Na Norah Damian, Mtanzania Digital
Majukwaa sita ya wanawake na wasichana wenye ulemavu yameanzishwa kwa lengo la kuimarisha uanaharakati katika kupinga ukatili wa kijinsia kwenye jamii.
Majukwaa hayo yaliyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mtwara, Iringa, Kilimanjaro na Zanzibar Magharibi yameanzishwa kwa ushirikiano wa Shirika la Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu Duniani (ADD Int) tawi la Tanzania.
Mkurugenzi Mkazi wa shirika hilo, Rose Tesha, amesema yanawawezesha wanawake na wasichana wenye ulemavu kupaza sauti na kutetea haki zao pamoja na kuboresha maisha yao.
Amesema majukwaa hayo yameanzishwa kupitia mradi wa kuimarisha uanaharakati wa wanawake na wasichana wenye ulemavu katika kupinga ukatili wa kijinsia kwenye jamii.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la ADD International, MaryAnn Clement, amesema ulemavu ni tatizo la jamii na si tatizo la watu wenye ulemavu na kuitaka jamii kubadilika na kuacha kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobass Katambi, amesema jitihada zinazofanywa na Serikali zimesaidia kupunguza mtazamo hasi kwenye jamii dhidi ya watu wenye ulemavu.