24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AKEMEA MAKUNDI MANISPAA YA SONGEA

Na MWANDISHI WETU -SONGEA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewakemea watumishi wa umma na madiwani ambao wameunda makundi ndani ya Manispaa ya Songea kwa kuweka mbele masilahi yao binafsi na akawataka wajirekebishe mara moja.

Ametoa onyo hilo juzi wakati akizungumza na watumishi wa manispaa na madiwani kwenye kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Songea, mjini Songea mkoani Ruvuma.

“Watumishi wa umma ni lazima muelewe kwamba katika Halmashaurti zenu mnafanya kazi na waheshimiwa madiwani sababu mnatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na mnapotekeleza majukumu yenu mzingatie maslahi ya umma. Mnalo jukumu la kuhakikisha Halmashauri yenu inaongozwa kitaalamu.

“Nanyi waheshimiwa madiwani, mtambue kuwa mnaongoza wataalamu wa fani tofauti. Lakini hapa Songea, madiwani mmeigawa Halmashauri, mnaiendesha vibaya. Miradi haiendi vizuri kwa sababu mmejiingiza kwenye kujali maslahi yenu binafsi.

“Mmebishana sana katika miradi ya maji, ujenzi wa kituo cha mabasi kwa sababu kila mmoja anataka mtu wake aingie. Wakati mwingine pesa zinatumwa, nyie mnaanza kubishana tu, sasa ni mwisho. Mkitaka kutuangusha Serikali, ama tutawafukuza uanachama ama tutavunja Halmashauri,” alionya.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Tina Sekambo kwa uamuzi wake wa kuruhusu mradi mmoja uendelee baada ya kuona kuna malumbano ya kimaslahi miongoni mwa madiwani.

“Mkurugenzi chapa kazi, na usimwogope mtu yeyote, iwe ni diwani au mstahiki meya. Simamia sheria kama ulivyofanya kwenye mradi ambao ulileta maneno, ukaamua Naibu Meya asaini nyaraka, na mradi ukaendelea. Kisheria, Naibu Meya anaruhusiwa kusaini,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Serikali inakusanya kodi ili wananchi wapate maendeleo na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haina subira na mtu anayeharibu kazi.

Aliwaagiza Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa wasimamie kazi na yeyote atakayeleta uzembe, wamripoti kwake.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwonya Ofisa Elimu wa Manispaa hiyo, Edith Kangomba na kumtaka aache tabia ya kuchochea migomo kwa madiwani.

“Mkurugenzi wa manispaa mpe taarifa akirudi kwamba tutamfukuza kazi kwa sababu anashirikiana na baadhi ya madiwani kuleta migomo kwenye utekelezaji wa miradi. Mwambie leo ninamwomya, siku nyingine nitamfukuza hapa hapa kwenye kikao.

“Nasema hivi kwa sababu hao washirika wake, wako hapa hapa na wamesikia ujumbe huu. Serikali inahangaika, tunaleta fedha ajili ya elimu, lakini zikifika mnachaguana, na Manispaa yenu iko nyuma kielimu,” alielekeza Waziri Mkuu

Pamoja na hali hiyo aliwataka wakuu wa idara wasimamie idara zao na kuziongoza kwa uadilifu na kuwaeleza kuwa Serikali inatambua upungufu wa watumishi unaozikabili Halmashauri nyingi uliosababishwa na zoezi la uhakiki wa vyeti.

“Tunaajiri kidogo kidogo kwa awamu ili kuziba pengo la vyeti feki. Tunajua sekta za afya na elimu ndizo zimeathirika zaidi. Lakini nasisitiza tena, tunataka watumishi waadilifu, waaminifu na wawajibikaji. Endeleeni kuchapa kazi,” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles