Na ELIYA MBONEA-ARUSHA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka wataalamu wa halmashauri na washauri wa miradi, kuacha kutumia dhamana ya vyeo vyao kutengeneza chuki kwa makandarasi.
Agizo hilo alilitoa jana mjini hapa, alipozindua na kutembelea kiwanda cha kutengeneza bidhaa za plastiki cha Lodhia Plastics kilichopo Njiro.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko ya baadhi ya makandarasi waliodai wamekuwa wakilazimishwa na kutishwa na wahandisi wa halmashauri na washauri wa miradi wanaowataka wanunue mabomba ya plasiti kwa matumizi katika miradi ya maji kutoka viwanda vya Dar es Salaam na si Arusha.
Akizungumza kiwandani hapo, Majaliwa alisema haoni sababu ya halmashauri kushinikiza makandarasi wazawa hususani wa mkoani Arusha kununua mabomba ya plastiki kutoka nje ya mkoa huo.
Alisema ni vyema washauri wa miradi wakaacha kujielekeza katika kutanguliza chuki, badala yake wakahakikisha bidhaa zinazoletwa zimekidhi viwango kupitia Shirika la Viwango (TBS) na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO).
Majaliwa alisema kitendo cha kuwalazimisha makandarasi wanunue bidhaa zikiwamo mabomba ya plastiki yanayotengenezwa Arusha nje ya mkoa huo ni kitendo cha kuwaongezea gharama zisizokuwa na msingi wowote.
“Sisi Serikali tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kuenzi na kuvilinda viwanda vya ndani. Tunatamani kuona viwanda kama hiki vikiendelea kuanzishwa ili kusaidia ajira kwa wananchi, kodi kwenda serikalini,” alisema Majaliwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Sailesh Pandit, alieleza kwamba wanashindwa kuuza bidhaa zao katika miradi mikubwa ya maji iliyopo mkoani Arusha licha ya na TBS na ISO kutokana na hujuma wanazofanyiwa na baadhi ya wahandisi na washauri elekezi wa miradi.
“Imeshatokea mara kadhaa kwa makandarasi wanaotekeleza miradi kuzuiwa kununua mabomba ya maji kutoka Lodhia Plastics na badala yake hulazimishwa kununua mabomba kutoka nje ya mkoa,” alisema.