22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Majambazi waiba Sh sifuri UDSM

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Na Agatha Charles, Dar es Salaam

MAJAMBAZI wawili jana wamesababisha hofu katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kufyatua risasi ovyo baada ya kumwibia kijana aliyekuwa akitoka Benki ya NBC bahasha isiyokuwa na fedha.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka chanzo chake kinachofanya kazi eneo hilo, zinasema kijana huyo akiwa karibu na tawi la NBC majambazi hayo yalimkwapua bahasha hiyo wakidhani ina fedha na kuanza kukimbia nayo.

Chanzo hicho kinasema majambazi hao walifika eneo la UDSM katika eneo la Utawala saa nane mchana wakiwa na pikipiki maarufu kama bodaboda.

“Walimbana kijana yule ambaye hata hivyo iligundulika kuwa bahasha hiyo haikuwa na chochote zaidi ya nyaraka zake, huku fedha aliyokuwa nayo kiasi cha shilingi 50,000 alikuwa tayari amelipa chuoni kwa ajili ya kujisajili,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alidai baada ya kufanikiwa kukwapua bahasha hiyo walikimbilia geti linaloelekea Ubungo Maji lakini hawakufanikiwa kutoka baada ya kukuta geti limefungwa.

Alisema baada ya kushindwa kupita huko walirudi njia waliyopitia awali kwa ajili ya kutaka kupita geti linalotokea Chuo cha Ardhi (AU) lakini nalo walikuta limefungwa.

Alisema baada ya kuona mageti yote yamefungwa ikawalazimu wakimbilie bondeni ambako nako walishindwa kupita kutokana na mto unaoelekea eneo la Makongo.

“Baada ya kukuta mto walirudi tena geti la Ardhi ambako waliendelea kutishia kwa kufyatua risasi ovyo ili wasikamatwe na hapo walifanikiwa kushuka na kufungua geti ambalo walipita na kutokomea,” alisema mtoa taarifa huyo.

Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura, ambaye alikiri watu kutishiwa maisha na watu hao.

Alisema tukio hilo lilitokea jana mchana lakini hakuna tukio la uporaji lililoripotiwa mbali na kutishia maisha.

“Hadi sasa hakuna aliyeripoti kuwa kuna ujambazi umetokea na mtu ameporwa kitu cha thamani, watu wameripoti kutishiwa maisha getini ambako walipiga risasi na watu walifungua geti kwa hofu,” alisema Wambura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles