26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kutunisha bajeti sekta ya ubunifu

*Ni kutoka bilioni 1 hadi bilioni 5.5 katika mwaka ujao wa fedha

*Wabunifu watakiwa kuchangamka

Ramadhan Hassan, Dodoma

WIZARA ya Elimu Sayansi na Teknolojia imeongeza bajeti ya masuala ya ubunifu nchini kutoka Sh bilioni 1 kwa mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh bilioni 5.5 kwa mwaka ujao wa fedha 2022/23.

Hayo yameelezwa Mei 4,2022 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Eliamani Sedoyeka, wakati akifungua mafunzo kwa Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Dodoma kuhusu Wiki ya Ubunifu Tanzania 2022 iliyoandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia mradi wake wa FUNGUO.

Amesema katika bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2021/22 ambao unaishia Juni 30, mwaka huu, kiasi cha Sh bilioni moja kilitengwa kwa ajili ya kuendeleza wabunifu.

Katibu huyo amesema fedha hizi zipo Tume ya Taifa Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na tayari wapo wabunifu ambao wamepokea na wanaendelea kunufaika.

Prof. Sedoyeka amesema kwa mwaka ujao wa fedha (2022/23), serikali imepanga kutenga Sh bilioni 5.5 kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi ya kubuni na kuendeleza bunifu, kujengea uwezo taasisi na mbunifu mmoja mmoja.

“Mtu akifanya bunifu tunamshauri sana kwenda serikalini kulingana na ubunifu wake, lakini Shirika la Viwango Tanzania(TBS) kushauri viwango vinavyotakiwa kulingana na ubunifu uliobuniwa, pia bunifu zifanywe kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi,” amesema Prof. Sedoyeka.

Amesema hadi sasa wabunifu ambao wametambuliwa, kuziangalia teknolojia na kuziingiza kwenye vituo atamizi kwa matumizi ya nchi ni takribani 200 na Sh bilioni 2.3 zimetumika kuendeleza gunduzi zao.

Katibu Mkuu huyo amesema kati ya bunifu ambazo zimefanya vizuri sana ni Magila Tech alyoanza akiwa mwanafunzi IFM na kwenda COSTECH na akapewa ushirikiano na serikali.

“Sasa hivi yeye ni kati ya wabobezi duniani katika usalama wa mitandao na juzi amefungua ofisi Dubai ikiwa ni Ofisi yenye vijana wa Kitanzania saba, NIT pia wameshatengeneza gari, nimeona Kipanya ametengeneza gari, ukienda Arusha Tech imetengeneza gari ndogo kwa ajili ya wenye changamoto za kutembea kwa miguu ambayo inatumia umeme jua,” amesema Prof. Sedoyeka.

Nae, Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Prof. Maulilio Kipanyula amesema mashindano ya mwaka huu yameshindanisha wabunifu 862 kutoka makundi ya shule ya msingi, sekondari, vyuo vya ufundi, vyuo vya ufundi wa kati, mfumo usio rasmi, taasisi za utafiti na vyuo vikuu.

Amesema wizara imeendelea kuandaa mazingira wezeshi ili wabunifu waweze kuonekana pamoja na bunifu zao ziweze kufika sokoni, kushirikiana na wadau katika kutekeleza hilo na kutenga bajeti ili kuendeleza wabunifu.

Kwa upande wake Meneja wa Programu ya FUNGUO ya UNDP, Joseph Manirakiza amesema wamekuwa wakishirikiana na wizara katika kuwaendeleza wabunifu, kutoa msaada wa kitaalamu kwa wabunifu hao kupitia kumbi za atamizi lakini pia kushirikiana na serikali kuweka mazingira rafiki ya wabunifu katika kuendesha biashara.

Wiki ya Ubunifu Tanzania kwa mwaka huu ina kauli mbiu “Ubunifu kwa Maendeleo Endelevu” na inashirikisha wabunifu 70 ambao wameshindanishwa kutoka kwa wabunifu 862 waliowasilisha bunifu zao.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Waandishi Mkoa wa Dodoma ambaye ni Mwandishi wa Redio Uhuru, Sakina Abdulmasoud ameishukuru wizara hiyo kwa kuandaa semina ambayo imewasaidia kupata uelewa kuhusu mambo ya ubunifu.

Sakina ambaye ni Balozi wa Mazingira, amewataka wabunifu kubuni teknolojia ambazo ni rafiki katika masuala ya mazingira huku akidai wataendelea kufanya kazi pamoja na wizara hiyo huku akikipongeza kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara hiyo kwa kuonesha ushirikiano mkubwa kwa waandishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles