22.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA, HUU NDIYO UKWELI WA LOLIONDO

majabungeni

Na Masyaga Matinyi

SEPTEMBA 23, 2013, aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akiwa Loliondo alitoa tamko lililoruhusu shughuli za kibinadamu katika eneo lote la Pori Tengefu Loliondo, bila kujali athari dhidi ya uhifadhi.

Tamko hilo la Pinda lilitengua tamko halali kisheria lilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Machi 19, 2013, lililoelekeza kupunguza ukubwa wa Pori Tengefu Loliondo kutoka kilomita za mraba 4,000 hadi kilomita za mraba 1,500.

Uharibifu mkubwa wa mazingira na mrundikano wa maelfu kwa maelfu ya mifugo ndani ya eneo hilo muhimu kwa mustakabali wa uhifadhi Tanzania unaoshuhudiwa hii leo, ni matokeo ya uamuzi wa Pinda ulioweka pembeni ushauri wa kitaalamu uliolenga kuliokoa eneo hilo.

Jumatatu ijayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kufika Loliondo ikiwa ni sehemu ya ziara yake kikazi mkoani Arusha.

Bila shaka yoyote Majaliwa atapata fursa ya kujionea yale ambayo wadau wa uhifadhi wamekuwa wakipaza sauti zao kila kukicha, kuwa Loliondo inakufa, Loliondo inakufa.

Hatuwezi kufahamu ni zipi ajenda za Majaliwa atakapokuwa Loliondo, lakini bila shaka yoyote ile, suala la mgogoro kati ya mwekezaji, wanavijiji, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), suala la mifugo, uharibifu wa mazingira, utata wa mpaka wa Hifadhi ya Serengeti na Loliondo na mengineyo mengi ya kweli na uongo yataibuka tu.

Wakati ziara hiyo ikisubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wote wa maendeleo Loliondo, ni vema kurejea au kukumbushana mambo machache, lengo kuu likiwa kuiona Loliondo ikirejea katika uasili wake.

Tamko la aliyekuwa Waziri, Balozi Kagasheki:

Ukweli ni kuwa Balozi Kagasheki alifuata sheria alipotoa tamko kuhusu kupunguza eneo la Pori Tangefu Loliondo kutoka  kilomita za mraba 4,000 hadi 1,500, na kuliacha eneo la kilomita za mraba 2,500 litumiwe na wananchi.

Alifanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009, Sehemu ya 16 Vifungu Na. 4, 5 na 6.

Sheria hiyo inampa waziri mwenye dhamana uwezo wa kupitia upya mapori tengefu na kufanya marekebisho mbalimbali muhimu kwa manufaa ya wananchi bila kuathiri uhifadhi.

Pia alifanya uamuzi huo kwa kuzingatia taarifa mbalimbali za utafiti na uchunguzi ambazo ziliwahi kufanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) na alizingatia mapendekezo ya tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza mgogoro uliopo.

Mojawapo ya tume hizo ni Tume ya Waziri Mkuu ya mwaka 2010, ambayo ilijumuisha wajumbe kutoka wizara nane, Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro.

Pamoja na mambo mengine, tume hiyo ilipendekeza kuwa kuna umuhimu wa kupunguza eneo la Pori Tengefu Loliondo bila kuathiri mapito ya wanyamapori na vyanzo vya maji.

Pia kwa muda viongozi wa wizara husika walikutana na wananchi na viongozi wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Ngorongoro kujua kero zilizopo ili zitatuliwe.

Mikutano hiyo ilimwezesha Kagasheki kufanya uamuzi alioufanya wa kuligawa eneo hilo la Pori Tengefu la Loliondo.

Umuhimu wa Pori Tengefu Loliondo:

Wizara ya Maliasili na Utalii ilisisitiza kuwa eneo la kilomita za mraba 1,500 litaendelea kuwa Pori Tengefu na kumilikiwa na wizara kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 kwa sababu zifuatazo: (i) Ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori (ii) Ni sehemu ya mapito ya wanyamapori (iii) Ni vyanzo vya maji.

Kutokana na sababu kuu tatu hizo, eneo hilo linapaswa kuendelea kuwa chini ya wizara, kwa kuwa linachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mfumo wa ikolojia ya Serengeti.

Maslahi ya wananchi yalizingatiwa:

Wizara ilisisitiza kuwa ardhi iliyobaki baada ya kuondoa eneo la Pori Tengefu la Loliondo itasimamiwa na vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999.

Pia wananchi watawezeshwa ili waanzishe Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika ardhi hiyo kwa manufaa yao.

Tanzania inajali uhifadhi, lakini pia inajali maslahi ya wananchi, ndiyo maana asilimia 25 ya ardhi ya nchi imehifadhiwa bila kuwapo migogoro.

Hakuna migogoro kati ya wananchi na Serikali, kwa kuwa wananchi wanatambua umuhimu wa uhifadhi kwao na kwa vizazi vijavyo. Ndiyo maana wananchi wanatakiwa kuchangia kwa kiwango kikubwa katika kufanikisha uhifadhi.

Pale ambapo kunajitokeza mgogoro kuhusu uhifadhi, Serikali na wadau husika hujadili na kufikia mwafaka.

Uchochezi wa migogoro Loliondo:

Tatizo la Lolindo tofauti na maeneo mengine ya hifadhi, ni kuwapo migogoro inayochochewa na wanaharakati na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), mengi yakiwa yanatoka nje nchi au kuongozwa na wageni.

Hata hivyo, ajenda ya siri ya asasi hizo ilishagundulika kuwa ni kupandikiza chuki kati ya mwekezaji katika eneo la Kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC), Serikali na wananchi kwa ujumla kwa manufaa ya wachache.

Wananchi wa Loliondo mara kadhaa wametakiwa kupuuza mbinu za wanaharakati hao ambazo hazina maslahi kwao, wala kwa uhifadhi na Taifa kwa ujumla.

NGOs hizo zina ofisi katika vijiji vilivyomo ndani ya Pori Tengefu ambavyo ni Ololosokwan, Soitsambu, Oloipir, Olorian Maiduguri, Losoito Maaloni, Arash na Piyaya.

NGOs hizo ni Tanzania Pastoralists Community Forum, Ujamaa-CRT, PINGO’s Forum, Tanzania Pastoralists Hunter Gatherers Organization, Pastoral Women Council, CORDS, PALISEP, NGONET na Maasai Pastoralist Development Organization – Lareto.

Kutokana na wingi wa asasi kulinganisha na ukubwa wa eneo husika, ndilo eneo lenye NGOs nyingi Tanzania, lakini wingi wa asasi hizo hauwiani na kiwango au kasi ya maendeleo ikiwamo elimu katika eneo hilo.

Juhudi za Serikali kutatua migogoro Loliondo:

Serikali kwa muda mrefu sasa imefanya mengi kujaribu kutatua migogoro ya ardhi katika Pori Tengefu Loliondo, ili kunusuru uhifadhi wa rasilimali za Taifa.

Rasilimali hizo ni pamoja na wanyamapori, ardhi oevu ambayo ni chanzo cha mito kama Grumeti, Pololeti na Lemugur ambayo ni vyanzo vya maji vinavyotegemewa na hifadhi za Taifa Serengeti na Ngorongoro, mazalia ya wanyamapori wanao hama kwa nyakati tofauti kutoka Mbuga ya Masai Mara katika nchi jirani ya Kenya kupitia Loliondo na hatimaye kuingia Serengeti na Ngorongoro.

Serikali imetuma tume mbalimbali kama Kamati ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Mazingira, Tume ya Waziri Mkuu iliyojumuisha wizara nane, ambapo tume zote zilipendekeza eneo hilo ligawanywe.

Chanzo cha migogoro:

Suala la migogoro katika eneo la Loliondo limekuwa la muda mrefu sasa, vyanzo vya migogoro ni vingi lakini kubwa zaidi ni ongezeko la idadi ya watu na mifugo.

Mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yameathiri kwa kiwango kikubwa uoto wa asili, hivyo kusababisha kiwango cha mvua kupungua mwaka hadi mwaka.

Hali hiyo imechangia kupungua kwa malisho ya mifugo na wanyamapori kwa kuwa majani hayaoti vya kutosha, hivyo kuwapo ushindani wa malisho kati wanyamapori na mifugo.

Pia wakazi wa kabila la Kimasai kubadilika kutoka ufugaji peke yake na kuanza kushughulika na kilimo, sheria zinzoongoza Tasnia ya Wanyamapori kukinzana na sheria ya Ardhi ya Vijiji, upotoshaji unaofanywa na NGOs na ukosefu wa uzalendo.

Nini kifanyike:

Mifugo yote inayomilikiwa na wakazi halali wa Loliondo iwekwe alama, ili kuitambua na kujua idadi kamili ya mifugo katika Wilaya ya Ngorongoro.

Kwa kufanya hivyo, itasaidia Serikali kujua idadi, kuboresha malisho, kutoa huduma bora ya mifugo na kudhibiti uingiaji holela ya mifugo.

Kufutwa kwa NGOs zilizopo Loliondo na kusajiliwa upya. Jambo hili litasaidia kuondoa migogoro ya Loliondo na kuweka mtazamo mpya kwa NGOs zitakazosajiliwa upya. Ni vyema kila shirika likaonyesha malengo na dira, ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Sheria ya wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 kwa sasa haifanyi kazi, hivyo ni vyema eneo la Loliondo likafanyiwa marekebisho kisera, ili kuweza kubaini maeneo ya vijiji na hifadhi kuondoa mkanganyiko uliopo sasa.

Kuwepo kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika eneo la Loliondo. Ardhi ya vijiji na hifadhi zibainishwe.

Karibu Loliondo Majaliwa, tunaamini busara, uwazi na uchapakazi wako usio na woga wala unafiki, utatoa suluhu ya kudumu Loliondo na kurejesha uasilia wake.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles