27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Miaka 60 ya Uhuru na Mapinduzi ya Huduma ya Afya ya Uzazi nchini

Na Yohana Paul, Geita

Tangu mwaka 1961, ikiwa ni miaka 60 sasa toka Tanganyika (Tanzania Bara) kupata Uhuru, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa ikitekeleza Sera, Miongozo na Sheria mbalimbali kufikia maboresho ya huduma za afya nchini.

Mapema mwezi Aprili mwaka jana (2021), Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu akihutubia bunge, aliainisha kuwa sekta ya afya, hususan kitengo cha afya ya uzazi ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayoangaliwa zaidi na serikali.

Anasema kwa miaka mitano iliyopita (2015-2020) taifa limeshuhudia mafanikio makubwa ya sekta ya afya kwa kujenga vituo vya kutolea huduma za afya 1,887 (zikiwemo zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 99, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10 na Hospitali za Rufaa za Kanda 3.

Rais Samia anasema, katika miaka hii mitano (2021 mpaka 2025, serikali imelenga kuwekeza zaidi na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kuendelea kujenga miundombinu, kuongeza watumishi, vifaa tiba, dawa na vitendanishi.
Mafanikio ya Huduma ya Afya hadi 2021.

Akitoa taarifa kwa umma juu mafanikio ya wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto kwa miaka 60 ya uhuru wa Tanzania bara mwezi novemba mwaka huu mjini Dodoma Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima anasisitiza hatua kubwa imefikiwa kwenye sekta ya afya.

Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima.

Dk. Gwajima anaweka wazi kiashiria kikubwa cha kuboreshwa kwa huduma za afya ni Idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote kuongezeka hadi kufikia vituo 8,537 ikilinganishwa na vituo 1,343 mwaka 1960.

Anasema, ongezeko hili ni sawa na asilimia 84.26, huku kati ya vituo hivyo, serikali inamiliki asilimia 64, Mashirika ya dini asilimia 9 na vituo binafsi asilimia 27.

Anaeleza, Mtandao wa vituo vya huduma za afya umepanuka na kusogea karibu zaidi na wananchi na kufanya jumla ya zahanati kufikia 7,242; vituo vya afya 926; na Hospitali za Wilaya ni 178, Hospitali zingine zikiwa ni 151.

Anasema, Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) ni miongoni mwa kampeni iliyochagiza mafanikio hayo, ambapo Jumla ya Vituo vya Afya 487 kati ya vilivyopo vinafanya upasuaji wa dharura.

“Aidha, hospitali za kibingwa ngazi ya mikoa ni (28), ngazi ya Kanda Sita (6), hospitali za ubingwa maalumu ni Tano (5) na hospitali ya taifa ni moja (MNH). Vituo vyote hivi vina jumla ya vitanda 90,488 ikiwa ni sawa na ongezeko la vitanda 71,656 sawa na asilimia 79.18.

“Kwa sasa uwiano wa vituo kwa idadi ya watu ni kituo kimoja kwa watu 6,751.5 na hivyo, kuifanya Tanzania kufikia malengo ya umoja wa mataifa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa kuzingatia idadi ya watu na jiografia,”

Kwa maneno yake Dk. Gwajima, idadi ya watumishi na wigo wa kada za wataalamu kwenye vituo vya huduma umepanuka kiasi kwamba hivi sasa vituo vya afya vinafanya hadi huduma za upasuaji mkubwa ambao awali ulikuwa haufanyiki.

Anasema idadi ya wataalamu wa baadhi ya kada mbalimbali za msingi kwenye afya waliosajiliwa imeongezeka hadi kufikia zaidi takribani 71,365 na usajili unaendelea kila siku.

“Hawa ni baadhi tu ya kada zinazojumuisha madaktari bingwa, wa kawaida, wauguzi, wataalamu wa maabara, mionzi, wafamasia na mionzi. Kabla ya uhuru wote hawa kwa ujumla walikuwa 435 tu,” anaeleza.

Mafanikio Kitengo cha Afya ya Uzazi

Akizungumuzia kada ya sekta ya afya kitengo cha Afya ya Uzazi, Dk. Gwajima anasema idadi ya Kliniki za afya ya uzazi imeongezeka na sera ni kuwa katika kila kituo cha huduma za afya kuwe na huduma za afya ya uzazi na mtoto.

Dk. Gwajima anaelezea, mafanikio hayo yamegusa ongezeko la wajawazito waliohudhuria mahudhurio manne au zaidi ya kiliniki na hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2021, asilimia 93.4 ya wajawazito walihudhuria kliniki.

“Ongezeko la akina mama kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya limefikia hadi asilimia 83.1 mwaka 2020 ambayo ni zaidi ya lengo la Mpango Mkakati wa Nne wa Sekta ya Afya (HSSP IV) la asilimia 65,”.

Anasema idadi ya akinamama waliojifungua na kurudi kiliniki siku mbili baada ya kujifungua imefikia asilimia 62 huku mwitikio huo ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.

“Asilimia 60 ya vifo vitokanavyo na uzazi hutokea kipindi cha baada ya kujifungua kutokana na matatizo ya kupoteza damu, kifafa cha mimba na maambukizi ya bacteria,” anasema.

Anasema maboresho ya afya ya uzazi yamewezesha hadi kufikia Machi 2021, jumla ya akina mama 332,620 wameweza kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi kwenye vituo 794 vya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi.

“Pia, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 112 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2004/05 hadi vifo 50 kila vizazi hai 1000 mwaka 2020.

“Vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja (Infant Mortality) vimepungua kutoka 94 kwa vizazi hai 1000 mwaka 1992 hadi vifo 36 kwa vizazi hai 1000 mwaka 2020 (DHS projection 2020),” anaongeza.

Dk. Gwajima anasema pia vifo vya watoto wachanga ndani ya siku 28 (neonatal mortality) vimepungua kutoka vifo 32 kwa kila vizazi hai 1000 kwa mwaka 2004/05 hadi vifo 20 kwa kila vizazi 1000 kwa mwaka 2020.

Waziri huyo mwenye dhamana ya sekta ya afya anasema juhudi za serikali zimefanya vifo vya wajawazito kupungua kutoka vifo 870 kwa kila vizazi 100,000 mwaka 1990 hadi kufikia vifo 321 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2020.
Mikakati ya Serikali Kuimarisha Afya ya Uzazi.

Akisoma hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto Dk Gwajima anasema kwa mwaka wa fedha 2020/2021 maboresho zaidi yanafanyika kuboresha huduma ya afya.

Dk.Gwajima anasema, miongoni mwa malengo ya taifa ni kulenga kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, watoto wachanga na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Anasema jumla ya sh. Bilioni 63.5 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha mnyororo mzima wa huduma za chanjo ikiwemo majokofu 1,200 na magari 60.

“Hivi sasa, Wizara inaendelea na usambazaji wa vifaa na vifaa tiba ili kuviwezesha vituo vya afya vilivyoboreshwa kutoa huduma za dharura za uzazi ikiwa ni pamoja na kufanya upasuaji wa kumutoa mtoto tumboni pindi mama anapopata uzazi pingamizi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles