25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mabondia Watanzania walivyouteka Usiku wa Mabingwa 2021

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania

BOXING Day ilikuwa siku ya kipekee kwa wadau wa masumbwi nchini baada ya kushuhudia burudani ya mchezo huo ya kufungia mwaka 2021 ambapo pambano kubwa lililokuwa likisubiriwa kwa hamu ni kati ya bondia Mtanzania Selemani Kidunda na Tshimanga Katompa kutoka DR Congo.

Hata hivyo pambano hilo lililokuwa la ubingwa wa WBF International la raundi 10 uzito wa kilo 76 halikufikia mwisho na mbabe kupatikana kutokana na kukatishwa katika raundi ya tatu baada ya Katompa kumchezea faulo mbaya Kidunda na kuamuliwa kuwa ni sare kulingana na kanuni za Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Duniani (WBF).

Ismail Galiatano akivalishwa mkanda wake wa ubingwa wa PST baada kumtwanga Mmalawi Denis Mwale.

Katika usiku huo wa Mabingwa, uliofanyika jana Desemba 26, 2021 kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam, jumla ya mapambano 13 yalipigwa, huku Watanzania waking’ara dhidi ya wageni.

Miongoni mwa mabondia waliopeperusha vizuri bendera ya Tanzania na kuzikosha nyoyo za mashabiki wa ngumi ni George Bonabucha kutoka JWTZ aliyemchapa Mzimbabwe Hassani Millanzi kwa pointi na kutwaa ubingwa wa PST.

George Bonabucha akiwa na mkanda wake baada ya kumchapa Mzimbabwe Hassani Millanzi kwa pointi.

Bondia mwingine wa JWTZ, Ismail Galiatano aliendeleza ubabe kwa kumtwanga Mmalawi Denis Mwale na kuondoka na mkanda wa PST, huku Juma Choki akimchakaza vibaya kwa K.O Mmalawi Salim Chazama.

Daniel Matefu akipatiwa huduma ya kwanza baada ya kuangushwa na konde zito la Haruna Swanga katika pambano la utangulizi la uzito wa juu.

Wengine waliobuka kidedea katika Usiku wa Mabingwa ni Haruna Swanga alimtwanga Daniel Matefu kwa K.O, Ibrahim Class alimpiga K.O raundi ya kwanza Kelvin Majiba, Joseph Mchapeni alimchapa T.K.O Pascal Manyota, Paul Richard alimpiga Paul Magesta na Vigulo Shafii akimdunda Ally Kilongora.

Iddi Jumanne ‘Kibakuli’ alimpiga kwa pointi Hamisi Kibodi,King Makasy akimtwanga Ibrahim Mpili, wakati upande wa wanawake Grace Mwakamele alipoteza dhidi ya Ruth Chisale wa Malawi, pambano lililokuwa la ubingwa, Leila Yazidu akichapwa na Najma Isike mchezo wa utangulizi.

Mashabiki walioshuhudia burudani hiyo, walionekana kufurahishwa na kiwango kilichooneshwa na mabondia wa Tanzania, huku wakiomba pambano la Kidunda na Katompa lipangiwe siku ya kurudiwa ili kumpata mbabe.

MwakameRuth Chisale kutoka Malawi na Grace Mwakamele wakitwangana, pambano la ubingwa wa PST

Akizungumzia michezo hiyo, Mratibu wa Usiku wa Mabingwa, Kapteni Selemani Semunyu, amesema Watanzania wanatakiwa kujipongeza kwa kufunga mwaka vizuri na wanajipanga kuendelea kuleta mambo mazuri.

“Kidunda ameshinda, bondia ni binadamu, ingekuwa faulo ya ngumi angeendelea lakini ya kichwa ni mbaya.Nafikiri Watanzania wadau wa ngumi tujipongeze tumemaliza mwaka 2021 vizuri, ngoja tujipange, mambo mazuri yanakuja waendelee kutupa ushirikiano,” amesema Kapten Semunyu.

Refa akimhesabia Pascal Manyota akiwa amekalishwa na konde baada ya kuchapwa na Joseph Machapeni katika raundi ya pili.

Kwa upande wake Kocha wa Kidunda, Hassam Mzonge, amesema mambondia wake wamefanya kazi nzuri anaamini watazidi kuwa bora zaidi na kuitangaza Tanzania.

Pamoja na mashabiki wa ngumi walijitokeza kushudia mapambano hayo, pia walikuwepo wasanii mbalimbali wa muziki na filamu Tanzania ambao walinogesha usiku huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles