28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Makala: Atom ya Amani Urusi inavyotoa mchango wa kipekee kwa maendeleo endelevu Afrika

Na Mwandishi Wetu

Upanuzi wa ushirikiano kati ya Urusi na nchi za Afrika katika miaka michache iliyopita hauhusishi tu utekelezaji wa miradi ya pamoja katika nyanja ya uchumi bali mipango kadhaa mikubwa ya kijamii na kibinadamu.

Shirika la Kiserikali la Rosatom, mmoja wa mabalozi wakuu wa Urusi barani Afrika, tayari limewasilisha fursa za kipekee za teknolojia za nyuklia nje ya tasnia ya nishati – katika dawa, kilimo, utafiti wa kisayansi na nyanja ya mazingira – kwa washirika wake huko Afrika Kusini, Tanzania, Rwanda, Zambia na nchi nyinginezo.

Moja ya mipango mashuhuri ambayo tayari imetekelezwa kwa kiwango cha vitendo ni mradi wa kuhifadhi idadi ya faru nchini Afrika Kusini kwa kutumia isotopu zenye mionzi, ambazo zinaweza kupelekwa hadi nchi zingine za Afrika katika siku zijazo.

Moja ya mafanikio hayo ni pamoja na zaidi ya makubaliano 500 yaliyosainiwa kati ya kampuni za Urusi na Afrika zenye thamani ya takriban rubi bilioni 800 (zaidi ya dola bilioni 10) – haya ndio matokeo makuu ya mkutano wa kwanza wa Urusi na Afrika uliofanyika Sochi nchini Urusi mnamo mwaka 2019.

Chama cha Ushirikiano wa Kiuchumi na nchi za Kiafrika, kilichoanzishwa kama matokeo ya tukio hilo, kilichukua jukumu la kukuza kwa utaratibu biashara ya Urusi barani humo, ambapo hawajawahi kusahau juu ya msaada mkubwa ambao Umoja wa Kisovieti ulikuwa ukitoa kwa nchi changa ambapo hadi sasa ushirikiano kati ya Urusi na Afrika umefikia kiwango kipya.

Afrika ni bara lenye utajiri wa maliasili, pamoja na amana ya urani, ambayo shirika la serikali ya nyuklia la Urusi Rosatom kwa muda mrefu imeonyesha nia ya kuiendeleza. Hata hivyo, tasnia ya nyuklia ya Urusi ya leo inaweza kuipatia Afrika sio tu uchimbaji wa malighafi na miradi ya ujenzi wa mitambo ya nishati ya nyuklia.

Ushirikiano wa muda mrefu wa Rosatom na nchi za Kiafrika ni pamoja na miradi kadhaa ya kibinadamu na kijamii kwa watu wa eneo husika inayolenga kufikia malengo ya maendeleo endelevu barani Afrika, ambayo inakabiliwa na hatari za ulimwengu, kama vile mabadiliko ya hali ya hewa na uharibifu wa mazingira.

Teknolojia za Nyuklia Kulinda Viumbe anuwai

Mnamo Mei mwaka huu, mradi wa ubunifu wa kimataifa wa uhifadhi wa idadi ya faru, uitwao Rhisotope (faru + isotopu), ulizinduliwa nchini Afrika Kusini. Kikundi cha utafiti kinajumuisha wawakilishi wa Afrika Kusini (Chuo Kikuu cha WITS), Australia (ANSTO), USA (Chuo Kikuu cha Jimbo la Colorado) na Urusi iliyowakilishwa na Rosatom, Chuo Kikuu cha Tomsk Polytechnic na Kituo cha Sayansi na Ufundi “Utafiti wa Fizikia ya Nyuklia”.

Waandishi wa mradi huo wana jukumu kubwa mbele yao – kukuza na kutekeleza njia ambayo itamaliza ujangili wa faru, ambayo inaweza kusababisha kutoweka kabisa kwa wanyama hawa katika miaka ijayo ambapo hatua kadhaa za kuwalinda ambazo zilichukuliwa hapo awali hazikufanikiwa – kuangamizwa kwa faru kunaendelea, kwani pembe yao inabaki kuwa bidhaa maarufu sana kwenye soko haramu.

Sayansi ya nyuklia inatoa suluhisho bora kwenye tatizo hili, ikiwa sehemu salama ya isotopu ya nyuklia imeingizwa ndani ya pembe ya faru, itafanya uwezekano wa kugundua wahalifu, ambao wanajaribu kuchukua pembe nje ya Afrika Kusini, wakitumia vifaa vya kugundua mionzi kwenye udhibiti wa mipaka.

Hadi sasa, kulingana na wataalamu wa Rosatom, sehemu ya utafiti wa mradi inaendelea na Watafiti wanaangalia faru wawili ambao walipokea sindano ya isotopu zisizo na mionzi C-13 (kaboni) na N-15 (nitrojeni), na ikiwa vipimo vinathibitisha kuwa dutu hii haiingii ndani ya mwili wa faru na haimdhuru, vifaa vya mionzi vitatumika katika hatua inayofuata ya jaribio ambapo Rosatom ina mpango wa kuwa muuzaji wao katika hatua ya mwisho.

Mradi wa Rhisotope unaonyesha wazi uwezekano mkubwa sana wa kutumia teknolojia za nyuklia. Baada ya kukamilika utafiti kwa mafanikio, ujuzi huu unaweza kutumika katika nchi zingine za Afrika na kwingineko kwa ulinzi wa aina zingine za wanyama zilizo hatarini , Kulingana na huduma ya uhusiano wa waandishi wa habari wa Rosatom, mali miliki, pamoja na programu za mafunzo, zitatolewa kwa mashirika ya kimazingira yanayotaka bila malipo.

Ushirikiano wa miaka kumi

Tanzania, ambapo teknolojia kama hizo zinaweza kusaidia kuhifadhi idadi ya tembo, ni moja ya nchi ambazo matokeo ya mradi wa Rhisotope yanaweza kuongezwa katika siku zijazo.

Mwaka huu ni mwaka wa kumi tangu Rosatom ianze kufanya kazi katika nchi hii kufatia kupata leseni ya kuendeleza amana ya urani ya Mto Mkuju uliopo Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma na mradi huo baadaye uliahirishwa kwa sababu ya bei ya chini ya urani, lakini hii haikuzuia Rosatom kutekeleza mpango mkubwa wa uwekezaji wa kijamii nchini Tanzania.

Huko nyuma mnamo 2013 shirika lilianza kutoa msaada kwa Pori la Akiba la Selous (sasa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, zamani sehemu ya kaskazini, magharibi na kusini ya Pori la Akiba la Selous) katika vita dhidi ya ujangili, kwani tatizo lilifikia kiwango cha kutisha kati ya mwaka 2009 na 2013, idadi ya tembo ilipungua kwa theluthi mbili kwa sababu ya uwindaji haramu – hadi kufikia wanyama elfu 13 tu.

Kama sehemu ya mpango wa ushirikiano na Serikali ya Tanzania, kampuni hii ya Urusi ilisaidia kundi la mgambo kufanya doria katika eneo la kilomita za mraba elfu 20, iliwapatia mafunzo, vifaa na vifaa vya kiufundi, pamoja na picha za kisetilaiti na dronu.

Kupitia mradi wa kupambana na ujangili wa Mantra timu nne za doria zilipewa posho, nyenzo nzuri za porini kama magari, GPS, mahema na jenereta ya umeme kwenye makao makuu, anasema Lembolos Ngengeya, Askari wa uhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Hii ilisaidia kuwaongezea motisha askari wa wanyapori kulinda wanyama walio hatarini kama tembo wa Kiafrika, mbwa mwitu wa Afrika na faru weusi na hatimaye, shughuli za askari zinalenga kuhifadhi mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, makazi yake, bioanuwai, uhamiaji wa mamalia wakubwa na ndege.

“Baada ya kufanikiwa kukamata idadi kubwa ya majangili katika Hifadhi ya Nyerere hii iliwaogopesha wawindaji wengine haramu na kutuwezesha kupunguza kabisa ujangili hadi asilimia sifuri katika eneo hilo linalodhibitiwa na timu za Mantra za kuzuia ujangili kutoka 2017 hadi leo. Hayo yalikuwa mafanikio makubwa kadri tunavyofanya doria zaidi ndivyo aina za wanyama zilizo hatarini ziko salama na kuwafanya waweze kuzaliana tena na kuongezeka katika mazingira yao ya asili ”, anasema Ngengeya.

Kwa kuongezea, Mantra iliunga mkono na kutoa mafunzo mafupi ya ziada kwa askari ili kujenga ukakamavu, mbinu za kupambana porini na elimu ya huduma ya kwanza. Hii ilikuwa muhimu sana kwa ufanisi wa askari wa wanyamapori na usalama wao wakati wa doria.

Upeo wa miradi hii inaweza kupanuliwa zaidi ya eneo la awali kwa kuongeza idadi ya timu za doria kutoka timu nne hadi saba ili kuruhusu kulinda eneo kubwa zaidi, kwa mujibu wa Ngengeya na kuwa Tembo na mbwa mwitu ni spishi zinazohamahama, ambayo inamaanisha wanaendelea kutoka eneo moja kwenda lingine, anaelezea.

Hata hivyo mmoja wa mgambo wa TAWA ambaye hakutaja jina lake amesema kuwa ili kuweza kuwalinda wanyama vyema na kuwa na ufuatiliaji wa karibu wa mahali walipo kuna haja ya askari wa ziada na ushirikishwaji wa wenyeji ambao wana habari za majangili ambapo inapaswa kufanya kazi kwa karibu na watoaji habari wa eneo hilo ambao watakusanya na kutupatia habari kuhusu majangili ili tuweze kuwakamata kabla ya kuingia kwenye hifadhi au kabla ya kuua tembo.

Katika miaka miwili ya mradi, idadi ya tembo katika Hifadhi ya Nyerere iliongezeka kwa elfu mbili kulingana na sensa iliyofanywa na shirika la utafiti wa wanyapori (TAWIRI) kati ya mwaka 2014 na 2018 inaonyesha tembo waliongezeka na kuwa 15,500.

Mnamo mwaka wa 2015, kwa kutambua mipango na ushiriki mzuri wa Mantra katika program za kijamii, kampuni hii tanzu ya Rosatom nchini Tanzania, ilipewa tuzo ya Rais ya Uwajibikaji wa Kijamii na Uwezeshaji kwa kuwa “Kampuni bora inayohusika na utafiti wa madini”.

Tanzania inashirikishwa katika sehemu kama hiyo ya shughuli za Rosatom kama kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wenye sifa kwa nchi za Kiafrika na katika Tanzania pia, shule kadhaa zilifadhiliwa kununua vifaa – kutengeneza maabara za shule na kutoa madawati 1,500 kwa shule zilizopo katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Katika wilaya hiyo ya Namtumbo, ambapo Mradi wa Mto Mkuju uko, Mantra imetoa maktaba saba za kisasa zikiwemo maktaba nne za elektroniki zenye thamani ya zaidi ya USD 40,000 sawa na Shilingi Milioni 92 za kitanzania.
Akipokea moja ya maktaba za kielektroniki hivi karibuni, mkuu wa shule ya Sekondari ya Namabengo, Gabriel Mwanzila aliishukuru Mantra na kusema “Maktaba ya kisasa ya kielektroniki hakika itasababisha kuboreshwa kwa utendaji kwa asilimia 100 kwa wanafunzi na walimu kwani wataweza kufikia na kupata rasilimali mbalimbali za mtandaoni”.

Tangu 2013, Rosatom imekuwa ikiwapatia vijana kutoka Afrika fursa ya kusoma nchini Urusi bure chini ya mipango ya masomo ya uhandisi na kwa sasa wanafunzi kadhaa kutoka Tanzania wanafundishwa katika vyuo vikuu vya Urusi katika maeneo yanayohusiana na tasnia ya nyuklia.

Mwaka jana watoto wa shule na wanafunzi kutoka Tanzania pia waligundua juu ya fursa za kupata elimu katika vyuo vikuu vya Shirika la Rosatom ndani ya mfumo wa mihadhara kadhaa zilizoandaliwa na ubalozi wa nchi hio ya Afrika huko Moscow ambapo mwaka huu, Rosatom, pamoja na vyuo vikuu vinavyoongoza vya Urusi, walifanya mihadhara kadhaa kwa njia ya mtandao kwa Tanzania kuhusu uwezo wa teknolojia za nyuklia za sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles