30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi watengwa Katiba Mpya

Bunge
Bunge

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

NI siku ya 14 sasa tangu wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walipokutana kwa awamu ya pili Agosti mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine walijadili mabadiliko ya kanuni za Bunge hilo kabla ya kuanza kupitia sura 15 za Rasimu ya Katiba.

Hadi sasa baadhi ya kamati zimeshamaliza kazi ya kupitia sura zote hizo ambazo zinakamilisha sura 17 za rasimu hiyo, ikiwa ni baada ya sura ya kwanza na ile ya sita kujadiliwa kwenye awamu ya kwanza ya Bunge hilo.

Wakati kamati hizo zikitarajiwa kuhitimisha shughuli zake Agosti 27, mwaka huu, hadi sasa sehemu kubwa ya rasimu hiyo imeshatolewa maoni na kupigiwa kura kwenye ngazi ya kamati.

Sura zilizoongezwa na Bunge hilo zinazohusu mambo ya ardhi na maliasili, Serikali za Mitaa na ile ya mambo ya uchumi na fedha ndizo ambazo karibu kamati zote hawajamaliza kazi ya kupitisha.

Hadi kufika hatua hiyo kamati hizo zimebadilisha sura na ibara nyingi ambazo mwanzo zilikuwepo kwenye rasimu iliyowasilishwa kwa Rais na Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Mbali na mfumo wa Serikali tatu ambao ulipokewa kwa mtazamo chanya na wananchi wengi, vifungu vya Katiba hiyo vilivyopendekeza kuwa mawaziri wasitokane na wabunge vilionekana kuwapendeza wengi.

Pia kifungu kilichotaka wananchi wawe na mamlaka ya kumwajibisha mbunge wao, ilikuwa ni sehemu nyingine ya rasimu hiyo ambayo ilionekana kuwapa wananchi mamlaka kikatiba.

Kupunguza mamlaka ya Rais haswa kwenye suala la uteuzi, mfumo wa Bunge ni maeneo mengine ambayo yalionekana kutoa fursa ya mambo yanayohusu wananchi kujadiliwa.

Katika mdahalo uliofanyika jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa mwezi huu, Jaji Warioba alisema ingawa wajumbe wa Bunge hilo wameshindwa kuafikiana kwenye suala la Muundo wa Serikali, wakifika kwenye mambo yenye masilahi watakubaliana.

Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alisema pendekezo la wabunge kutawala kwa vipindi vitatu ni zuri na alitaka aendelee kuongoza jimbo hadi pale wananchi watakapomchoka.

“Yawezekana kuwa bado mbunge anapendwa na wananchi wake, kwanini umkatishe baada ya misimu miwili au mitatu, tumeona tuache wananchi wenyewe watafanya maamuzi.

“Pia kwa upande wa kuwapa wananchi mamlaka ya kumuondoa mbunge wao pale watakapoona hafanyi kazi vizuri, pia wajumbe wameona hiyo italeta shida huko majimboni.

“Kwanza hakuna njia ya kupima nani anafanya kazi vipi na sote tunajua siasa za huko kwenye majimbo yetu, tumeamua kuacha vyama viwe na hayo mamlaka kuona kama mbunge anatekeleza ilani ama vipi,” alisema Hamad.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati Namba 10, Anna Abdallah, alipinga kuwepo kwa mfumo wa mabunge matatu na kusema haufai kwa kuwa itakuwa ni kurudisha Serikali tatu ambazo tayari zimeshakataliwa kwa sasa.

Katika hatua nyingine, alisema kamati yake inaijadili rasimu hiyo kwa maudhui ya Serikali mbili na kwamba masuala yote yanayoweka muundo wa Serikali tatu wanayaondoa ikiwa ni pamoja na kubaki na muundo wa Bunge kama ulivyo na siyo kuwa na mabunge matatu kama kamati nyingine zinavyopendekeza.

Alisema muundo wa Serikali tatu ni sawa na kuvunja Muungano na kwamba kusema kuwe na mabunge matatu na Serikali mbili hakuna tofauti yoyote hivyo ni bora kuwa na muundo uliopo sasa.

Hadi sasa limeendelea kupokea maoni ya makundi mbalimbali wakiwamo wakulima, wafugaji, wavuni na leo Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, anatarajiwa kukutana na kundi la wasanii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles