ADDIS ABABA, ETHIOPIA
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Chad, Moussa Faki Mahamat amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), akimshinda Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Balozi Amina Mohamed baada ya upigaji kura uliochukua raundi nane.
Mahamat, alishinda kwa kura 12 baada ya kupata kura 38 dhidi ya 26 za Amina kufuatia raundi saba za upigaji kura mjini hapa jana.
Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Chad (56), anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Nkosazana Dlamini-Zuma wa Afrika Kusini, ambaye aliamua kutogombea tena.
Kushindwa kwa Balozi Amina ni pigo kubwa kwa Serikali ya Kenya iliyotumia nguvu na mamilioni ya shilingi kumpigia debe.
Katika kampeni hiyo iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, ilishuhudiwa wakizitembelea nchi nyingi za Afrika kuhakikisha Amina anaukwaa wadhifa huo.
Hata hivyo, Msemaji wa Ikulu ya Kenya, Manoah Esipisu, alisema Rais Kenyatta ambaye alishiriki uchaguzi huo jana na marais wenzake, alimpongeza mwenyekiti mpya kwa kupigana vyema katika kinyang’anyiro hicho na amemtakia kazi njema.
Amina, hata hivyo alifanikiwa kumshinda Dk. Abdoulauye Bathily wa Senegal, Mba Mokuy wa Guinea ya Ikweta, Pelonomi Venson Moitoi wa Botswana na kuingia fainali alikopambana na Mahamat.
Mahamat alikuwa mstari wa mbele kupambana na wanamgambo wenye itikadi kali nchini Nigeria, Mali na Niger na aliahidi ‘maendeleo na usalama’ kuwa kipaumbele chake kama bosi wa chombo hicho cha juu zaidi barani Afrika.
Alisema ana ndoto ya kuwa na Afrika, ambayo ‘milio ya risasi na mizinga itazibwa na mafuriko ya nyimbo za utamaduni na kelele za viwanda’ na kuahidi kuondoa ukiritimba AU wakati wa utawala wake wa miaka minne.