27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

MKURUGENZI TANESCO ALIYETUMBULIWA APANGIWA KAZI NYINGINE


Na GABRIEL MUSHI -

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba, amepangiwa kazi nyingine ikiwa ni takribani miezi 12 imepita tangu alipotumbuliwa na Rais Dk. John Magufuli.

Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mramba Januari Mosi, mwaka huu bila kutaja nafasi nyingine aliyopaswa kupangiwa kwa kuwa ni mtumishi wa umma, huku nafasi yake ikichukuliwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Tito Esau.

Mramba ni mmoja kati ya vigogo waliorudishwa kazini baada ya aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, SACP Christopher Fuime aliyepewa cheo kingine, baada ya kusimamishwa kazi takriban miezi tisa iliyopita sambamba na askari wengine 11 waliotajwa kujishughulisha na biashara ya dawa za kulevya.

Kwa sasa Fuime anaongoza Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Kiuchumi ambacho ofisi zake zipo maeneo ya Kamata, Dar es Salaam.

Kitengo hicho ndicho ambacho hivi karibuni kilimhoji Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), kwa tuhuma za kutoa takwimu za ukuaji wa uchumi zinazopingana na zile za Serikali.

Kuhusu Mramba, taarifa zilizolifikia MTANZANIA Jumapili kwa nyakati tofauti kutoka kwa chanzo chake kimoja, zinasema kwamba kwa sasa amehamishiwa Chuo cha Tanesco (TSS) kilichopo Masaki, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ofisa mmoja mwandamizi aliyepo serikalini, alimpigia simu Mramba na kumuuliza iwapo kama ameshapata barua ya kurudishwa kazini na yeye alimjibu kwamba bado hajarudishwa.

Pia chanzo hicho kilisema kuwa ofisa huyo alimwambia Mramba kuwa tayari Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, ameshaandikiwa barua ampangie kazi nyingine.

Kutokana na taarifa hizo, MTANZANIA Jumapili lilizungumza na Mramba kwa simu, ambaye alisita kukubali au kukanusha kwamba amepangiwa kazi nyingine na kumtaka mwandishi kuwasiliana na mamlaka husika ili kupata ufafanuzi zaidi.

“Naomba nisijibu swali hilo, wajibu wanaohusika, mimi sina jibu lolote. Maswali hayo yajibiwe na wahusika, mimi sina la kujibu,” alisema Mramba.

Pia MTANZANIA Jumapili lilizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, ambaye alisema suala hilo linapaswa kutolewa ufafanuzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Dk. Alexander Kyaruzi.

MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta Dk. Kyaruzi, naye alisema kuwa Dk. Ndumbaro ndiye anatakiwa kutolea ufafanuzi suala hilo.

“Anayemrudisha kazini ni Katibu Mkuu Utumishi, yeye anaweza kukupa hizo taarifa kama amerudishwa ama la.

“Kwa mujibu wa utaratibu, anayempangia kazi ni Katibu Mkuu Kiongozi kwa sababu ni mteule wa rais, au anaweza kumwambia Katibu Mkuu Utumishi kuwa apangiwe kazi fulani, huo ndio utaratibu,” alisema Dk. Kyaruzi.

Katika hatua nyingine, MTANZANIA Jumapili lilifanikiwa kuzungumza na Dk. Ndumbaro ambaye alisema Tanesco na Mramba mwenyewe ndio wanajua kazi anayoifanya kwa sasa.

“Mramba mwenyewe ndiye anayejua kuwa yuko wapi saa hizi. Mramba mwenyewe ndiye anayejua kuwa anafanya kazi gani. Hakuna mtu ambaye kazi yake imefichwa kwa sababu kazi ya mtu si siri.

“Mimi siwezi kukutajia kuwa amepangiwa kazi gani kwa sababu watumishi wa umma wapo zaidi ya 500,000. Kwahiyo mimi sijui anafanya kazi gani. Mimi si msemaji wa kazi za watu wanazofanya,” alisema Dk. Ndumbaro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles