WAZIRI Mkuu, Kasim Mjaliwa, jana aliwaongoza maelfu ya wakazi wa mji wa Dodoma pamoja na mikoa mingine katika mazishi ya aliyekuwa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dodoma, marehemu Askofu Matias Isuja.
Askofu Isuja alifariki dunia wiki iliyopita katika Hospitali ya St. Gasper ya Itigi Manyoni mkoani Singida, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Marehemu Askofu Isuja ambaye alizikwa jana katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya utumbo.
Akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa alisema wakati wa uhai wake, Askofu Isuja alitoa mchango mkubwa kwa jamii ya watu wa Dodoma na nje.
Alisema wakati wa uhai wake, Askofu Isuja alikuwa na mchango mkubwa katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo maji, elimu na afya.
Alisema kifo chake ni pigo kubwa kwa wakatoliki na wasio wakatoliki, kwani wakati wa uhai wake hakubagua watu.
Alisema kinachotakiwa sasa ni kumwombea na kuendeleza yale yote mazuri ambayo aliyaanzisha.