25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa: JIPIMENI

ChopaNA MAREGESI PAUL, NZEGA

MGOMBEA Urais wa Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema kila Mtanzania anatakiwa kujipima   aone kama anastahili kukipigia kura Chama cha Mapinduzi (CCM).

Amesema  maisha ya Watanzania ni magumu na kila mmoja anatakiwa kumpigia kura yeye pamoja na wagombea wengine wanaounda  Ukawa kwa kuwa wamedhamiria kuboresha maisha ya Watanzania.

Lowassa ambaye pia aliwahi kuwa  Waziri Mkuu, aliyasema hayo jana mjini hapa alipohutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Laini Polisi mjini Nzega, Mkoa wa Tabora.

“Bado siku 49   muamue kama mnataka kuendelea kuishi bila elimu bora; bado siku 49 muamue kama mnataka kuishi bila maji; bado siku 49 muamue kama mnataka kulala kitanda gani hospitalini na vile vile bado siku 49 muamue kama mnataka kula mlo mmoja, miwili au milo mitatu kwa siku.

“Siku hizo zinakuja, tafakarini vizuri, angalieni nyuma tangu TANU itawale nchi hii hadi CCM ilipoanza kutawala umepata kitu gani?

“Jipimeni, angalieni nyuma kwa nini muendelee kuwa waoga, kwa nini mfanye uamuzi wa kupiga kura. Nipeni kura zenu nikafanye mabadiliko katika nchi hii kwa sababu tuko nyuma sana katika maendeleo.

“Mwambieni huyo aliyekopa tumbaku hapa Tabora  kwamba nikiingia madarakani tu  ile wiki ya pili atawalipa mara mbili kwa sababu nitaunda Serikali ya kisasa, sitaki Serikali nyoronyoro, nataka Serikali   inayokimbia.

“Lazima tusonge mbele, hatuna sababu ya kuzidiwa na Wakenya, hatuna sababu ya kuzidiwa na Wanyarwanda na pia nchi yetu haina sababu ya kuzidiwa na Waganda,” alisema Lowassa.

 

SUMAYE: Walioficha fedha nje watazirudisha

 

Naye Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye,   alisema kama Lowassa atafanikiwa kuingia madarakani Watanzania walioficha fedha nje ya nchi watazirudisha.

Kwa mujibu wa Sumaye, fedha hizo ambazo Serikali ya CCM imeshindwa kuzirudisha zitatakiwa kurudi kwa sababu ni mali ya Watanzania.

“Jana (juzi) mmemsikia Magufuli (Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli), akisema atakapoingia madarakani atarudisha mashamba ya wananchi yaliyoporwa.

“Kwanza kabisa namwambia Magufuli kwamba Ikulu haingii, lakini sisi tutakapoingia madarakani  tutahakikisha walioiba fedha za Watanzania na kuzificha huko Ulaya au Uswisi wanazirudisha,” alisema Sumaye.

Sumaye pia alizungumzia suala la rushwa nchini na kusema kama CCM wangekuwa waungwana wasingemsimamisha mtu yeyote kugombea urais kwa sababu wameshindwa kuwaletea maisha bora Watanzania.

“Magufuli anasema akiingia madarakani atakomesha rushwa sasa kama ana uwezo huo kwa nini ameshindwa kuikomesha wakati na yeye ni waziri katika Serikali iliyokithiri kwa rushwa?

“Magufuli anasema akiingia madarakani atakuza uchumi, kama kweli ana uwezo wa kukuza uchumi kwa nini ameshindwa kuukuza kupitia Serikali ya CCM ambayo yeye ni waziri?

“Magufuli hana lolote, msimchague kwa sababu ameshiriki kununua feri mbovu inayotoka Bagamoyo  kwenda Dar es Salaam,” alisema Sumaye.

Katika maelezo yake, Sumaye alizungumzia pia taarifa za viongozi wa CCM wanaodaiwa kuwatisha wananchi wasimchague Lowassa kwa kisingizio kwamba nchi itaingia katika vita kama ilivyotokea Libya na katika nchi nyingine za Afrika Kaskazini.

Sumaye alisema hakuna vita itakayotokea  wapinzani watakapoingia madarakani na kwamba vita hiyo itatokea kama Serikali ya CCM haitataka kuondoka madarakani.

 

MBOWE: Ulofa, upumbavu ni kwa sababu ya CCM

 

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema ili umasikini unaowakabili Watanzania uweze kuondoka lazima washirikiane kuiondoa madarakani CCM.

Alisema ulofa na upumbavu wanaodaiwa kuwa nao Watanzania umesababishwa na Serikali ya CCM kwa kuwa haiwajali Watanzania.

Mbowe alisema tofauti zao siasa walizokuwa nazo  walilazimika kuziacha na kuungana wakati wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu lengo lao ni kuing’oa CCM madarakani.

Mwenyekiti huyo wa Chadema alilazimika kuwapigisha kura za mikono wananchi wa Nzega waliohudhuria mkutano huo ili kutatua mvutano wa wagombea wa ubunge katika Jimbo la Nzega Mjini lililokuwa na wagombea wawili wa Ukawa.

Wakati wa kura hizo, mgombea wa Chadema, Charles Mabura, aliibuka mshindi dhidi ya mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Meza John.

Pamoja na mkutano huo, Lowassa alihutubia mikutano mingine ya kampeni katika Majimbo ya Bukene, Sikonge na Igunga mkoani Tabora.

Wakati huo huo, leo Lowassa anatarajia kulisimamisha tena jiji la Dar es Salaam  atakapohutubia mikutano ya kampeni katika Majimbo ya Kawe na Kibamba.

Lowassa atafanya mikutano hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu Ukawa walipozindua kampeni zao Agosti 29 mwaka huu katika Viwanja vya Jangwani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles