33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli kutumbua majipu ya kina Museveni, Kagame EAC

magufuli*Ni watendaji wa jumuiya hiyo watakaoharibu kazi
NA WAANDISHI WETU, ARUSHA/DAR
MWENYEKITI wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais Dk. John Magufuli, amehamishia kampeni yake ya kubana matumizi na kutumbua majipu kwa watendaji wa sekretarieti ya jumuiya hiyo watakaokiuka maadili ya kazi.
Amesema ikiwa kuna jambo litatokea kwa mtendaji yeyote, ataitisha kikao cha wakuu wa nchi za jumuiya hiyo na kuwaeleza suala hilo na ikiwezekana watendaji hao watatumbuliwa katika nchi zao.
Msimamo huo aliutoa jijini Arusha jana wakati mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika Hoteli ya Ngurudoto, ambako aliongezewa muda wa mwaka mmoja wa kuongoza jumuiya hiyo,baada ya wakuu wa nchi hizo kuridhia kwa kauli moja.
Kauli hiyo aliitoa mbele ya marais wa nchi wanachama wa jumuiy hiyo, Rais Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda), Uhuru Kenyatta (Kenya), Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, Joseph Butole na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Aliwataka watendaji wa sekretarieti kuhakikisha wanabana matumizi katika utendaji kazi wao wa kila siku.
“Nitahakikisha ninawafuatilia kwelikweli na endapo atabainika mtendaji wa sekretarieti anayekwenda kinyume na maadili, nitatoa taarifa kwa mkuu wake wa nchi ili atumbuliwe jipu.
“Nchi za Afrika Mashariki ni masikini, kwa hiyo sekretarieti wanatakiwa wajue wanafanya kazi ya watu masikini, hivyo wanatakiwa wabane matumizi wanapofanya vikao vyao au kuandaa mkutano wa wakuu wa nchi ili fedha nyingine zipelekwe katika masuala ya maendeleo ya jumuiya,” alisema Rais Magufuli.
Alisema sekretarieti inatakiwa kuandaa sheria na mambo ya kusaidia nchi na kuacha tabia ya kulalamika na badala yake wajikite katika kutafuta njia za kutatua matatizo yanayozikabili nchi wanachama.
“Tunataka tubane matumizi na si kuwa tegemezi, kwa mfano ukumbi tunaoutumia Ngurdoto ni wa hali ya juu, kila mtu mmoja anatozwa dola 45 (sawa na Sh 10,8000) wakati mkutano huu ungefanyika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa AICC kila mtu angetozwa dola 30 (sawa na Sh 72,000) punguzeni matumizi kwani fedha hizo zingeweza kununulia madawati kwenye shule mbalimbali, hususani za vijijini,” alisema Rais Dk. Magufuli.
Aliitaka sekretarieti kufanya kazi pasipo kuangalia matatizo yanayokabili nchi moja moja na badala yake wanatakiwa kuungana na kuyakabili kwa pamoja.
“Baada ya Sudan Kusini kuingizwa kwenye umoja huu, tumekuwa na watu karibu milioni 150 ambao tukishirikiana tunaweza kutatua matatizo ambayo yapo kwenye nchi moja moja, kama Sudan iliyo na njaa inaweza kupelekewa chakula na Tanzania iliyo na chakula kingi,” alisema.
Awali akifungua mkutano huo, Rais Magufuli alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki inatakiwa kukomesha tabia ya kutumia bidhaa wasizozalisha na kuzalisha wasizotumia hali inayosababisha kuwa tegemezi kwa nchi za Magharibi na Asia.
Alisema nchi hizo, zinatakiwa kuimarisha viwanda ikiwamo vya nguo na ngozi ambavyo malighafi yake inazalishwa kwa wingi miongoni mwa nchi za jumuiya hiyo.
“Afrika Mashariki tuna bahati ya kuwa na rasilimali za kutosha ikiwamo ardhi yenye rutuba, hivyo tukisimama na kushirikiana vizuri katika uendelezaji wa viwanda na kilimo, hatutategemea nchi za Magharibi kwa sababu tutakuwa tunajitosheleza kwa kila kitu,” alisema Rais Magufuli.
Alisitiza utekelezaji wa kuwa na lugha moja ambayo ni lugha ya Kiswahili na kusema ni moja ya zana ya kudumisha umoja, kupanua mawazo na kudumisha utamaduni.

MKAPA KUSULUHISHA BURUNDI
Pia Rais Dk. Magufuli, alitumia fursa hiyo pia kudokeza maazimio yaliyofikiwa na wakuu wa nchi wanachama, ikiwamo uteuzi wa Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa kuwa msuluhishi wa mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Burundi.
Alisema Mkapa atasaidiwa na mtangulizi wake katika kazi hiyo, Rais Museveni ili kuhakikisha wanakuwa na mazungumzo yatakayohusisha vyama vya upinzani na Serikali ya Rais Piere Nkurunziza wa Burundi katika kuleta amani nchini humo.
“Nampongeza Rais Museveni kwa jitihada zake za kurudisha amani nchini Burundi na tunawaomba wadau wengine kumuunga mkono katika kuhakikisha Burundi inarejea katika hali yake ya amani kwani bila amani hakuna maendeleo, ndiyo maana tumemteua Mkapa ili asaidie katika hilo,” alisema Rais Magufuli.
Alisema mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa EAC uliridhia kuiingiza Sudan Kusini katika jumuiya hiyo na kusema wanatarajia kuwa kuingizwa kwake kutakuwa chachu ya kuongeza kasi ya maendeleo ya jumuiya.

KATIBU MPYA
Kikao hicho kilichofanyika kwa mara ya kwanza chini ya uenyekiti Rais Dk. John Magufuli, kilimteua Liberate Mfumukeko wa Burundi kuwa Katibu Mkuu mpya wa jumuiya hiyo kuchukua nafasi ya Dk. Richard Sezibera wa Rwanda anayemaliza muda wake wa miaka mitano katika nafasi hiyo Aprili 20, mwaka huu.
Mfumukeko anakuwa mtendaji mkuu wa tano wa jumuiya hiyo tangu ilipoanza mwaka 1999.

SUDAN KUSINI WASHUKURU
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Sudan Kusini, James Wani Iga, aliishukuru EAC kwa kukubali ombi la nchi yake kujiunga na jumuiya hiyo licha ya kuwa ni taifa changa.
Alisema katika kipindi chote nchi yao itakuwa mwanachama mwaminifu na itashiriki kikamilifu katika kuiendeleza EAC.

Habari hii imeandaliwa na Janeth Mushi (Arusha), Jonas Mushi na Shabani Matutu (Dar)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles