31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wanasayansi wapata njia kutibu Ukimwi

*Majaribio yaliyofanywa yafanikiwa kwa asilimia 100

*Mamlaka zikiruhusu, tiba kuanza kutolewa mwakani

NEW YORK- MAREKANI

WATAFITI nchini Marekani wamesema wamefanikiwa kuondoa Virusi Vya Ukimwi kutoka kwenye vinasaba (DNA) vya panya, mafanikio ambayo wanasayansi wanasema  yanaweza kuwa hatua ya kwanza kuelekea tiba ngumu ya ugonjwa huo kwa binadamu.

Matokeo ya utafiti huo yaliyotangazwa wiki hii yamethibitishwa na wanasayansi zaidi ya 30  kutoka Vyuo Vikuu vya Temple na kile cha Tiba cha Nebraska.

Mmoja wa watafiti waandamizi aliyeshiriki katika utafiti huo Kamel Khalili  wa Chuo Kikuu cha Temple cha nchini Marekani amesema kutokana na mafanikio hayo endapo mamlaka za chakula na dawa zitathibtisha tiba hiyo kwa binadamu inaweza kuanza kutumika mapema mwaka ujao.

Watafiti hao wanasema hatua hiyo imewezekana kwa kuchanganya dawa za kufubaza maambukizi ya virusi na kifaa kinachoitwa CRISPR ambacho kinaweza kubadilisha jeni.

Watafiti hao waliondoa Virusi Vya Ukimwi katika panya 9 kati ya 23 ambao mifumo yao ya kinga ilibadilishwa kulingana na ile ya binadamu.

Khalili na wataalamu wengine wa Virusi Vya Ukimwi  wanasisitiza kuwa hatua hiyo ni kubwa kisayansi na matokeo yaliyoonekana kwa panya hao yanatoa mwanga wa tiba hiyo kufanikiwa kwa binadamu.

” Tulijua kile tulichohitaji kufanya, lakini teknolojia haikupatikana,” Khalili  aliliambia Washington Post, akisema timu yake ilikuwa ikisubiri nyenzo kama CRISPR ili kukabiliana na virusi.

Khalili alikaririwa na Washington Post akisema matokeo hayo yalikuwa ni ya kushangaza.

Ukimwi ni ugonjwa unaoathiri kinga ya mwili, hivi sasa unaweza kudhibitiwa tu kwa tiba inayojulikana kama ‘antiretroviral’ ambayo inafubaza virusi lakini haitibu.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha ugonjwa wa ukimwi umeathiri watu milioni 37 duniani kote.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka WHO watu milioni 22 ndio wanaotumia dawa hiyo za kufubaza virusi.  

WHO inasema  karibu watu milioni moja walikufa kwa magonjwa yanayoendana na Ukimwi  mwaka 2017.

Mapema mwaka huu, wanasayansi walionya juu ya  uthibitisho wa mtu wa pili aliyetangazwa kupona virusi vya ukimwi baada ya yule aliyetangazwa miaka 12  iliyopita, wakisema ilikuwa ni mapema mno kutangaza mtu huyo kupona.

Wagonjwa wote wawili waliotangazwa kupona awali walitibiwa kwa  ‘stem cell transplant’, matibabu ambayo watalaamu walisema ni hatari yanaweza kusababisha athari kwa upande mwingine na kuleta madhara makubwa  na walionya tiba hiyo kutopelekwa kwa watu wengine wengi.

MATIBABU YA SASA

Awali, kabla hawajafanikiwa kupata tiba kamili, timu ya Khalili huko Temple walibaini njia ya kuondoa Virusi vya Ukimwi kutoka kwenye DNA ya panya haikuweza kuondoa kabisa maambukizi.

Kwa sababu hiyo timu hiyo ya maabara ya Khalili iliunganisha nguvu na timu kutoka Chuo Kikuu cha Tiba Cha Nebraska (UNMC)  ili kuangalia njia tofauti ya kushambulia tatizo.

Kwa pamoja wanasayansi hayo walichanganya mbinu ya kubadilisha jeni kwa kutumia dawa iliyotengenezwa kushambulia Virusi Vya Ukimwi iliyotengenezwa na UNMC.

Howard Gendelman kutoka UNMC  aliiambia Washington Post kuwa dawa yao ya majaribio imeonekana kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi kuliko dawa za kawaida, maana yake ni kwamba inaweza kutumiwa kila miezi michache badala ya kila siku kama zilivyo dawa nyingine zinazotumika sasa.

Kwa sababu hiyo alisema dawa hiyo  imeonekana kurahisisha kazi iliyofanywa na timu ya Khalili ya kubadilisha jeni na hivyo kutokomeza Virusi vya Ukimwi.

“Ikiwa unaweza kupunguza kiasi cha virusi ambacho kinaachwa na CRISPR, uwezekano wa CRISPR kuwa na ufanisi zaidi  ukiendelea upo,” alisema.

Pamoja na hayo Khalili alisema yeye na timu yake wataweza kufanya majaribio kwa binadamu kwa kutumia dawa za kawaida hata kama zile zilizozalishwa katika maabara ya UNMC hazitaruhusiwa kwa matumizi .

Steven Deeks, Profesa wa Chuo Kikuu cha California kilichoko San Francisco ambaye amefanya kazi sana juu ya ugonjwa wa ukimwi, alisema kutumia njia ya kubadili jeni kuondoa Virusi vya Ukimwi   kutoka kwa mnyama aliye hai ni hatua kubwa ya mbele.

Lakini alionya kwamba kutumia njia hiyo kwa binadamu inaweza kuwa na changamoto zaidi.

“Wanasayansi watalazimika kukabiliana na tofauti nyingi za virusi, shida zaidi katika kutoa teknolojia ya kubadili jeni na zaidi uwezekano  wa kukata jeni za binadamu wakati wa kujaribu kulenga Virusi Vya Ukimwi,” alisema Deeks ambaye alisisitiza kuwa njia yenyewe iliyogundulika haina shaka isipokuwa utekelezaji wake.

Wakati wanasayansi wakija na taarifa hizo, Dk. Leonard  Maboko wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) akielezea hali ya maambukizi kwa hapa nchini alisema watu milioni 1.4 wanaoishi na ugonjwa huo nchini.

Alipotakiwa kutoa maoni kuhusu utafiti huo mpya, Dk Maboko alilitaka gazeti hili kuwasiliana na Wizara ya Afya kwa kuwa wao ndio wanaoshughulika na tiba na chanjo.

Gazeti hili liliwasiliana na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi lakini alimtaka mwandishi amtumie ujumbe mfupi lakini baadae alipopigiwa hakupatikana.

Walipotafutwa Wizara ya Afya kupitia kwa msemaji wao, Catherine Sungura alisema Waziri, Naibu na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo walikuwa kwenye mkutano.

Catherine alisema kwa uelewa wake tiba hiyo ni hadi pale WHO itakapoidhinisha ndipo nchi nyingine ziweze kutumia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles