MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema ikiwa atachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano Serikali yake itafuta makongamano na semina elekezi kwa watendaji wa Serikali ili kulinda fedha za umma.
Wakati akiyasema hayo kwenye mikutao aliyoifanya asubuhi katika Wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro, jioni akiwa kwenye mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri na kuhudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete, mgombea huyo alizidisha dakika 21 kwa kumaliza mkutano saa 12: 21 jioni badala ya saa 12:00 jioni inayotakiwa kisheria.
Wakati wa uzinduzi wa kampeni ya mgombea huyo uliofanyika katika viwanja vya Jangwani Dar es Salaam, Dk. Magufuli alizidisha dakika 33.
Akizungumza kwenye mikutano yake ya asubuhi jana , alisema, “haya yanayofanyika sasa ya makongamano na semina ni marufuku katika Serikali itakayoongozwa na Magufuli.
“Wananchi hawapati huduma fedha zao zinatumika kwenye shughuli hizi, tunasema tutazifuta. Kuendelea kufanyika mambo haya ni ufujaji wa fedha za umma,” alisema Dk. Magufuli
Alisema kutokana na hali hiyo hata baraza lake la mawaziri atakaloliunda litakuwa la watu wachache ambao watafanyakazi usiku na mchana kuhudumia wananchi.
Hivi sasa ni lazima wale watakaoteuliwa kuingia katika Baraza la Mawaziri wajiandae kufanya kazi na si vinginevyo, alisema.
Ujenzi wa viwanda
Dk. Magufuli alisema iwapo Watanzania watamchagua kuongoza nchi atahakikisha anajenga viwanda vikubwa na vidogo kukuza uchumi.
“Serikali yangu itakuwa rafiki kwa wananchi wote na katika hili ninapenda kusema hapa kuwa tutahakikisha tunajenga viwanda vikubwa na vya kati ambavyo vitasaidia kuchochea maendeleo.
“Kilosa ipo jirani na Wilaya ya Kilombero na hapa mnalima mpunga na miwa lakini bei ni tofauti na matarajio yenu wakati wa kuzalisha. Kwenye miwa kuna vyama vya msingi vinawanyonya wakulima.
Agoma kutoa hifadhi
Akiwa njiani kutokea wilayani Kilombero, msafara wake ulizuiwa na wananchi wa Kijiji cha Mkula ambao walikuwa na mabango wakimtaka atakapochaguliwa awape eneo la ardhi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa lakini aliwagomea kutekeleza ombi hilo.
“Napenda kusema ukweli sitaki kuvunja sheria na katu sitovunja kwa ombi lenu. Hii hifadhi ipo kwa mujibu wa sheria ndugu zangu,” alisisitiza.