Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameipa wiki mbili kuanzia jana (Ijumaa, Desemba 18, 2020) Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ihakikishe ifikapo Januari Mosi, mwakani Bandari ya kimkakati ya Kagunga iliyoko katika Kata ya Kagunga wilayani Kigoma iwe imeanza kutoa huduma.
“Leo nimekuja hapa kuona bandari, hii bandari ilikamilika mwaka 2017 imekaa tu, nyumba zimejaa popo tu na mle ndani kumejaa takataka na mmefagia jana baada ya kusikia mimi nakuja, hovyo kabisa nawauliza hapa wanajikanyaga tu tuna mtumishi hapa hakuna mtumishi amekuja jana badaa ya kusikia nakuja hovyo kabisa hawa,”
Majaliwa alitoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Desemba 18, 2020) baada ya kukagua mradi wa bandari ya Kagunga iliyopo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika, wilayani Kigoma.
Waziri Mkuu amechukizwa na kitendo cha bandari hiyo kushindwa kutoa huduma licha ya kuwa imekamilika.
Waziri Mkuu alisema mbali na bandari hiyo ya Kagunga kuanza kazi Januari Mosi, 2021, pia ameagiza soko la kisasa la Kagunga nalo lianze kazi siku hiyohiyo ili kuwawezesha wananchi wa Kagunga waanze kufanya biashara na kuinua kipato chao.
Pia, Waziri Mkuu ameshangwaza na kuchukizwa na kitendo cha Meneja wa Bandari kutoka Makao Makuu ya TPA ambaye hajawahi kufika katika bandari hiyo na haijui. “Kama kweli wewe ni Meneja wa Bandari Tanzania bandari zako huzijui na unamiaka chungunzima unafanya kazi gani, hovyo kabisa,” amesema Majaliwa.
Amesema mradi wa ujenzi wa bandari hiyo ulikamilika 2017 ukihusisha ujenzi wa jengo la abiria pamoja na la mizigo, nyumba ya kuishi mtumishi na jengo maalumu lakini hakuna mtumishi katika bandari hiyo ambayo ujenzi wake uligharimu Sh bilioni 3.8.