25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Viongozi wa dini imarisheni malezi kwa vijana

Na Mwandishi Wetu

Viongozi wa dini nchini wametakiwa kuendelea kuimarisha malezi na mafundisho ya kiroho kwa vijana ili kuepusha mmomonyoko wa maadili ili taifa liendelee kung’ara, kuheshimika na kusifika duniani kwa utulivu, amani na umoja. 

 Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa, leo Ijumaa Julai 5, jijini Dodoma wakati alipomwakilisha Rais Dk. John Magufuli kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 53 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ulioambatana na harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa kitega uchumi cha jumuiya hiyo.

Amesema Serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini ikiwamo CCT katika kutengeneza mustakabali mwema na ustawi wa familia kupitia mahubiri ya injili na malezi ya kiroho.

“Kwa waumini mtakubaliana nami kuwa siku zote Taifa imara msingi wake hujengwa na familia imara, serikali inatambua mchango wa malezi ya kiroho katika ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla na mafundisho yake kwani yamesaidia kujenga watumishi wa umma ambao wamelelewa katika misingi bora ya kumcha Mwenyezi Mungu,” amesema.    

 Akizungumzia kuhusu harambee hiyo ambayo jumla ya Sh. milioni 357.35 zilipatikana, Waziri Mkuu amesema ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa CCT wa miaka mitano (2017 – 2022) wenye lengo la kuiwezesha jumuiya hiyo kujitegemea kwa kuwa na vitega uchumi vyake ambavyo vitawawezesha kujiendesha kwa asilimia 80.

 Waziri Mkuu amesema kwa msingi huo, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za CCT na madhehebu mengine ya dini katika kuwahudumia Watanzania kupitia sekta za elimu, maji, afya na shughuli za ujasiriamali

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Askofu, Alinikisa Cheyo, wakati akiwasili katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 53 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Amesema suala la kujitegemea ndiyo msingi wa uongozi wa Rais Dkt. Magufuli wa kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 na katika kufanikisha hilo, Serikali imeendelea kupunguza kiwango cha utegemezi.

“Kiwango cha utegemezi kutoka kwa washirika wa maendeleo katika bajeti kimepungua kutoka asilimia 12.5 mwaka 2017/2018 hadi asilimia nane 2019/2020, kuimarika huko kwa bajeti yetu kunakwenda sambamba na kuimarika kwa huduma za kijamii kama vile elimu, maji na kupungua kwa umaskini wa mahitaji muhimu,”amesema Majaliwa.

 Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Canon Moses Matonya, amesema jumuiya hiyo imeanzisha mkakati wa kuwa na vitega uchumi vyake kwa lengo kuondokana na utegemezi wa fedha za ufadhili ambazo zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles