Na Elizabeth Kilindi, Njombe.
Mbunge wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe, Joseph Kamonga amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ludewa, Sanday Deogratius, kwa kuendelea kukuza kiwango cha ukusanyaji wa mapato.
Kamonga ameyasema hayo juzi wakati wa baraza la kwanza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Ludewa lililofanyika ukumbi wa halmashauri.
“Mwaka wa kwanza aliofika mkurugenzi alikusanya milioni 600 ,mwaka uliofuata alikusanya milioni 800 na mwaka huu amesema ana mpango wa kukusanya zaidi ya bilioni moja na mpaka sasa ameshafikisha asilimia 55,” amesema Kamonga.
Pia Kamonga amewataka madiwani na wakuu wa idara kuendelea kushirikiana ili kukuza mapato.
“Madiwani pamoja na wakuu wa idara mimi ni mtalaamu mwenzenu naomba tushirikiane ili kukuza zaidi mapato ya halmashauri yetu,’’amesema Kamonga.
Pia amesema katika swala la usafiri kwenye ziwa nyasa kutokana na kusimamishwa ataendelea kufuatilia ili kujua zaidi kuhusu usafiri huo.
“Kule ziwa Nyasa tunashukuru Rais (Dk. John Magufuli) alitutengenezea meli tatu lakini meli zile zilifanya safari moja halafu zikapaki, tunaendelea kufuatilia kuhakikisha wananchi waliotuchagua hatuwaangushi,” amesema.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mlangali Hamis Kayombo (CCM),a mesema wameyapokea yote waliyoaswa ikiwemo swala la mapato ambalo ndio msingi wa halmashauri.