29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aagiza ukaguzi mradi wa maji

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Bilinith Mahenge, ampeleke Ofisa Kilimo wa Mkoa Bernad Abraham, akakague mradi wa umwagiliaji wa Mpwayungu wilayani Chamwino  ili kubaini waliohusika na ubadhirifu wa Sh bilioni 1.2 za mradi huo.

Alitoa agizo hilo jana baada ya Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), kumwomba awasaidie kuhusu upotevu wa Sh bilioni 1.2 zilizotolewa kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji ambazo matumizi yake hayajulikani.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi wilayani Chamwino, Dodoma alipokea ombi hilo la mbunge huyo wakati akizungumza na wananchi wa Tarafa ya Mpwayungu, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mpwayungu.

Alisema mara baada ya Ofisa Kilimo, Abraham kukamilisha ukaguzi wa mradi huo wa umwagiliaji apelekewe taarifa ili waliohusika na ubadhirifu wa kiasi hicho cha fedha wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alivunja kamati ya kusimamia huduma ya maji ya kijiji hicho na alimwagiza Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Chamwino, Godfrey Mbabaye aunde kamati mpya.

Waziri Mkuu alichua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji wa kamati hiyo ambayo ilishindwa kutekeleza majukumu yake ikiwemo ujenzi wa vituo vya kuchotea maji licha ya kukusanya Sh milioni 20 kwa mwezi, mradi huo unavituo vinne tu.

Alisema kitendo cha kamati hiyo kushindwa kuongeza kujenga vituo vingine vya kuchotea maji licha ya kukusanya fedha nyingi kwa mwezi kinasababisha malalamiko kutoka kwa wananchi ambao ndio wanufaika wa mradi huo.

Pia Waziri Mkuu alimuagiza mhandisi huyo aombe taarifa ya akaunti ya benki ya mradi huo ili kubaini katika mfuko wa mradi huo una fedha kiasi gani na ndipo aunde kamati mpya ya maji ambayo anatakiwa ashirikishe wanawake kwa kuwa wao ndio wahusika wakuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles