*Vijana washindwa kujiajiri katika sekta ya kilimo
*Wananchi wabaki njia panda, Serikali yaeleza
Na Ashura Kazinja, Morogoro
UPATIKANAJI wa ajira nchini umeendelea kuwa mgumu mwaka hadi mwaka huku kukiwa na vijana wengi wanaohangaika mtaani kutafuta kazi bila mafanikio na hivyo kubaki wakiwa hawajui la kufanya.
Machi 3, mwaka huu, Serikali kupitia Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Patrobas Katambi, ilieleza kuwa vijana milioni 1.7 wenye uwezo wa kufanya kazi hawana ajira. Kiwango hicho ni asilimia 12.2 ya vijana wenye umri wa miaka 15-35.
Kutokana na changamoto hiyo wengi wamekuwa wakijaribu upande wa pili wa Shilingi kwa kujaribu kujikita kwenye kilimo bila mafanikio kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha, hali ya mvua imeenda ikibadilika na kutokuwa ya kutegemewa kwa ajili ya kilimo kutokana na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kufanya kilimo kuwa cha kubahatisha tofauti na zamani, hali iliyopelekea serikali kuamua kujenga skimu za umwagiliaji katika maeneo tofauti nchini ili kuongeza tija na usalama wa chakula nchini.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe anabainisha katika Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya Mwaka 2023/2024 kuwa Sekta ya kilimo katika mwaka wa 2021 ilikua kwa asilimia 3.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.9 mwaka 2020.
“Vilevile sekta ya kilimo imechengia asilimia 26.1 katika pato la taifa; imetoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda na asilimia 100 ya chakula nchini,” anasema Waziri Bashe.
Wakati Waziri Bashe akibainisha hayo, Dira ya Taifa 2025 inaeleza kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kutegemea zaidi kilimo licha ya mchango wake katika pato la taifa kuendelea kushuka, na kwamba kilimo kinaajiri takribani asilimia 66.3 ya nguvu kazi ambayo wanawake ni asilimia 52 na wanaume asilimia 48.
Soma pia: https://mtanzania.co.tz/makala-skimu-ya-umwagiliaji-morogoro-yakwama-kwa-zaidi-ya-miaka-10/
Aidha, malengo makuu matano yaliyoainishwa kwenye dira ya maendeleo ya Taifa 2025 ni pamoja na kuboresha hali ya maisha ya Watanzania na kujenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine.
Vijana wa kata ya Rudewa wilayani Kilosa mkoani Morogoro ambao wanategemea kilimo kama ajira yao kuu ni miongoni mwa wale wanaoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo kuwafanya kuishi bila kazi ya kuwawezesha kupata kipato cha kujikimu kimaisha wao na familia zao na kubaki kuwa tegemezi kwa wazazi na walezi wao.
Matumaini yao ya kujiendeleza kwa kilimo yamekatishwa tamaa na mradi wa skimu ya umwagiliaji iliyokwama kukamilika kwa zaidi ya miaka kumi na mbili sasa na hivyo kuwafanya wakazi zaidi ya 11,000 wa vitongoji vitatu vya Rudewa Batini, Mbuyuni na Gongoni hususani vijana ambao ni wengi kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.
Kukwama kwa skimu hiyo kwa muda mrefu kumeathiri pakubwa maisha ya vijana hao na hivyo nguvu kazi ya Taifa kupotea bure kwani wamekuwa wakishinda vijiweni na nyumbani bila kazi maalum wala vibarua vya kufanya kutokana na hali ngumu ya maisha katika vitongoji hivyo.
Mkulima na mkazi wa Rudewa Batini, Mohamed Mtalame Maarufu Mzee Mobutu, anaeleza kuwa kutokamilika kwa wakati kwa skimu ya umwagiliaji kijijini hapo imewafanya kuishi maisha magumu kwa muda mrefu hususani vijana huku wakiwa hawajui hatima ya maisha yao kiuchumi, chakula na hata namna ya kutunza familia zao kutokana na kilimo wanachokitegemea kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi.
“Mwaka jana tulikosa kabisa mazao. Tunategemea mvua lakini mvua yenyewe hakuna, haieleweki, bei ya chakula iko juu, lakini kungekuwa na skimu ya umwagiliaji sasa hivi mambo yangekuwa mazuri watu wangeweza kuvuna mara mbili au tatu kwa mwaka,” anasema Mobutu.
“Mwaka jana tulikosa kabisa mazao. Tunategemea mvua lakini mvua yenyewe hakuna, haieleweki, bei ya chakula iko juu, lakini kungekuwa na skimu ya umwagiliaji sasa hivi mambo yangekuwa mazuri watu wangeweza kuvuna mara mbili au tatu kwa mwaka,” anasema Mobutu.
Mobutu anasema kuwa vijana wengi kijijini hapo wanahangaika na maisha huku wengine wakibaki nyumbani na wazee kutokana na kukosa ajira na kazi za kufanya mashambani, na kwamba hata vibarua imekuwa ngumu kwao kupata kutokana na hali ya kiuchumi kwa wananchi kuwa ngumu.
“Vijana wanahangaika sana hakuna ajira wala vibarua, nani akupe kibarua wakati yeye mwenyewe hajapata, tunateseka sana hali ya mazao imekuwa ngumu, kungekuwa na skimu ya umwagiliaji mtu angeweza kujitahidi na vijana wengi wangepata kazi na kujiajiri kwenye kilimo mashambani,” anasema Mzee Mobutu.
Nae, Mwenyekiti wa Kijiji cha Rudewa Batini, Hamadi Maboga, anasema kuwa kukwama kwa mradi huo kwa zaidi ya miaka kumi na mbili kumepelekea changamoto mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi kwa wananchi wake huku vijana ambao wengi wao wanategemea kilimo kujipatia kipato wakiwa hawana ajira ya kueleweka.
Maboga anasema kuwa kwa sasa wao kama viongozi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kuchangisha michango mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao kutokana na hali ya uchumi ya wananchi ambao wengi wao ni vijana kuwa ngumu kwani hata fedha za kujikimu wao wenyewe hawana.
Mkazi wa Rudewa Batini, Yunus Kasim anasema wananchi wa Rudewa wanamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kupitia wizara ya kilimo kuwafikiria kwani hata hiyo skimu ikikamilika haitoshi, na kwamba wananchi wa Rudewa wanategemea kilimo kujiajiri hususan vijana.
Diwani
Diwani kata ya Rudewa, Subiri Joseph Mwamalili, anasema kama skimu hiyo ikikamilika wataweza kuvuna gunia zaidi ya 30 kwa ekari moja tofauti na sasa gunia 10-15, hivyo kuondoa kabisa hali mbaya ya chakula na uchumi inayowakabili wananchi wa kata yake.
Tume ya Umwagiliaji
Kwa upande wake Mkurugenzi Tume ya Umwagiaji Morogoro, Elibariki Mwendo, anasema kuwa mradi wa skimu ya umwagiliaji ya Rudewa haukukwama kama wengi wanavyosema, bali ni kutokana na fedha kutolewa kidogo kidogo na kadri zinavyokuwa zinapatikana ujenzi unaendelea.
“Baada ya awamu ya kwanza na ya pili hela ikawa hamna, ndio imepatikana sasa hivi shilingi bilioni saba, hivyo wanachimba mfereji wote wamalize pamoja na kutengeneza barabara na mifereji yote ya shambani, hela ilikuwa haijatoka, inatoka kidogo kidogo, kwahiyo ikitoka tunafanya kinachowezekana,” anaeleza Mwendo.
Mwendo anasema skimu hiyo ambayo mwajiri wake ni Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inajengwa na Kampuni ya C0MFIX & Engeneering LTD ya Dar es Salaam na kwamba imefikia asilimia 25 ya ujenzi wake, na kuwa inatarajiwa kukamilika Septemba 5, mwaka huu na hivyo kuondoa adha waliyokuwa wanakumbana nayo wananchi hao.
Ni hatari sana kwa vijana ambao ndio nguvu kazi inayotegemewa na taifa kukaa bila kazi maalum ya kufanya ili kuwaingizia kipato na kuwawezesha kumudu maisha yao, hivyo serikali inatakiwa kuwatengenezea mazingira mazuri vijana ambao wameamua kukaa vijijini na kujiajiri katika kilimo ili wasikimbilie mijini ambako huko pia hakuna ajira.