25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

NEEC YAWAPIGA MSASA WABUNGE  

Na Mwandishi Wetu-Dodoma


SERIKALI  imewataka wabunge  kuielewa dhana ya ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji (Local Content)  waweze kuwa  mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi kushiriki kwa ukamilifu kwenye shughuli za  uchumi na uwekezaji   nchini.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki   na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista  Mhagama ambaye aliwataka wabunge hao kuhakikisha wanatumia nafasi zao kutoa elimu kwa wananchi.

“Mafunzo haya yanayotolewa kwenu yatasaidia kuleta mabadiliko chanya na jamii itashirikishwa kwa ukamilifu katika uwekezaji unaofanyika katika maeneo yao kupitia kwenu  nyinyi wabunge,” alisema.

Alisema wakati umefika kwa Watanzania kuanza kunufaika  kutokana na uwekezaji na hatimaye uchumi wa nchi kukua.

“Ni muhimu wananchi waliopo katika sehemu ambako viwanda au miradi inaanzishwa kushirikishwa katika hatua za awali za uwekezaji au utekelezaji wa miradi,” alisema    Mhagama

Alisema mafunzo hayo kwa kamati mbalimbali za Bunge, pia yametoa nafasi kwa wabunge kutambua majukumu ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC)  ambalo ndilo lenye dhamana ya kuratibu shughuli zote za uwezeshaji nchini.

  Mwenyekiti wa Bodi ya NEEC, Dk. John Jingu, alisema uhusiano wa karibu kati ya wawekezaji na wananchi katika eneo  la mradi  unatakiwa kuimarishwa ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji wa miradi katika maeneo yao.

“Changamoto kubwa ni ujuzi wa wananchi wetu katika uwekezaji na ushiriki wao,” alisema Dk. Jingu na kuongeza kuwa Baraza limejipanga kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu ya namna bora ya kushiriki katika uwekezaji na kukuza uchumi wao.

Mbunge wa Muheza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu, alisema semina hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwao.

 “Tuna kila sababu za kuwaelimisha wananchi wetu juu ya kuongeza thamani ya bidhaa  waweze kuendana na matakwa ya wawekezaji,” alisema Balozi Adadi.

Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa, alisema lengo kubwa la semina hiyo kwa wabunge ni kuwafahamisha majukumu ya baraza na pia mchango wao katika dhana hiyo ya ushiriki wa wananchi katika uwekezaji.

“Wabunge wanatoka katika halmashauri ambako miradi inafanyika, hivyo italeta wepesi kwao kusimamia utekelezaji wa dhana hii   itakapoanza,” alisema Beng’i.

Wajumbe 152 wa kamati za Bunge walihudhuria semina hiyo iliyoratibiwa na NEEC na kudhaminiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles