32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 12, 2024

Contact us: [email protected]

NENO LA KWANZA ALILOLITOA LISSU BAADA YA KUZINDUKA

Na Waandishi Wetu – dar es salaam

BAADA ya operesheni mbili tofauti zilizochukua takribani saa 17 kuokoa maisha ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), aliyeshambuliwa kwa risasi wiki hii na watu ambao vyombo vya dola bado havijawabaini, hatimaye juzi usiku alizinduka na kuzungumza maneno kadhaa.

Mkuu wa Idara ya Uenezi Chadema, Hemed Ali, miongoni mwa viongozi wa chama hicho waliofanikiwa kumwona Lissu kati ya saa 4 na 5 usiku wa kuamkia jana katika chumba maalumu cha uangalizi (ICU) alichowekwa katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa mwanasiasa huyo alimuuliza yuko wapi na amefikajefikaje.

Kauli hiyo ni wazi inaonyesha ni ama Lissu alikuwa hana kumbukumbu ya kilichokuwa kikiendelea kwa wakati wote wa takribani saa 17 tangu alipoingizwa chumba cha upasuaji wa kwanza hadi anaondolewa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na kupelekwa nchini Kenya.

Haijafahamika mara moja kama wakati huo wote alikuwa bado kwenye dawa ya usingizi au la!

Hemed alisema zaidi ya hayo, Lissu pia alihoji huku akiwa na kumbukumbu ya shambulizi la Dodoma kwamba ni akina nani waliompeleka huko.

“Nimetoka ICU, tena kama mtu wa mwisho kumwona mheshimiwa Lissu, nimeongea naye akinitambua kwa jina, akikumbuka kilichotokea Dodoma na kuniuliza alipo, kwa kweli Mungu ni mwema,” alisema Hemed kupitia ujumbe wake mfupi aliotuma usiku wa kuamkia jana.

Hemed pia alisema madaktari wamempa taarifa fupi inayoonyesha Lissu anaendelea vizuri kwa kila walichotegemea.

“Tuendelee kumwomba Mungu amponye haraka,” alisema Hemed ambaye aliungana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kufuatilia kwa ukaribu matibabu ya Lissu nchini Kenya.

Wakati Hemed akisema hayo, taarifa nyingine ambazo gazeti hili lilizipata jana kutoka katika Hospitali ya Nairobi zinaeleza kuwa matibabu ya Lissu huenda yakachukua muda mrefu kutokana na ukubwa wa shambulio.

Jana hadi kufikia mchana viongozi hao walikuwa hawajamwona, na taarifa zilieleza kuwa madaktari wanaomtibu walikuwa wakiendelea kumwangalia.

Mbowe jana alitegemewa kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya Lissu, lakini hakufanya hivyo.

 

MASWALI MAGUMU

Wakati hali ya Lissu ikielezwa kuwa na matumaini, tukio la kushambuliwa kwake kwa risasi takribani 30 akiwa ndani ya gari, siku chache baada ya kulalamika kuwa anafuatiliwa na gari aina ya Premio lenye namba za usajili T 460 CVQ, bado limeacha maswali magumu.

Gari hilo ambalo pia limetajwa kuwafuatilia baadhi ya wabunge kwa nyakati tofauti, akiwamo Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), bado kiza kimetanda kuhusu aina ya umiliki wake na anayelimiliki.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, juzi alisema hajawahi kupokea malalamiko yoyote kuhusu gari hilo, ambalo limetajwa kuambatana na mwanamke mmoja na wanaume wawili, na kwamba ndio kwanza alikuwa akizisikia habari hizo.

WABUNGE WAHOJIWA

Pengine kutokana na muktadha wa sasa, na hatua ya Spika wa Bunge, Job Ndugai juzi kuiagiza Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama ikutane na vyombo vya ulinzi na usalama ili kujadili hali ya usalama nchini, tayari baadhi ya wabunge wameanza kuhojiwa.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kuwa miongoni mwa walioitwa kuhojiwa ni Nape ingawa yeye mwenyewe alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo na madai yake kuhusu gari hilo kumfuatilia, alikataa kuzungumza chochote akisema kuwa ameamua kunyamaza kimya kwa kuwa mengi amekwishayasema.

Juzi, Spika Ndugai aliliambia Bunge kuwa taarifa itakayopatikana baada kamati hiyo kukutana na vyombo vya ulinzi na usalama, itawasilishwa bungeni kwa ajili ya mjadala kabla Bunge linaloendelea mjini hapa, halijaahirishwa mwishoni mwa wiki ijayo.

Agizo hilo la Spika lilitanguliwa na hoja iliyoibuliwa na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), kuomba awasilishe hoja ya dharura iliyohusu jinsi hali ya usalama ilivyo nchini baada ya uwepo wa matukio ya utekaji na matumizi mabaya ya silaha kwa baadhi ya watu.

“Kutokana na hali ilivyo, nashauri kamati ya ulinzi na usalama ya Bunge, ikae na vyombo vya ulinzi na usalama ili tuelezwe juu ya kinachoendelea, kwa sababu hadi sasa hakuna anayejua uhakika wa usalama wa maisha yake,” alisema Bashe na kuungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge waliosimama.

Nape juzi wakati akizungumza na mtandao mmoja wa kijamii, aliitaja gari hilo kuwa liliwahi kumfuatilia hata yeye miezi zaidi ya miwili iliyopita kabla ya kumsikia Lissu naye kudai linamfuatilia.

Alisema kuwa aliwahi kulifikisha suala hilo kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.

Nape alisema tukio la Lissu limemsikitisha kwa kuwa ni mmoja wa wabunge waliolalamika kufuatiliwa na magari, na akatoa hadi namba, rangi na idadi ya watu wanaomfuatilia, lakini hakuona hatua zozote zikichukuliwa na hivyo ikaonekana kama limepuuzwa hadi wiki hii alipopigwa risasi.

“Jambo hili si jambo dogo, Bunge limefanya uamuzi wa kulipeleka kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama, ninaamini baada ya pale hatua zitachukuliwa,” alikaririwa Nape na mtandao huo.

DEREVA WA LISSU, DK. MASHINJI WAITWA POLISI

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, limemtaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji na dereva aliyekuwa akiliendesha gari la Lissu siku ya tukio, ambaye gazeti hili limefanikiwa kupata jina lake moja tu la  Adam, wafike katika Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Dodoma au Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.

Jeshi la Polisi limetangaza uamuzi huo katika siku ambayo gazeti la MTANZANIA Jumamosi lilikuwa limebeba habari ya dereva huyo na kusema kuwa kwa sasa hayupo sawasawa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Gilles Muroto, alisema sababu za kumhoji Katibu Mkuu wa Chadema ni kutokana na kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kudai kuwa anawafahamu waliohusika katika tukio la kumpiga risasi Lissu.

“Jeshi la Polisi peke yake ndilo lililopewa jukumu la kufanya uchunguzi katika makosa yote ya jinai, kwa hiyo pia tunamtaka Vicent Mashinji ambaye pia ameonekana kwenye press conference jijini Dar es Salaam, ambaye anasema anafahamu waliofanya tukio hilo.

“Haitoshi kuongea na vyombo vya habari pekee, hivyo afike Dodoma katika Ofisi ya Upelelezi au Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi,” alisema.

Kuhusu dereva wa Lissu, Kamanda Muroto alisema walikuwa wakimtafuta bila mafanikio, lakini kwa sababu taarifa zake zimeandikwa na Gazeti MTANZANIA Jumamosi, basi ameanza kuonekana.

“Mheshimiwa Lissu alikuwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Adam, tangu tukio hili limetokea dereva huyu hatujamuona, sababu za kutokuonekana hazifahamiki, lakini tuna taarifa ameanza kuonekana na ametoa taarifa kwenye gazeti la Mtanzania la leo (jana),” alisema Kamanda Muroto huku akilionyesha gazeti hilo.

Aliongeza: “Amewezaje kufika Dar es Salaam asifike Dodoma ambako tukio limetokea? Kwa hiyo natoa notisi kwa dereva Adam afike Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Dodoma, au Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Dar es Salaam aje atupe taarifa za tukio hili, sisi Jeshi la Polisi tunaamini ni mtu muhimu na aliye na siri za tukio hili.

“Dereva kama alikuwepo hospitali, alipaswa kwenda polisi, yeye alikuwa ametoka salama, bosi wake ambaye ni mheshimiwa mbunge amejeruhiwa na yeye alikuwa pale, sasa angekuja kutueleza polisi kilichotokea.”

FAMILIA YA NAIBU SPIKA YAHOJIWA

Jeshi hilo la Polisi pia lilisema linaihoji familia ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Akson kutokana na tukio hilo kutokana na kuwa watu wa kwanza kuona tukio na kumkimbiza Lissu hospitali.

NAPE ATAKIWA KUPEKA NAMBA ZA GARI

Kamanda Muroto, pia alimtaka Nape kama anazijua namba za gari, basi awapatie ili ziweze kuwasaidia katika upelelezi wao.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo lilisema limewakamata watuhumiwa 30 kwa makosa mbalimbali mkoani Dodoma.

MAGARI MANANE YAKAMATWA

Zaidi jeshi hilo lilisema kuwa limeyakamata magari manane aina ya Nissan mara baada ya kutokea tukio hilo.

Gari aina hiyo jeupe, ndilo linalotajwa kutumiwa na mtu/watu waliomshambulia Lissu.

AIGUSA DUNIA

Taarifa  za kujeruhiwa Lissu, zimeonekana si tu  kugusa wanasiasa na watu wa kada tofauti hapa nchini, bali pia uso wa dunia kwani kwa siku tatu sasa mfululizo, kumekuwapo na matamko kutoka nchi mbalimbali na zaidi vyombo vya habari vya kimataifa vikiwamo Aljazeera na Shirika la Utangazaji la Uingereza – BBC vikiripoti kwa ukaribu tukio hilo.

Ubalozi wa Marekani nchini, umeliita tukio hilo ni la kijinga, Umoja wa Ulaya (EU) umetaka haki itendeke kwa kuwapata wahusika, ikiwa ni pamoja kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles