NEW YORK, Marekani
WAZAZI wawili mjini New York nchini Marekani wamefanikiwa kushinda kesi waliyokuwa wakipambana nayo ili kumuondoa kijana wao mwenye umri wa miaka 30 nyumbani kwao, baada ya kukaidi kuondoka
Kesi hiyo iliamriwa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Donald Greenwood na akamueleza kijana huyo, Michael Rotondo, ombi lake la kutaka kuendelea kubaki nyumbani hapo kwa miezi sita zaidi haikubaliki
Katika mashtaka hayo ambayo waliyawakilisha wiki iliyopita, wazazi hao, Christina na Mark Rotondo walionesha nakala ya nyaraka walizokuwa wakimuamuru kuondoka nyumbani tangu Februari 2 mwaka huu na moja ya nakala ilikuwa ikimueleza kijana huyo kuwa kuna kazi zinapatikana hata kwa wenye historia ya tabia mbaya kama za kwake.
”Kuna kazi zinapatikana hata kwa wale wenye historia mbaya ya kufanya kazi kama wewe” ”Nenda katafute kazi-unapaswa kufanya kazi,”ilieleza moja ya nakala.
Mbali na nakala hizo, pia wazazi hao waliiambia mahakama kuwa wampatia dola za Marekani 1,100 ili aondoke nyumbani na wakamtaka auze baadhi ya vitu vyake ikiwemo gari yake mbovu aina ya Volkswagen Passat, lakini akakataa kuondoka.
Wakati wa kujitetea, Rotondo ambaye alijiwakilisha mwenyewe mahakamani, alisema kuwa mpaka sasa hafahamu ni kwa nini wazazi wake hawataki kusubiri kidogo ya kuondoka.
Alisema kuwa miezi sita ndio muda sahihi kwa mtu ambaye alikuwa akiwategemea watu kuweza kujiandaa ili akaanze maisha mapya.
Jaji akiwa anatabasamu alimtaka kijana huyo azungumze na wazazi wake,na kuamua kwa hiyari kuondoka nyumbani, lakini Rotondo alikataa.
Kwa mujibu wa Kituo Cha Televisheni cha ABC, hata hivyo pamoja na utetezi wake huo, Jaji Greenwood alimuwekea ngumu na kumuamru aondoke.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika shauri hilo,Rotondo alikiri kupokea kiasi hicho cha fedha na kukitumia na huku akikiri kutotoa msaada wowote katika familia na kisha akasema ataka rufaa kupinga hukumu hiyo na amepanga kuondoka nyumbani hapo baada ya miezi mitatu.