27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

BILIONEA ANUNUA NYUMBA YA LUGUMI MIL 700/-

Na AGATHA CHARLES – dar es salaam

HATIMAYE moja ya nyumba za mfanyabiashara Said Lugumi imeuzwa Sh milioni 700 kwa Kampuni ya Al-Naeem Enterprises Ltd katika mnada wa wazi uliofanyika Upanga, Dar es Salaam jana.

Kampuni ya Al-Naeem inayoongozwa na mfanyabiashara Haroon Zacharia, ilinunua nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Mazengo, Upanga kupitia mnada ulioendeshwa na Kampuni ya Yono Auction Mart & Co Ltd ili kufidia deni la kodi ya Sh bilioni 14 ambalo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaidai Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd.

Zacharia ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wa sukari hapa nchini ambaye mwaka jana, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilifanya ukaguzi katika maghala yake ili kubaini kama kuna sukari imefichwa.

Kampuni ya Yono kupitia wakurugenzi wake, Yono Kevela na Scholastika Kevela, pia waliendesha mnada katika nyumba mbili nyingine za Lugumi zilizoko eneo la Mbweni, Dar es Salaam, lakini hazikufanikiwa kuuzwa baada ya wanunuzi kushindwa kufikia bei inayotakiwa.

Baada ya mnada huo, Kevela, alisema katika nyumba hiyo ya Upanga lengo limetimia isipokuwa kwa nyumba za Mbweni zilizopata wateja kwa Sh milioni 460 na Sh milioni 440.

“Lengo hapa limetimia, huku ni mjini, katikati ya mji, hivyo wanunuzi ni haraka. Imekuwa rahisi tu na imevuka lengo letu tulilokuwa tumeweka, lakini Mbweni bado kuna utata. Waliofika bei ni shilingi milioni 460 na shilingi milioni 440 ambayo haijafikia lengo,” alisema Kevela.

Alipotakiwa kufafanua lengo lilikuwa ni bei gani kwa nyumba zote, aligoma na kudai kuwa kitakachofanyika ni kuwashawishi wateja hao walioonekana kukaribia kufikia lengo ili waweze kuongeza fedha.

“Tunawashawishi hao wakikubali tunamaliza kazi, wakishindwa itabidi turudie mnada,” alisema.

Kuhusu masharti ya mnada, Scholastika, alisema ni kulipa asilimia 25 ya thamani ya bei hapo hapo, huku asilimia 75 iliyobaki ikitakiwa kulipwa ndani ya siku 14 tangu kufanyika kwa mnada.

Awali, baada ya madalali na wateja kufika katika nyumba hiyo, ilikuwa imefungwa na walinzi wa Kampuni ya Suma JKT waliokuwa wanailinda, walijibu kuwa mtu aliyekuwa akiishi hapo amesafiri.

Baada ya majibu hayo, kampuni hiyo ya udadali iliyoambatana na askari polisi waliovaa kiraia na wengine sare za jeshi hilo, waliwataka walinzi hao kutoka nje na walitii kwa sababu nyumba hiyo tayari ilikuwa mikononi mwa TRA.

Gazeti hili liliacha wanunuzi hao wakiendelea kuandikishiana na kufuata utaratibu wa malipo, huku nyumba hiyo ikiwekwa walinzi wapya na madalali hao.

Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Huduma za Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alikaririwa akisema kuwa Lugumi anadaiwa kodi za aina mbalimbali zinazotokana na mapato yake pasipo kutaja idadi.

Lugumi alikuwa gumzo mwaka jana baada ya sakata la zabuni ya Sh bilioni 34 ya kuweka mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole kwa Jeshi la Polisi.

Katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilionyesha kuwa alilipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha za zabuni ili kuweka vifaa hivyo katika vituo 138 kote nchini, lakini hadi wakati wa ukaguzi vilikuwa vimewekwa 14 tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles