28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WIZARA YA NISHATI, MADINI YAKOSA WAZIRI KWA SIKU 110

 

Na MWANDISHI WETU

SASA ni wazi kuwa Wizara ya Nishati na Madini ni kaa la moto baada ya kutimiza siku 110, sawa na zaidi ya miezi mitatu, bila kuwa na waziri kamili.

Wizara hiyo imebaki bila kuwa na waziri tangu Mei 24, mwaka huu baada ya Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo aliyekuwa ameiongoza kwa takriban miaka miwili.

Rais Magufuli, alichukua uamuzi wa kutengua uteuzi wa Muhongo, baada ya kupokea ripoti ya kamati maalumu ya uchunguzi wa mchanga wa madini (makinikia) katika makontena 277 yaliyozuiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi kuyeyushwa, ili kupata kiwango cha madini yaliyomo, iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma.

Tangu uamuzi huo utolewe, wizara hiyo imebaki na Naibu Waziri, Dk. Medard Kalemani. Kuna taarifa zinadai kwamba Rais Magufuli bado anatafuta mtu imara wa kuiongoza.

Pia inadaiwa kuwa Rais Magufuli atajaza nafasi hiyo na za wizara nyingine zilizo wazi baada ya kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri au kuteua kutoka nje ya baraza. Hadi sasa kuna nafasi nne zilizo wazi katika Baraza la Mawaziri.

Mabadiliko hayo yanatajwa kufanywa kutokana na nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Abdallah Possi, ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa balozi nchini Ujerumani, alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu).

Nafasi nyingine zimeachwa na George Simbachawene, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi na Edwin Ngonyani, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambao walijiuzulu.

Mawaziri hao wawili walijiuzulu juzi baada ya kutajwa katika ripoti za Kamati Maalumu za Bunge zilizochunguza uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa madini ya almasi na tanzanite, ili kupisha uchunguzi zaidi unaofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Kamati hizo mbili zilizoundwa wakati wa mkutano wa saba wa Bunge la 11, ni ile iliyochunguza almasi iliyoongozwa na Mussa Zungu na ile ya tanzanite, ikiongozwa na Dotto Biteko.

Ripoti hizo zilizotolewa Jumatano ya wiki hii mjini Dodoma, zilipokewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliyezikabidhi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye naye alimkabidhi Rais Magufuli Ikulu, Dar es Salaam juzi.

Kutokana na nafasi hizo nne kuwa wazi katika Baraza la Mawaziri, ni wazi Rais Magufuli atapanga upya safu kwa kufanya mabadiliko makubwa, ili kwenda sambamba na kasi yake.

Itakumbukwa kuwa Machi, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri, aliloliunda Desemba 10, mwaka juzi, kwa kumteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, kuziba nafasi ya Dk. Harrison Mwakyembe, aliyepelekwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, iliyokuwa ikishikiliwa na Nape Nnauye.

Agosti, mwaka huu, Rais Magufuli alionyesha kutoridhishwa na kasi ya mawaziri watatu katika utekelezaji wa maagizo ya Serikali, akiwamo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, aliyeelezwa kuchelewa kuchukua uamuzi wa kunyang’anya viwanda kwa wasioviendeleza.

Mawaziri wengine ambao Magufuli hakuridhishwa na kasi zao, ni Dk. Charles Tizeba (Kilimo, Mifugo na Uvuvi) kwa kutofika Kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh kutatua matatizo waliyokuwa nayo na Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) kwa kushindwa kutoa uamuzi kwa mwaka mmoja kuhusu ujenzi wa ‘flow meters’ bandarini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles