27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Makinda: Ninang’atuka

anne-makinda*Asema anafuata nyayo za Kikwete

*Ampisha Magufuli kuunda timu yake

 

Agatha Charles na Allen Msapi (GHI)

SPIKA wa Bunge la 10, Anne Makinda, jana alitangaza kustaafu wadhifa wake wa uspika kwa sababu ya umri kumtupa mkono.

Makinda alitangaza uamuzi huo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam.

Alisema ameamua kustaafu wadhifa wa uspika kwa sababu ya umri wake kuwa mkubwa na pia kupisha damu changa za wanasiasa vijana kushika wadhifa huo. Aidha, Makinda alisema ameamua kumpa nafasi Rais John Magufuli kuunda timu yake mwenyewe.

“Mimi maisha yangu yote nilikuwa bungeni na Oktoba nilitimiza miaka 40 ndani ya Bunge, sasa kwa sababu hiyo nimeamua kutogombea, Kikwete (Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete) ni rika langu, lakini amestaafu, na mimi nastaafu. Ni vizuri niachie wengine kwani ningekuwa nimestaafu miaka sita iliyopita. Hii itampa nafasi Rais wa sasa kuunda timu yake mwenyewe,” alisema Spika Makinda.

Akizungumzia nafasi alizopata kushika katika maisha yake bungeni, alisema katika kipindi cha miaka 40 ameshika nyadhfa za uenyekiti wa Bunge, Naibu Spika na Spika.

Akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari baada ya kutoa tangazo lake ya kuachia ngazi, Makinda alitoa maelezo ya kina kuhusu kustaafu kwake kwa kueleza kuwa kunatokana na taratibu za kidemokrasia nchini ambazo humtaka mwanasiasa au Spika kukaa katika kiti chake kwa miaka mitano kabla ya kuitisha uchaguzi mwingine.

“Kwa mujibu wa taratibu za demokrasia nchini wanasiasa wanatumikia miaka mitano ikiwemo nafasi ya uspika, lakini ukitaka unarudi lakini rasmi tunamaliza Novemba 17 atakapochaguliwa mwingine,” alisema Makinda.

Makinda alisema atashirikiana na uongozi utakaokuwepo na kwamba Bunge aliloliongoza limefanikiwa kuacha kanuni bora ambazo hata hivyo alisema zinaweza kubadilishwa.

Tathmini na mafanikio ya Bunge la 10

Akizungumzia tathimini ya utendaji kazi wa Bunge la 10, Makinda alisema anajivunia bunge hilo ambalo lilikuwa na changamoto nyingi na hoja mbalimbali zilizopitia kwenye Kamati za bunge ambazo ziliwaondoa baadhi ya mawaziri.

“Bunge la 10 kulikuwa na vijana wengi na tulijifunza na kuzoea. Walikuwa wachangamfu na lilikuwa Bunge zuri sana. Kuna kamati ziliwaondoa mawaziri kutokana na kanuni tulizozitunga wenyewe,” alisema Makinda.

Makinda alisema alipoingia Bunge la 10 alishtuka baada ya kuona wengi ni vijana, lakini aliwazoea kutokana na rika lao.

Alisema Bunge la 10 lilifanikiwa kubadili mzunguko na sheria ya Bajeti ambayo haikuwepo kwa kuwa Bajeti ya Serikali ilikuwa ikijadiliwa mwezi Juni kwa siku tano.

“Bajeti ilikuwa inajadiliwa siku tano, baada ya hapo mnapiga kelele hadi mwezi wa nane lakini katika Bunge hili wabunge walibadili na ilitungwa sheria ya bajeti ambayo pia wabunge wana haki ya kubadilisha bajeti ya Wizara ya Fedha,” alisema Makinda.

Aliyataja mafanikio zaidi yaliyopatikana kwenye Bunge la 10 kuwa ni pamoja na uwepo wa huduma za afya karibu na Ofisi za Bunge, kuongezeka kwa makatibu wa Bunge hadi kufikia watatu, akiwemo wa huduma kwa wabunge na uendeshaji.

Alisema Bunge lilisaidia kuongeza idadi ya watumishi hadi kufikia 260, kupata ufahamu  kwa kila mbunge ndani na nje ya nchi pamoja na kufanikisha uwepo wa ofisi za Kamati na sehemu ya mazoezi.

Makinda alisema analikumbuka Bunge kwa  sababu alilifurahia kwa kuwa na wabunge machachari na wanaozijua vema kanuni.

“Wabunge wa Bunge la 10 walikuwa wanajua kanuni, nililifurahia sana Bunge kwa kuwa na mimi ninapenda ukorofi kidogo.

“Huwezi kupendelea, pale wana haki za kikanuni na ukiwabania wanainua kanuni mnashindana, nilifurahi kufanya kazi nao, ninawamisi sana,” alisema Makinda.

Bunge la 11

Akizungumzia sifa za mtu anayefaa kuwa Spika wa Bunge la 11, alisema anapaswa kuwa mtu atakayekabiliana na hali ya sasa, mtulivu na mwenye kujifunza aina na tabia mbalimbali za wabunge wake.

“Wabunge ni taasisi ya kubadilishana mawazo hivyo anapaswa kuwa ‘passion’, unatakiwa usiwe mwepesi wa kukasirika hata kimataifa tunajifunza hivyo,” alisema Spika Makinda.

Alisema kutakuwa na maelekezo ya taratibu za kibunge kabla ya kuanza kwa bunge pamoja na namna bora ya kujenga hoja.

Makinda alisema anaachana na uongozi ndani ya siasa, lakini si siasa kwa kuwa ni maisha ya kila siku na kuongeza kuwa atakuwa tayari kushirikiana na uongozi ujao wa Bunge wakati wowote utakapomhitaji.

Hali mbaya za wabunge

Akizungumzia hali ya maisha ya kawaida ya wabunge, Makinda alisema wana hali mbaya  kwa sababu hawana fedha za kutosha za kujikimu kimaisha tofauti na ambavyo imekuwa ikidaiwa.

“Wabunge hawana fedha, wana hali ngumu, wana madeni, wengine wameondoka kwenye nafasi zao na madeni pamoja na kwamba serikali inawasaidia mafuta na mshahara, lakini bado. Tuna mazungumzo nadhani yamefikia pazuri ili wajiunge na mfuko wa NSSF na hata kukopa huko kwa riba,” alisema Makinda.

Mgogoro wa Zanzibar

Kuhusu mgogoro wa Zanzibar, Makinda alisema ni wa Kikatiba, hivyo Bunge la Jamhuri ya Muungano halina mamlaka ya kuushughulikia.

“Ule mgogoro ni wa Kikatiba, sisi hatuna ‘mandate’ ya kulishughulikia suala hilo, wabunge wa Jamhuri wapo na wataendelea na Bunge, wale ni wawakilishi,” alisema Makinda.

Akizungumzia idadi kubwa ya wana CCM waliojitokeza kuwania nafasi ya uspika, alisema ndiyo kukua kwa demokrasia na kwamba watu wapya ndani ya Bunge watajifunza namna ya kuongoza.

Rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa wakati wa uhai wa Bunge la 10 ambalo Makinda aliliongoza, liliwang’oa baadhi ya mawaziri na watendaji wa serikali.

Kwa mujibu wa rekodi hiyo, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyokuwa chini ya uenyekiti wa James Lembeli, katika ripoti yake ya Operesheni Tokomeza ya mwaka 2013 iliwaangusha aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, David Mathayo, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki.

Aidha, Bunge la 10 kupitia ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Zitto Kabwe na Makamu wake akiwa marehemu Deo Filikunjombe kuhusu uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow iliwang’oa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Anna Tibaijuka na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles