NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM
MAJERUHI 12 kati ya 19 wa ajali ya basi la Safari Njema namba T 990 AQF, waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu, wameruhusiwa kurejea nyumbani.
Ajali hiyo ilitokea juzi eneo la Kimara Stop- Over, barabara ya Morogoro ambako basi hilo liligongwa na lori la mizigo namba T 534 BYJ na kusababisha moto mkubwa.
Moto huo ulisambaa gari zima ndani ya dakika 15 na kusababisha kifo cha mtu mmoja ambaye mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Uhusiano wa MNH, Neema Mwangomo alisema mwili huo bado haujatambulika.
Alisema kati ya majeruhi hao 19, 11 kati yao ni wanawake na wanane walikuwa ni wanaume ambao walipokewa na kutibiwa katika kitengo cha dharura hospitalini hapo.
“Majeruhi hao ni Hussein Kipilipili (17), Fatuma Ndugumbi (40), Julius Shamboo (52), Irene Thomas (23), Redusi Emma (7), Vumilia Chellegu (17), Joyce Wambura (19), Said Kipilipili (19), Monica Mabele (5), Veronica Wambura (27), Mwajuma Chijuna (50) na Peter Mkini (50),” alisema.
Mwangomo alisema majeruhi wengine watatu ambao ni Miriam Thadei (44), Miriam Mkeni (45) na Asha Kipilipili (13) walipewa huduma ya dharura na kuhamishiwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kwa matibabu zaidi.
Alisema majeruhi wengine akiwamo Tausi Rajabu (30), Daniel Madambe (32) na Abdul Kiyeyu (30), walihamishiwa idara ya upasuaji kwa matibabu zaidi na majeruhi mmoja, Emmanuel Mdachi (54) amehamishiwa katika idara ya meno.
Ofisa Uhusiano wa MOI alisema majeruhi wawili kati ya watatu walipatiwa matibabu na kuruhusiwa na mmoja, Mariam Thadei bado amelazwa hospitalini hapo.
Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam walishauri serikali itoe maelekezo kwa makondakta wa mabasi katika kila gari kuelimisha jamii jinsi ya kujiokoa inapotokea majanga kama hayo ya moto katikati ya safari.