25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Njombe ilivyopiga hatua utoaji wa chanjo ya Polio kwa Watoto

*Yavuka lengo la utoaji chanjo, wananchi wapongeza

Na Elizabeth Kilindi, Njombe

Ugonjwa wa polio huathiri watoto chini ya miaka mitano huku wengine wakipooza. Kifo pia kinaweza kutokea iwapo kupooza huko kutaathiri misuli inayosaidia mfumo wa upumuaji.

Hakuna tiba lakini chanjo dhidi ya ugonjwa huo huwalinda watoto maisha yao yote. Chanjo hii hutolewa kwa njia ya matone ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo ambapo kisa kimoja kimeripotiwa nchini Malawi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa Wizara ya Afya, mtoto chini ya miaka mitano asipopata chanjo ya polio anajiweka kwenye hatari ya kupata madhara makubwa.

Chanzo chake

Ugonjwa huu unasababishwa na virusi aina ya (Poliovirus) vinavyoishi kwenye mfumo wa kumeng’enya chakula na si kila mtu anayeambukizwa virusi hivi vya polio hupooza na watu wengi huwa na dalili za kawaida tu kama maumivu ya kichwa, homa, kutapika, maumivu ya mgongo, maumivu ya misuli na kuwashwa ngozi.

Hata hivyo, ili kuzuia ugonjwa wa polio ni kupata chanjo ambayo hufanya kazi kwa ufanisi mkubwa, inaweza kukinga zaidi ya 90 ya maambukizi.

Watoto wanapopata chanjo hii hubaki katika matumbo yao kwa kipindi kifupi kuwapa kinga wanayotarajia na kisha hutoka kwa njia ya haja kubwa ambapo inaweza kubaki katika mazingira.

Kampeni ya kuchanja chanjo ya ugonjwa wa polio kwa watoto zaidi ya milioni tisa inafanyika katika nchi nne za Kusini na Mashariki mwa Afrika baada ya kuthibitishwa mlipuko wa ugonjwa huo nchini Malawi.

Kampeni hiyo  inajumuisha nchi jirani za Msumbiji, Tanzania, Zambia kulingana na Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF) ambayo inafanya kazi na serikali na washirika wengine.

Katiika awamu ya tatu zaidi ya watoto milioni 20 wanatarajiwa kufikiwa na chanjo hiyo.

Maeneo yanayoathiriwa zaidi na Polio

Misuli inayoruhusu kukunja, kukunjua na kutanua mguu kuanzia kwenye kiuno pia misuli inayoruhusu kukunja, kukunjua goti, misuli inayonyanyua, misuli ya bega, misuli ya nyuma ya bega hadi kwenye kiwiko ndiyo sehemu zinazoathiriwa zaidi na ugonjwa huu.

Sehemu nyingine ni misuli ya mgongo pande zote mbiliza uti wa mgongo, misuli ya vidole, misuli inayoipa nguvu ’’Tendons’’ zinazoruhusu kukunja

Takwimu

Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa ile inayotekeleza zoezi hilo hapa nchini ambapo kwa kuanza imepanga kuwafikia watoto 110,173 lakini hadi sasa wamefikia watoto 128,223 sawa na asilimia 116.

Kwa upande wa Halmashauri ya Mji wa Njombe wamevuka lengo kwa kuchanja watoto 24,082 sawa na asilimia 124 huku lengo lilikua ni 18,821.

Hali ya chanjo ya polio Halmashauri mji Njombe

Kwa upande wa mratibu wa huduma za chanjo Halmashauri ya mji Njombe, Simon Ngassa, anasema ili kukabiliana na ugonjwa wa polio mikoa jirani ikiwemo Njombe tayari imechukua tahadhari kwa kuhakikisha watoto wote chini ya miaka mitano wanapata chanjo.

Anasema kuwa kampeni ya awamu ya kwanza ilianza machi 24 hadi 28 ambapo lengo lilikua ni kufikia watoto 18,821 na kuvuka lengo kwa kufikia watoto 24,082 sawa na asilimia 124.

Ngassa anasema kuwafikia watoto hao ilikua ni kwa namna ya kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba, katika vituo vya kutolea huduma za afya, maeneo ya mikusanyiko, maeneo ya taasisi kama shule na vituo vya kulelea watoto mchana.

“Ufanisi huu au kiwango hiki cha uchanjaji kilichofikiwa kimetokana na jitihada za halmashauri uratibu wake, upatikanaji wa dawa wenyewe na ufanisi wa watoa chanjo ambao huduma hii ilifanyika kwa njia kuu tatu, njia ya kwanza ni kutembea nyumba kwa nyumba, vituo vya huduma pamoja na kutembelea taasisi,’’ anasema Ngassa.

Ngassa anasema kuwa kwa maeneo ya vijijini pia walitumia mbinu ambazo zilifanyika mtaa kwa mtaa, kijiji kwa kijiji ili kuhamasisha chanjo hiyo.

“Kazi imefanyika, jamii ilihamasika kujitokeza kuleta watoto ili kupata chanjo ya polio ambayo lengo kuu ilikuwa ni kujikinga dhidi ya ugonjwa wa polio ambao umeripotiwa nchi jirani ya Malawi. Lakini kampeni hii haikuishia awamu ya kwanza, hii inakwenda mfululizo kwa awamu kuu nne, tukiamini kwamba mtoto ili aweze kukingwa dhidi ya ugonjwa wa polio angalau apate dozi nne,’’ anasema Ngassa.

Ngassa anasema kuwa chanjo ya polio awamu ya pili inatarajia kuanza Mei 12, mwaka huu.

“Naomba jamii iendelee kujitokeza kwenye awamu ya pili na  zote zijazo ili kuhakikisha mtoto amepata matone kwa awamu kuu nne kwa kufanya hivyo watoto chini ya miaka mitano watakua wamekingwa dhidi ya ugonjwa huu hatari,” amesema Ngassa.

Ngassa anasema: ’’Ugonjwa huu ni hatari ndio maana ameripotiwa mtoto mmoja tu katika nchi jirani imekua ni janga huhitaji kuona ni watoto wangapi, mgonjwa mmoja tu naweza kuonyesha kwamba hiki kitu ni hatari na unamadhara makubwa,” anasema.

Wananchi wanena

Mmoja wa wakazi wa mjini Njombe, Hidaya Michael anasema kuwa anaipongeza wizara ya afya kwa kuja na mkakati wa kutoa chanjo nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo.

“Huu mkakati ni mzuri kwa sababu ukienda katika majukumu yako ukimuacha mtoto nyumbani uhakika wa kupata chanjo upo, hii ni nzuri sana kwa kweli,’’ anasema Hidaya.

Nae, Agnes Mligo anasema madhara ya ugonjwa wa polio ni makubwa hivyo wazazi wajitokeze, watoe maelekezo katika nyumba zao ili kuhakikisha watoto wanamaliza dozi zote.

“Mimi nina mdogo wangu mwanae alipata madhara kutokana na ugonjwa huu sio mzuri, niwaombe wazazi wenzangu hapa tusifanye mchezo. Tuhakikishe watoto wanapata chanjo kwa vipindi vyote hii itasaidia watoto wetu kuwa salama,’’ anasema Agnes.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles