23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Majambazi yapora kininja Sinza

Pg 2 majambaziNa Waandishi Wetu

WATU wanaodaiwa kuwa ni majambazi  wakiwa wameficha nyuso zao huku wakiwa wamebeba silaha kali mkononi  jana walilisimamisha eneo la Sinza Kijiweni, jijini Dar es Salaam kwa takribani nusu saa baada ya kuvamia  gari lililokuwa limebeba pombe aina ya Banana na kupora Sh milioni 34.

Tukio hilo ambalo liliambatana na milio  ya risasi takribani sita zilizopigwa hewani lilitokea saa 5:30 mchana katika makutano ya barabara ya Shekilango na Tandale, Sinza Kijiweni.

Watu walioshuhudia tukio hilo dakika chache kabla ya waandishi wa gazeti hili hawajafika walieleza kuwa watu hao wanaodaiwa kuwa ni majambazi walikuwa katika pikipiki tatu wakati wanalivamia lori hilo aina ya Fuso lenye namba za usajiili T 210 BUU.

Inaelezwa kuwa baada tu ya kulivamia walianza kwa kupiga risasi katika tairi la kushoto hali iliyozua taharuki kwa watu waliokuwa karibu na eneo hilo akiwemo mwandishi wa habari hizi.

Watu hao ambao matendo yao yanaonyesha kuwa na utaalamu wa masuala ya silaha na kudhibiti walijipanga kila mmoja akiwa na kazi yake.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, mmoja alionekana akilizuia gari hilo kwa mbele huku akiwa ameelekeza bunduki kwa dereva.

Mwingine alionekana upande wa ubavuni wa gari hilo akimwamuru dereva wake atoe begi walilodai kuwa na fedha hizo.

Taarifa hizo zinadai kuwa katika kundi hilo, mtu mwingine wa tatu alikuwa upande wa eneo la Sinza Madukani na yeye alipewa shughuli ya kuzuia magari yanayoelekea katika eneo la tukio ambalo ni Sinza Kijiweni.

Inaelezwa kuwa wakati wakiwa katika harakati za kupora,

walipiga risasi moja kwenye tairi la gari, risasi nyingine ilipigwa juu ili kutisha na kutawanya watu waliokuwa karibu na eneo hilo, haikufahamika mara moja risasi nyingine mfululizo kama tatu zilizopigwa hewani zilitokea wapi.

Hali hiyo ilizua taharuki si tu miongoni mwa raia waliokuwa karibu na eneo hilo bali pia kwa watu hao wanaodaiwa kuwa ni majambazi na hivyo kuwafanya wafyatue risasi nyingine kama mbili kuelekea upande ilipo Benki ya BOA na Kituo cha mafuta cha Puma ambako mara nyingi kunakuwa na ulinzi.

Hata hivyo, watu hao walifanikiwa kuchukua begi lililokuwa na fedha na wakati wakitokomea wakiwa kwenye pikipiki zao hizo aina ya boxer mwandishi wa habari hizi aliwaona.

Baada tu ya watu hao kuondoka umati mkubwa wa watu ulionekana kukimbia kuelekea eneo la tukio tofauti na mwanzo ambapo walikimbia na kusababisha vumbi kubwa.

Waandishi wa MTANZANIA Jumamosi hata walipowafikia dereva pamoja na wasaidizi wake wawili waliokuwamo katika lori hilo ili kujua chanzo cha kuvamiwa kwao, walionekana kutetemeka kiasi cha kushindwa kujieleza.

Kila mmoja alionekana akipiga simu na hakuna aliyeweza kulizungumzia tukio hilo kwa ufasaha.

Baada ya muda saa sita mchana gari ndogo ya polisi aina ya Ashok Leyland  yenye namba PT 2083  liliwasili katika eneo hilo ambapo askari watatu walishuka huku wakiwa na silaha.

Kutokana na kitendo cha askari hao kuchelewa kuwasili katika eneo la tukio wananchi walionekana kuchukizwa na kitendo hicho huku mmoja akisikika akisema: “Hawa askari wetu wanajua tu kuzuia maandamano,” alisema shuhuda huyo.

Gazeti hili liliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura ambaye mara kadhaa majibu yake yalikuwa, “sina taarifa nilikuwa msibani,  nipigie baadaye.”

Alipopigiwa baadaye alijibu; “bado sijalifanyia kazi suala lako subiri nitakupigia” na mara ya tatu kabla gazeti hili halikwenda kiwandani alipopigiwa simu hakupokea kabisa.

Eneo la Sinza mara kadhaa limekuwa likikumbwa na matukio ya utapeli, ujambazi na kupora kwa kutumia risasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles