23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yalipa walimu bil 1.9/-

Asifiwe George na Imani Nathaniel (RCT), Dar es Salaam

CHAMA cha Walimu Tanzania Mkoa wa Dar es Salaam, kimesema Serikali imeanza kulipa deni la madai ya walimu kiasi cha Sh 1,936,572,146.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CWT wa mkoa huo, Amina Kisenge, alisema kwa kipindi cha  kuanzia mwaka 2013 hadi Julai 2015 walikuwa wanaidai Serikali kiasi cha Sh 3,916,432,471.

Alisema kwa sasa deni lililobaki ni Sh  1,979,860,325 ambazo bado walimu wanadai.

Alisema pamoja na changamoto hiyo nyingine ni mfuko wa PSPF kutowalipa walimu wastaafu kwa wakati na kudai kuwa walimu waliostaafu kuanzia Januari hadi Septemba 2015 hawajalipwa mafao yao.

“Kutokana na hali hiyo, tunatoa rai kwa Rais John Magufuli amalize usumbufu huu  kwa watumishi waliotumikia Taifa  kwa uadilifu ili waweze kulipwa mafao yao,” alisema.

Alisema kilio chao kikubwa kwa Rais Magufuli ni Serikali kupitia Mdhibiti  wa Mifuko  ya Hifadhi ya Jamii (SSRA)  kuanzisha kanuni mpya (kikokotoo) cha 1/580 inayoonyesha mafao ya walimu  yanayolipwa kwa mkupuo toka kanuni ya awali yaani 1/540.

Kisenge alisema jambo hilo halikubaliki, hata kama walimu walioko  kazini  sasa hawahusiki  na kanuni hii kwasababu inaanza  kutumika  kwa wale walioajiriwa kuanzia Julai mosi mwaka 2014.

“Kwa sababu hii hatukubaliani na msimamo wa SSRA na tunayapinga  mabadiliko haya kwa nguvu zote  kwani watakaoathirika na kanuni hiyo ni walimu ambao ni watoto wetu.

“Eneo lingine ambalo ni kero kwetu ni walimu Mkoa wa Dar es Salaam kutopandishwa madaraja kwa wakati, pia wanaostahili kupandishwa madaraja kwa mwaka husika sio wote wanaopandishwa na wanaopandishwa hawarekebishiwi mishahara yao,” alisema Kisenge.

Aliitaja kero nyingine kuwa ni Wakurugenzi wa Manispaa  kutotekeleza maagizo ya kupanua  wigo  wa madaraja  ya walimu kama yalivyoainishwa  kwenye waraka  wenye kumbukumbu namba CAC 2015/22801/D  ya Julai, 2014.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles