26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Uchaguzi Chadema vurugu tupu

John Mnyika
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika

SHABANI MATUTU NA OLIVER OSWALD, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kimebaini njama za kupandikiziwa mamluki wenye nia ya kuvuruga uchaguzi wa chama hicho pamoja na mabaraza yake unaotarajiwa kufanyika Septemba 14, mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, Chadema imedai kubaini uwepo wa mamluki hao ambao wengi wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika chama hicho huku wakikosa sifa stahili na hata kupanga mikakati ya kwenda mahakamani kupinga uchaguzi huo pindi majina yao yatakapokatwa kwa kukosa sifa.

MTANZANIA limeshuhudia pia uwepo wa majina ya wanachama waliochukua fomu za kuwania uongozi katika Baraza la Vijana Taifa (Bavicha), kinyume na kanuni zinavyotaka.

Kwa mujibu wa kanuni za Bavicha, mgombea yeyote anatakiwa kumaliza kipindi cha uongozi wake kama atachaguliwa akiwa na umri wa ujana ambao kwa kanuni za baraza zinasema asizidi miaka 35 pindi awapo madarakani.

Kanuni hizo zinafafanua kwamba, ni lazima mgombea yeyote asiwe amezidi umri wa miaka 30 wakati anagombea.

Kutokana na mvurugano huo, taarifa kutoka ndani ya Chadema zinaeleza baadhi ya wanachama waliochukua fomu wengi wao wanazijua sheria na kanuni za chama hali iliyosababisha kuzusha maswali miongoni mwao.

Katika uchunguzi uliofanywa kwa baadhi ya wanachama wanaowania nafasi hizo umebaini wengine wakiwa na umri ulio juu ya miaka ya kanuni ambayo ni 18-30.

Mmoja wa waliochukua fomu za kuwania uongozi ndani ya Bavicha ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini, aliliambia MTANZANIA kanuni alizotumia kuwania uongozi wa vijana ni za chama ambazo zinasema waziwazi kwamba umri wa ujana ni hadi miaka 35.

“Sidhani kama nina kosa kutumia haki yangu kuwania nafasi hiyo, kwa sababu naamini kwa mujibu wa kanuni za chama zinaonyesha wazi kwamba mtu mwenye miaka 35 bado ni kijana, kwa kuwa nina miaka 31 sioni kosa kwa kuwa bado ni kijana.”

MTANZANIA lilipofuatilia kwa undani ni kitu gani kinachowafanya baadhi ya makada hao kuweka mikakati ya kwenda mahakamani kuzui uchaguzi huo, baadhi yao walisema hivi sasa kuna mgongano wa kisheria kati ya kanuni za uchaguzi na katiba ya Chadema.

Baada ya kubainika mipango hiyo, Chadema imetoa maelekezo kwa viongozi wa vijana na wanawake kuhakikisha kila fomu ya mgombea inakuwa na vielelezo muhimu ikiwemo cheti cha kuzaliwa.

Kauli ya Chadema

Akizungumzia kuhusu mikakati hiyo, Mkurugenzi wa Oganaizesheni Uratibu wa Kanda, Singo Kigaira Benson, alisema suala la umri wa kijana uko wazi kwani kanuni zimekuwa zikisema sifa ya mtu anayestahili kugombea uongozi.

“Kanuni zinaposema mtu anayefaa kugombea ni yule ambaye hajazidi miaka 30, isichukuliwe kuwa ni maneno ya mtu yanayotoka kinywani, kama hao mamluki hawazijui kanuni za chama wasome. Na kama yupo anayejiingiza kugombea huku akijua umri wake umezidi na baadaye kwenda mahakamani atakuwa anajidanganya,” alisema.

Kigaila aliongeza kuwa chama hakitamvumilia yeyote atakayedanganya umri, ataadhibiwa kwa kutumia kanuni za chama.

Alisema: “Hiyo haiwezi kuwa sababu ya kufutwa kwa uchaguzi na wala uchaguzi wa Chadema haufutwi na mahakama bali unapingwa ndani ya vikao halali vya chama na hata mamluki wanapokuja wahakikishe wamejipanga,” alisema.

Alisema kuwa chama hicho kimeongeza muda wa kuchukua na kurudisha fomu kwa siku tano kutoka Agosti 25 na sasa utakuwa Agosti 30, mwaka huu saa kumi jioni.

Alisema kuwa sababu ya kusogeza mbele ilichangiwa na wingi wa maombi kutoka kwa wanachama mikoani wakitaka usogezwe ili waweze kumalizia uchaguzi wa ngazi za mikoa na kupata fursa pana ya kushiriki uchaguzi wa kitaifa.

Peneza ajigamba

Kwa upande wake mgombea wa nafasi ya Uenyekiti katika Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), Upendo Peneza, amesema chama chake hakikumtuma kugombea nafasi hiyo isipokuwa dhamira ya kuleta mabadiliko ndani ya chama na Taifa ndiyo vimemsukuma.

Upendo ni kijana wa kwanza mwanamke kugombea wadhifa huo ndani ya Bavicha.

Alisema kitu cha kwanza atakachokifanya endapo atafanikiwa kushika cheo hicho ni kuweka msisitizo katika ajenda za vijana ndani ya chama pamoja na taifa, ikiwemo ubora wa elimu iliyo sawa kwa wote pamoja na ajira za kudumu.

“Leo natangaza dhamira yangu ya kugombea nafasi ya uenyekiti katika Baraza la Vijana Chadema, kwani nimeshachukua fomu na kesho (leo) natarajia kuirudisha.

“Kikubwa kilichonisukuma kuchukua uamuzi huu ni nia yangu ya dhati kabisa ya kuleta mabadiliko ndani ya Bavicha na kwa vijana wote wa Tanzania bila kujali tofauti ya dini, kabila au vyama,” alisema Upendo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles