25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MAHITA AMFUNDA IGP SIRRO

NA AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu, Omari Mahita, amesema moja ya vitu ambavyo IGP Simon Sirro anapaswa kuvifanyia kazi kwa sasa ni namna ya kushughulika na wanasiasa.

Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana baada ya IGP Sirro kuitisha kikao cha kawaida na kukutana na wakuu wa Jeshi la Polisi wastaafu, makamishna wa jeshi hilo wastaafu na waliopo kazini, ili kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali.

Mahita aliyestaafu mwaka 2006, alitambulika kwa jina la Ngunguri lililotokana na uwepo wa neno ngangari walilokuwa wakijiita viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) walipokuwa wakiandaa maandamano.

“Kuna changamoto nyingi, lakini niwe muwazi, changamoto ya kwanza ninayoiona ni namna ya ku-deal (kushughulika) na wanasiasa, ku-deal na wanasiasa ni kazi, lakini nafikiri tutaenda tu kwa mikakati tuliyoiweka,” alisema Mahita.

Mbali na hilo, pia kikao hicho kilichofanyika katika Bwalo la Polisi Oysterbay, kilikuwa na lengo la kubadilishana uzoefu na mbinu za kukabiliana na uhalifu nchini.

“Hakuna kikubwa zaidi, wametuita kujua ni namna gani wanaweza kupambana na uhalifu, kiongozi ukiwa nje ni kioo, sisi tunayaona mengi, tumekaa nje muda mrefu, mimi nipo nje mwaka wa 11 huu, tunaona na kusikia mengi, pia tumewaambia kasoro za kiutendaji na jinsi ya kuzirekebisha,” alisema Mahita.

Awali, IGP Sirro alisema kikao hicho kilikuwa na lengo la kukumbushana mambo ya msingi, ikiwamo suala la mafunzo kwa askari ili kufanya jeshi hilo kuwa imara.

“Walikumbushia mafunzo ili jeshi liwe imara, kila askari lazima apitie mafunzo mbalimbali, hasa mafunzo maalumu,” alisema.

Sirro alisema wastaafu hao wamesisitiza zaidi mafunzo ya mitandao ili jeshi liweze kwenda na wakati.

Pia alisema kulizungumziwa suala la weledi, huku ikidaiwa kuwapo na kasoro katika utendaji wa baadhi ya askari.

Alisema ili kuhakikisha wanakuwa na jeshi imara, wameanzisha utaratibu wa kukutana na wastaafu hao kila baada ya miezi miwili hadi mitatu kwa lengo kupata mrejesho wa kiutendaji.

Naye Kamanda wa Polisi mstaafu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, alisema kwa sasa jeshi hilo limekuwa na changamoto nyingi tofauti na ilivyokuwa zamani, hivyo zinapaswa kushughulikiwa kisasa.

“Sisi zamani changamoto hazikuwa nyingi, kila siku dunia inabadilika, mambo yanabadilika pamoja na mbinu za uhalifu, uhalifu upo, lakini mbinu zinategemea na wakati,” alisema Tibaigana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles