mwaka,” amesema Elizabeth.

Ameshauri kuwa ni vema wasichana na wavulana wakahimizwa na wasaidiwe ili wazungumze kuhusu utetezi wa haki zao kama watoto. 

“Vijana hawana budi kuwa msitari wa mbele katika ulinzi wao wenyewe dhidi ya unyanyasaji, ukatili, unyonyaji na ubaguzi.

 
“Kila mtoto ana haki ya kukulia katika familia. Endapo familia haina uwezo wa kumhudumia mtoto, mamlaka katika jamii husika yachukue hatua ya kujua sababu za hali hiyo na yafanye kila juhudi ili kuiwezesha familia husika iendelee kuwa pamoja.

 
“Kila mtoto ana haki ya kuwa na jina. Kila mtoto ana haki ya kuwa na utaifa. Kusajili uzazi wa mtoto husaidia kumhakikishia haki yake ya kupata elimu, huduma za afya pamoja na huduma za kisheria na za kijamii,” anasema Elizabeth.

Anafafanua zaidi kuwa Duniani kote, uzazi wa takribani watoto milioni 230 wa umri wa chini ya miaka mitano haukusajiliwa mahali popote. Kusajili uzazi wa mtoto ni hatua muhimu katika kumlinda mtoto dhidi ya unyanyasaji na unyonyaji.

“Baada ya kuona tatizo hilo serikali yetu ya Tanzania kwa sasa kila mtoto anayezaliwa katika kituo cha afya ni lazima sasa asajiliwe kwa Msajili wa Vizazi na Vifo.

“Watoto wadogo wa jinsi zote yaani wakike na wakiume hawana budi kulindwa dhidi ya aina zote za ukatili na unyanyasaji,” anasema Elizabeth. 

Amefafanua zaidi kuwa ukatili ni pamoja na unyanyasaji wa kimwili, kingono na kihisia, utelekezwaji na kutendewa matendo hatarishi kama vile ndoa za utotoni na ukeketaji nakwamba familia, jamii na mamlaka ni lazima ziwajibike katika ulinzi dhidi ya ukatili huo.

 
“Watoto walindwe dhidi ya aina yoyote ya kazi za hatari. Kazi zisiwanyime watoto kwenda shule. Watoto wasitumikishwe kabisa kwenye ajira mbaya kama vila utumwani, kazi za kushurutishwa, uzalishaji na uuzaji wa dawa za kulevya.

 
“Wasichana na wavulana wanaweza kufanyiwa ukatili na unyanyasaji wa kingono katika maeneo ya nyumbani, shuleni, kazini au ndani ya jamii. Ni lazima hatua zichukuliwe kuzuia hali hiyo,” amesema Elizabeth. 

Ameongeza kuwa watoto waliofanyiwa vitendo vya unyanyasaji na unyonyaji wa kingono wanahitaji msaada wa haraka wa kuwawezesha kuondokana na hali hiyo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima.

Watoto wote wana haki ya kupata habari zinazoendana na umri wao, kusikilizwa na kushirikishwa katika kufikia maamuzi yanayowahusu. Kutekelezwa kwa haki hii huwezesha watoto kushiriki kikamilifu katika masuala ya ulinzi wao dhidi ya unyanyasaji, ukatili na unyonyaji, pamoja na kuwa raia wenye kujali wajibu

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles