23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AWATOA HOFU WANAODAI FIDIA


Na Mwandishi Wetu - Songea

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewatoa hofu wakazi 1,000 wa Manispaa ya Songea wanaodai fidia ya Sh bilioni 3.8 baada ya eneo lao kuchukuliwa na kugeuzwa kuwa la kiuchumi (Ruvuma SEZ) kwa ujenzi wa viwanda.

Akizungumza mjini hapa jana na wakazi wa Kata ya Mwengemshindo katika mkutano wa hadhara, Majaliwa alisema Serikali inatambua kilio chao ambacho ni cha muda mrefu na alishawahi kupata ombi maalumu kutoka kwa Mbunge wao wa zamani, marehemu Leonidas Gama.

“Alipotoka kutibiwa India alikuja ofisini kwangu na kunieleza kwamba ana mambo mawili ambayo nikifanya ziara mkoani Ruvuma anaomba niyatafutie ufumbuzi. La kwanza ni hili la fidia kwa wakazi wa Mwengemshindo na la pili ni la ujenzi wa kituo cha mabasi cha mjini Songea.

“Leo (jana) nimefanya ziara maalumu kwa ajili yenu, kwa sababu Serikali iko kwa ajili yenu na hasa wananchi wanyonge. Na tatizo hili inalijua. Kabla sijafika hapa, nilipita kwenye eneo husika na ofisa mipango miji akanionyesha ramani ya eneo lenu hili,” alisema.

Pia aliwaeleza wakazi hao kwamba eneo hilo limetengwa na manispaa kwa ujenzi wa viwanda na kwamba wawekezaji watatu tayari wamekwishajitokeza na wanataka kujenga viwanda vitatu.

“Kutakuwa na kiwanda cha kusindika mahindi, kutengeneza pumba za kuku na ng’ombe na mbolea. Kiwanda cha pili kitakuwa ni cha kusindika kahawa na cha tatu kitakuwa ni cha kukamua mafuta ya mbegumbegu,” alisema na kuongeza kuwa reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay inatarajiwa kupita eneo hilo.

Kuhusu kuchelewa kwa malipo hayo, alisema kati ya wawekezaji hao watatu, aliyekwishalipa fidia ni mmoja tu na kwamba kwa mujibu wa sheria ya uwekezaji, fidia inapaswa kulipwa na mnunuzi wa eneo husika.

Hata hivyo, alikiri kuwapo kwa upungufu wakati wa ulipaji kwa sababu walifuata orodha ya majina (ki-alfabeti) badala ya kutoa malipo kwa wakazi wa eneo husika. “Sasa hivi mwekezaji anataka kuanza ujenzi, lakini ndani ya eneo lake kuna watu ambao bado hawajalipwa, kwahiyo hawawezi kutoka hadi wale waliobakia nao walipwe. Serikali itawafuatilia hawa wawekezaji wengine ili nao walipe fedha zao haraka ili waliobakia walipwe,” alisema.

Jumla ya watu 2,179 walifanyiwa uthamini mwaka 2008 na gharama yao kubainika kuwa ni Sh 3,254,737,622.

Juni 8-19, mwaka juzi, Serikali iliwalipa wakazi 1,179 jumla ya Sh 1,920,242,121 na kati ya hizo, Sh 1,210,078,261 zilikuwa ni malipo ya thamani ya mali za wananchi na Sh 710,163,860 zilikuwa ni riba kutokana na malipo hayo kuchelewa kufanyika.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alimwagiza Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Songea, Kundaeli Ndemfoo, afuatilie suala la bibi Monica Miti na watoto wake wanaodaiwa kudhulumiwa nyumba ya urithi na aliyekuwa mwanasheria wa manispaa hiyo.

Alitoa agizo hilo katika mkutano huo baada ya kupokea bango lililoandikwa na bibi Miti kuomba arejeshewe umiliki wa nyumba ya marehemu mumewe.

Alipopewa nafasi ya kueleza tatizo lake, bibi huyo aliyemtaja mwanasheria huyo kwa jina moja la Mwakasungura, alidai kuwa alighushi hati ya nyumba na kuwatoa ndani yeye na watoto wake.

Alipotakiwa na Majaliwa aeleze alipo mwanasheria huyo, Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Tina Sekambo, alijibu kwamba alishahamishiwa Ukerewe.

Majaliwa aliwaagiza Tina na Kundaeli wafuatilie suala hilo na wampe majibu mapema iwezekanavyo. Pia alimwomba bbi huyo na wanawe wafike kuonana naye Januari 3, mwakani atakapokuwa Songea kwa mapumziko mafupi ya mwisho wa mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles