30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

DOLA IFANYE KAZI, JAMII ISUBIRI MATOKEO

Na RACHEL MRISHO – DAR ES SALAM

MATUKIO ya uhalifu yanayoendelea yanaanza kuinajisi nchi yetu ambayo kwa miaka mingi imekuwa kinara wa kuhubiri amani.

Tumeshuhudia mjadala mkubwa uliotamalaki katika vyombo mbalimbali vya habari vya kitaifa na kimataifa kuhusu kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Tukio hilo bado linajadiliwa kwa mitazamo tofauti kutokana na namna watu hao wanaodaiwa kutofahamika walivyomvizia Lissu, kisha kulimiminia risasi takribani 30 gari alilokuwamo wakati anarejea nyumbani kwake Area D, akitokea bungeni, mjini Dodoma.

Taarifa za awali zilieleza kuwa miongoni mwa risasi hizo, tano zilimpata na kumjeruhi  miguuni, mkononi na tumboni.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kwa sasa yupo katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, akipigania uhai wake.

Bila shaka shambulio la Lissu halina tofauti na matukio mengine ya kihalifu yaliyopata kutokea nchini, yakiwamo kushambuliwa na kuuawa kwa askari na raia mbalimbali maeneo ya Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani na kwingineko.

Kufanana kwa matukio hayo kunatokana na neno uhalifu. Kinachotofautiana ni malengo au kiini cha shambulio kwa muhusika.

Lissu ni mwanasiasa, ana hulka ya kuzungumza mambo mbalimbali kutokana na nafasi yake ya kisiasa na kisheria. Hupenda kusimamia hoja zake anazoziamini bila kutetereka.

Kama hiyo haitoshi Lissu ni binadamu kama walivyo wengine, anaishi na watu ambao huenda hata yeye mwenyewe hawafahamu vizuri.

Bila kujali nani amedhuriwa, ametekwa amejeruhiwa au amefanyiwa unyama wa aina yoyote, msingi hapa ni kwamba uhalifu si jambo jema, unapaswa kukemewa kwa njia yoyote ile.

Hoja yangu inajielekeza katika msingi wa kuvishauri vyombo vya ulinzi na usalama kwanza kujenga uaminifu kwa jamii, hasa katika kushughulikia masuala ya uhalifu nchini bila kujali yanayozungumzwa.

Naamini vyombo hivyo vitatumia mbinu zilizotumika kuwanasa na kuusambaratisha mtandao wa kihalifu wa Kibiti, pia naamini zitatumika mbinu zilezile zilizowezesha kupatikana mtekaji wa watoto.

Kwa upande wa jamii niiase tu kutojihusisha na utoaji wa taarifa zisizo sahihi za matukio ya kiuhalifu au kuhusisha uhalifu na masuala yoyote, badala yake waviachie vyombo vya usalama vifanye kazi yake.

Bila shaka jamii ikifanya hivyo itasaidia vyombo hivyo kufanya uchunguzi sahihi, kutoa taarifa sahihi na kuwanasa wahusika sahihi.

Tujitafakari kwa moyo tupunguze kuyatoa ya moyoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles