24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AMEJITOA SADAKA – MWIGULU

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba (kulia), akimnadi mgombea ubunge wa Jimbo la Longido kwa tiketi ya CCM, Dk. Steven Kiruswa, wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo jimboni humo uliofanyika Uwanja wa Longido jana (PICHA NA JANETH MUSHI)
Na JANETH MUSHI-LONGIDO -

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Rais Dk. John Magufuli amejitoa sadaka kwa Watanzania kwa kushughulikia masuala ya ufisadi na rasilimali za nchi.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana wakati akizindua kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) za uchaguzi mdogo wa nafasi ya ubunge katika Jimbo la Longido.

Pia alisema duniani kote hoja za msingi ambazo husimamiwa na watu wanaoipinga Serikali, ni masuala ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma na Magufuli amejitoa kwa masuala hayo, hivyo wanaoipinga Serikali wanakosea.

“Sasa rais amejitoa sadaka kwa ajili ya Watanzania, amejilipua kwenda mzima mzima, miguu yote, kushughulikia masuala hayo, ukikaa pembeni wakati masuala yamekaa sawa unapinga lipi lingine.

“Nikiwa kama mtaalamu wa uchumi, tuko kwenye njia sahihi kwa sera, uamuzi na hatua zinazochukuliwa, wengine wanaangalia matokeo ya hatua, wanataka kufanya kwenye ajenda, hawajui njia sahihi ni ipi wala hawajui uchumi,” alisema.

Mwigulu alisema katika njia sahihi za kiuchumi, huwezi kuwapandishia malipo watumishi, kuwapa ruzuku wakulima na wafugaji au kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi kwa fedha za kuomba au kukopa kwa sababu si njia endelevu.

“Unachofanya unatengeneza miundombinu ya uzalishaji ili utekeleze hayo, hayo ni mazingira ya kutengeneza uchumi endelevu,” alisema.

Kuhusu uchaguzi huo, aliwataka wananchi hao kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuwa Serikali itaongeza ulinzi katika uchaguzi huo na wanaotumia nafasi hiyo kufanya fujo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Mjitokeze kwa wingi mkapige kura, usalama upo wa uhakika wale ambao wanatumiaga uchaguzi kama sehemu za kufanya vurugu watakuwa wanatafuta matatizo, mara hii tutaangalia nani huwa anafanya fujo, tutakomesha uhuni ambao hufanyika, tutaongeza nguvu ya ulinzi, hakuna eneo la utekaji, wizi, ama vurugu ya aina yoyote, atakayefanya fujo anatafuta matatizo,” alisema.

Naye mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dk. Steven Kiruswa, aliwaomba wananchi wamchague na aliahidi kutatua kero zinazowakabili ikiwamo ya maji.

“Nawaomba mnichague, ninajua kero zenu, nitahakikisha kero kubwa ya maji inaisha, kila kijiji kitapata maji, kuna suala la mabadiliko ya tabianchi, nitalinda rasilimali ikiwamo ardhi, kusimamia mikopo kwa vijana na akina mama, najua uchaguzi huu ni muhimu baada ya kuonja joto ya jiwe kwa kukaa miaka miwili bila mbunge,” alisema.

Awali, aliyekuwa Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel, aliibuka katika uzinduzi huo na kupinga madai ya Chadema kuwa amenunuliwa na CCM ndiyo maana akajiuzulu na kuhamia chama hicho na alisisitiza kuwa amehama chama hicho kumuunga mkono Rais Magufuli.

“Wenzangu wana midomo mikubwa kuliko ubongo, wameishia kusema mambo ya kitoto nimewasaliti, si kweli, nimekuja  kuungana na rais anayetetea rasilimali za nchi, nimewakimbia kwa sababu hawana hoja za msingi.

“Nataka tuwaulize wanasema CCM inatununua, wao wanapingana ndiyo maana wanatetea mafisadi, wajiulize CCM wana ofisi kuanzia ngazi za juu hadi chini, wanalipa makatibu na viongozi wao, lakini wao wana ruzuku karibu shilingi milioni 360, tuwaulize wanamlipa nani?” alisema.

1,500 WAHAMA CHADEMA

Katika mkutano huo, wanachama zaidi ya 1,500 kutoka Chadema katika wilaya mbalimbali, zikiwamo Longido na Ngorongoro, walihamia CCM wakiongozwa na aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Ngorongoro mwaka juzi, Elias Ngorisa, ambaye pia alishawahi kuwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles