27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

Makada CCM wamgwaya Pinda

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutangaza nia ya kujitosa kuwani urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, baadhi ya wanachama wa CCM na wasomi wamekuwa na maoni tofauti.

Hali hiyo imekuwa tofauti ambapo Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, alishindwa kueleza kwa undani kauli hiyo ya Pinda huku akisema hawezi kuzungumza jambo lolote kwa sasa hadi pale atakapomaliza vikao vya chama.

Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Mangula alisema: “Kwa sasa sina la kusema kuhusu suala hili kwani nipo kwenye vikao, ninaomba nitafute baadaye ndugu yangu,” alisema kwa kifupi.

Mangula ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Nidhamu na Maadili ya CCM, hivi karibuni alitangaza mikakati ya chama katika kuwadhibiti wagombea wanaotangaza nia za kuwania nafasi za uongozi ikiwemo urais kabla ya wakati kwa kuwafungulia majalada kila mkoa kwa ajili ya kufuatilia mienendo ya wagombea hao.

Pamoja na kuomba atafutwe baada ya saa mbili, MTANZANIA lilifanya hivyo na simu yake alikuwa amezima hadi tunakwenda mitamboni.

Pamoja na hali hiyo, MTANZANIA pia lilimtafuta Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, ambaye simu yake iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu.

Akizungumzia uamuzi huo wa Pinda, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy Mohamed (CCM), alimmwagia sifa Waziri Mkuu Pinda kwa kusema ni kiongozi mwenye uwezo na asiye na kashfa ya aina yoyote ndani na nje ya Serikali.

Alisema kuwa kutokana na sifa yake hiyo, ni wazi kiongozi huyo wa Serikali hakukurupuka kuitaka nafasi hiyo ya uongozi wa juu ya nchi.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu mkakati wake wa kugawa fedha kwa wajumbe wa CCM waliokwenda katika kikao chake, Keissy alisema hakubaliani na taarifa hizo kwa Waziri Pinda kutoa kiasi cha Sh 50,000 kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa waliofikia 50 toka katika mikoa sita ya Kanda ya Ziwa.

Wajumbe wa mikoa hiyo wanaodaiwa kupewa kila mmoja Sh 50,000 kwa ajili ya fedha za nauli ni wa kutoka kwenye mikoa ya Simiyu, Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na Kagera ambao walikutana na Waziri Mkuu Pinda Ikulu ndogo ya jijini Mwanza.

“Hiyo si kweli kwani Waziri Pinda namjua hana fedha hiyo ya kuwagawia wajumbe wote hao, lakini kama kweli katoa atakuwa amefanya makosa, ila kwa kutangaza nia bado si kosa kwani kosa ni kufanya kampeni,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam Kitivo cha Elimu (DUCE), Profesa Kitila Mkumbo, alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia jambo liolote kuhusu kufaa au kutofaa kwa Waziri Pinda kuwania urais mwaka 2015.

“Imekuwa kawaida kwa mawaziri wakuu wa nchi hii kila mmoja pindi anapomaliza muda wake kutangaza nia ya kuwania urais, hivyo kwa suala la Pinda kama anafaa au hafai sina ‘comment’ kwa hilo,” alisema Profesa Kitila.

Inadaiwa Pinda pamoja na kugawa fedha hizo kwa kumtumia mmoja wa watu wake wa karibu, kugawa nauli ya Sh 50,000 kwa kila mjumbe, ambapo wajumbe hao waligomea posho hiyo kwa kueleza kuwa ni ndogo.

Pia Waziri Mkuu Pinda anatuhumiwa kutumia harambee ya Taasisi ya Benjamin Mkapa kujiimarisha kisiasa, kwani tayari CCM imepiga marufuku kwa viongozi wake na makada wake kuendesha harambee zozote zile zenye malengo ya kujiimarisha.

Waziri Mkuu Pinda aliwaeleza wajumbe hao kuwa baada ya kujitathimini na kupokea ushauri toka kwa baadhi ya maaskofu hapa nchini, kwa nia ya dhati kabisa ameamua kugombea urais kupitia CCM na kuwataka wajumbe hao wa mkutano mkuu kumuunga mkono.

Waziri Mkuu Pinda anadaiwa kuwaeleza wajumbe hao kuwa awali hakuwa na nia ya kugombea nafasi hiyo kutokana na mazingira ya nafasi yenyewe yalivyo, na kueleza kuwa hivi sasa ana ujasiri wa kugombea nafasi hiyo.

Waziri Mkuu Pinda anadaiwa kueleza wajumbe hao kuwa ana siri nzito moyoni kwa kuwa yeye ni Mjumbe wa Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CCM) na NEC na kutamba kuwa ana uhakika jina lake ni miongoni mwa majina matano ambayo yatapendekezwa na CC.

Alisema kuwa kutokana na mazingira hayo, ndio maana ameamua kukutana na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kwa ajili ya kuwaeleza nia yake ya kugombea nafasi hiyo ili waweze kumuunga mkono.

Kauli tata za Pinda

Januari 25, mwaka 2012, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitamka hadharani kwamba hana nia wala hataki kuwania urais mwaka 2015 Rais Jakaya Kikwete atakapomaliza muda wake, kwa kuwa kazi hiyo ni mzigo.

Badala yake alisisitiza kuwa hatajisumbua kuingia katika kinyang’anyiro hicho kwani amejipanga vyema kuanza maisha mapya ya kufuga nyuki baada ya kustaafu.

Kauli hiyo ya Pinda aliitoa mbele ya wahariri na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa nchi na masuala muhimu ya kitaifa yaliyojitokeza siku za hivi karibuni.

Alisema mwaka 2015 atakuwa mtu mzima sana na haamini kuwa kwa umri huo ataweza kuyamudu majukumu ya nafasi ya urais.

“Niliposema sitawania urais nilimaanisha hivyo na naomba watu wanielewe, urais si kazi ya kukimbilia kama kweli unataka kuwatumikia watu, kwa wale wanaotaka kwenda kuchuma sawa ni pazuri, lakini mimi naona ni mzigo, kuna wakati namwonea huruma Rais Kikwete maana kila kitu kigumu anaangushiwa yeye,” alisema.

“Mwaka 2015 nitakuwa na umri wa miaka 67, ina maana nikipata urais baada ya miaka mitano nitakuwa na 72, yanini nifike kote huko kwanini wakati nimeshalitumikia taifa langu muda mrefu sana, nimefanyakazi ya taaluma yangu ya sheria miaka mitatu tu nikaenda Ikulu ambako nimefanyakazi hadi leo hii, nimefanyakazi na Mwalimu Nyerere, nimefanyakazi na Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na hii awamu ya nne, kama watu hawajaridhika na mchango nilioutoa kwa nchi yangu inamaana hata nikiwa nani hawataridhika. Urais siutaki na wala siwazii wanaotaka waendelee tu,” alisema.

“Kuna wakati nikisema sitaki urais watu wananiambia acha kusema hivyo wewe, acha kabisa mzee usiseme hivyo, lakini mimi huwa nawaambia watu hawa kuwa huu ni uamuzi wangu na nataka Watanzania waelewe hivyo, anayetaka haya! Ila mimi sitakuwemo,” alisema.

Alisema anataka baada ya kustaafu ajikite zaidi katika ufugaji wa nyuki kwani amebaini kuwa biashara hiyo ina faida sana lakini Watanzania wengi bado hawajabaini fursa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles