Mwandishi wetu-Lindi
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza warajisi wasaidizi wa ushirika katika mikoa yote inayolima korosho nchini, waandae semina kwa maofisa ushirika, viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS), maofisa ugani na wakulima kuwawezesha kubaini na kupanga korosho katika madaraja kuanzia ngazi ya vyama vya msingi.
Alisema jambo hilo litasaidia mkulima aweze kujua korosho aliyoipeleka ina ubora gani akiwa huko kijijini na wanapoifikisha kwenye ghala kuu wafanye kazi ya kuthibitisha.
Hatua hiyo itasaidia kuondoa malalamiko kuhusu madaraja, alisema .
“Hatua hii licha ya kuthibitisha ubora itasaidia kuboresha uzalishaji kwa vile wakulima wataelimishwa namna ya kuimarisha na kuboresha uzalishaji wa korosho nchini ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya viatilifu,’’alisema.
Majaliwa alisema hayo jauzi alipotembelea Kiwanda cha Korosho cha BUCO Manispaa ya Lindi, ambako alishuhudia korosho zikipimwa ubora kwenye ghala kuu kiwandani hapo.
Aliagiza semina ifanyike mwakani maofisa ushirika baada ya kupata mafunzo wawasaidie wakulima kwenye msimu ujao watambue korosho walizopeleka kuziuza zina ubora gani.
Waziri Mkuu alisema katika semina hiyo wakutane maofisa kilimo na maofisa ushirika wapate taaluma hiyo itakayowawezesha kupima korosho na kuitenga katika madaraja na kuwaondolea shida wakati wa mauzo.
Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Lindi, Robert Nsunza, alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba wataandaa semina hiyo kwa wahusika na kuanzia hapo wakulima watakuwa wakitambua ubora wa korosho zao kuanzia vijijini.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Nangomba Holdings, Ramadhan Katau, ambaye ndiye mtunzaji wa ghala la korosho katika kiwanda cha BUKO, alisema ghala hilo lina uwezo wa kupokea na kutunza tani 10,000 za korosho.
Alisema hadi sasa tani zilizopo ghalani hapo ni 6,370 na ukusanyaji wa korosho unaendelea kwa kuwa sasa ndiyo katikati ya msimu .